Boti yapinduka Ziwa Tanganyika, watumishi sita wa afya wafa maji
Muktasari:
- Watumishi sita wa Idara ya Afya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wamefariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka katika Ziwa Tanganyika wakati wakielekea kutoa huduma ya chanjo.
Kigoma. Watumishi sita wa Idara ya Afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, mkoani Kigoma wamefariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka katika Ziwa Tanganyika.
Watumishi hao walikuwa wakitoka Kigoma Mjini kuelekea Kijiji cha Kagunga kutoa huduma ya chanjo walipokumbwa na ajali hiyo iliyosababishwa na upepo mkali uliosababisha mawimbi makubwa ziwani.
Akizungumza katika eneo la tukio leo Ijumaa Machi 13, 2026, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma, Michael Maganga amesema tukio hilo lilitokea saa mbili asubuhi katika Kijiji cha Kalalangabo, Wilaya ya Kigoma.
Boti ambayo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma iliyokuwa imebeba watumishi wa halmashauri hiyo kutoka Kigoma mjini kwenda kijiji cha Kagunga kwa shughuli ya kutoa chanjo.
Maganga amesema pamoja na watu sita waliothibitika kufariki dunia na miili yao kupatikana, bado wengine watatu waliokuwa kwenye boti hiyo hawajapatikana hadi sasa na juhudi za kuwatafuta zinaendelea.
Amesema watu wengine tisa waliokuwamo katika boti hiyo wameokolewa na kwa sasa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni.
Kwa mujibu wa Maganga, chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali uliosababisha mawimbi makubwa yaliyoifanya boti hiyo kupinduka.
Mtumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma idara ya afya, Rachel Msalila aliyefariki dunia kwenye ajali ya boti.
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa mashuhuda aliyeshiriki katika uokoaji, Habibu Ibrahim, amesema waliona boti hiyo ikikimbia upepo ziwani kabla ya kupinduka.
Amesema wakati tukio linatokea walikuwa wametoka msikitini na kukaa kibarazani, ndipo walipoiona boti hiyo ikiingia katika eneo hilo la ziwa ikiwa inajaribu kukwepa upepo mkali.
“Baada ya muda tuliiona ikipinduka na kuzama. Tulichukua mitumbwi iliyokuwa karibu na kukimbilia ziwani umbali wa mita 40 kutoka ufukweni kuanza kuokoa watu waliokuwa ndani,” amesema Ibrahim ambaye ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Ziwani.
Mtumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma, Winifrida Bisunga aliyefariki dunia kwenye ajali ya boti.
Ameongeza kuwa baadhi ya waliopoteza maisha walikuwa ndani zaidi ya boti hiyo na walizuiwa kutoka haraka kutokana na turubai lililokuwa juu ya boti, huku wengi wao wakiwa hawajui kuogelea.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amefika katika eneo la tukio na kutoa pole kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma pamoja na familia za marehemu.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro akiwa na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kigoma mara baada ya kuwasili eneo la tukio.
Amesema Serikali iko pamoja na waathirika wa tukio hilo na itatoa msaada unaohitajika, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia taarifa za hali ya hewa na usalama wa vyombo vya usafiri vinavyotumika katika maeneo ya ziwa.
Amesema tukio hilo linapaswa kuwa funzo kwa wadau wote kuhakikisha usalama katika ukanda wa Ziwa Tanganyika unaimarishwa.