Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bosco Chuwa kuzikwa Ijumaa Khambaita, familia yatangaza ‘Bosco Night’ kumuenzi

Mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Bosco Chuwa enzi za uhai wake. 

Muktasari:

  • Kabla ya maziko, mwili wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa kampuni ya ujenzi mjini Moshi, Bosco Chuwa, utawasili nyumbani kwake Mtaa wa Khambaita, Kata ya Soweto Alhamisi jioni kwa ajili ya mkesha wa ibada uliopewa jina "Usiku wa Bosco" (Bosco Night).

Moshi. Mwili wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Bosco Chuwa (67), unatarajiwa kuzikwa Ijumaa ya wiki hii nyumbani kwake Mtaa wa Khambaita, Kata ya Soweto, Manispaa ya Moshi, huku Alhamisi kukifanyika kumbukizi maalumu iliyopewa jina la ‘Usiku wa Bosco’.

Bosco Chuwa alifariki dunia Jumapili, Julai 5, 2026 baada ya kuugua ghafla akiwa njiani. Kwa mujibu wa familia, Chuwa alisimamisha gari pembeni (haikuelezwa ni wapi) na kuwasha taa za tahadhari (hazard) baada ya kujisikia vibaya, ndipo watu waliokuwa karibu walipowasiliana na mmoja wa watoto wake, Junior Bosco, aliyefika eneo hilo na kumkuta akiwa katika hali mbaya.

Familia ilieleza jitihada zilifanyika kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu, lakini madaktari walishindwa kuokoa maisha yake na alifariki dunia.

Ratiba ya mazishi imetangazwa na msemaji wa familia, Allen Chuwa, aliyesema Alhamisi kutafanyika Bosco Night, ambapo mwili wa marehemu utalala nyumbani kwake Mtaa wa Kambaita na kutakuwa na ibada mbalimbali pamoja na nafasi kwa ndugu, jamaa, marafiki na wananchi kutoa heshima zao za mwisho.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 8, 2027, Allen amesema shughuli za mazishi zitaanza Ijumaa saa 3:00 asubuhi kwa ibada na kuaga mwili kabla ya maziko kufanyika katika eneo la nyumbani kwa marehemu  mtaa wa Kambaita kata ya Soweto Moshi.

"Mazishi yatafanyika Ijumaa. Kabla ya hapo, Alhamisi kutakuwa na Bosco Night. Mwili utalala hapa nyumbani na kutakuwa na ibada mbalimbali. Shughuli za mazishi zitaanza Ijumaa saa 3:00 asubuhi na kuendelea hadi maziko yatakapokamilika," amesema.

Amesema Bosco Night itakuwa wazi kwa wananchi wote wanaotaka kufika kumuenzi marehemu na kutoa pole kwa familia, akisisitiza kuwa si tukio la wanafamilia pekee.

"Watu wote wanakaribishwa, Alhamisi na Ijumaa pia. Wale wanaotaka kuja kuaga mwili na kutoa salamu za pole watapata nafasi ya kufanya hivyo," amesema Allen.

Ameongeza kuwa kutokana na mchango mkubwa alioutoa Bosco Chuwa katika sekta ya biashara na maendeleo ya jamii, familia inatarajia viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi na wadau wa biashara kuhudhuria mazishi hayo au kutuma wawakilishi wao.

Wakati huohuo, waombolezaji wanaoendelea kufika nyumbani kwa marehemu wameeleza kuwa kifo chake kimeacha pengo kubwa kutokana na mchango alioutoa kwa jamii.

Giliadi Kiwia aliyesema alifanya kazi na Bosco Chuwa kwa zaidi ya miaka 30, amesema marehemu alikuwa mtu wa watu, aliyependa kusaidia na kujenga mahusiano mazuri na kila aliyekutana naye.

Amesema alipokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa na hakutaka kuamini hadi alipothibitishiwa na mmoja wa watoto wa marehemu.

Naye Magdalena Kidumbuyo amesema anamfahamu Bosco Chuwa akiendesha teksi tangu miaka ya 1980 walipoanza kufanya biashara mjini Moshi akimtaja kuwa mtu mkarimu, mwenye upendo na aliyekuwa akiwathamini watu wote.

"Nilimuona mara ya mwisho Ijumaa iliyopita. Tulisalimiana na aliniuliza hali ya nyumbani kama alivyokuwa akifanya siku zote. Sikutegemea kwamba baada ya muda mfupi ningepokea taarifa za kifo chake," amesema Magdalena huku akiipa pole familia na kuwaombea nguvu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.