Brela yawataka wafanyabiashara kufuata sheria

Mkuu wa sehemu ya makampuni kutoka Brela, Isdor Nkindi
Arusha. Wamiliki wa kampuni mbalimbali nchini wametakiwa kufuata sheria na taratibu kwa kufanya biashara zao kwa njia halali badala ya kupitisha vitu vya kiuhalifu kwani sheria itawakamata.
Hayo yamesemwa leo machi 8,2023 jijini Arusha na Mkuu wa sehemu ya makampuni kutoka Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA), Isdor Nkindi wakati akizungumza katika majadiliano kuhusu utekelezaji wa kanuni za wamiliki manufaa baina ya wakala na vyombo vya uchunguzi.
Amesema lengo la majadiliano hayo ni kupeana elimu ya kiutendaji kama wadau wao wakubwa na watumiaji wa taarifa za
wamiliki manufaa kwani wote kwa pamoja wanategemeana sana katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi ya kila siku.
Amesema ilibainika kuwepo kwa baadhi ya kampuni ambayo hutengenezwa kwa nia mbaya ikiwemo kukwepa kodi na kufanya biashara haramu ikiwemo dawa za kulevya, hivyo amewataka wamiliki wa makampuni mbalimbali kuhakikisha wanafuata sheria na kuondokana na vitendo hivyo vya kiuhalifu.
Amesema BRELA wamekuwa wakishirikiana kwenye shughuli zao mbalimbali za kiutendaji kazi ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho mbalimbali ya kisheria na kimfumo ili kuhakikisha kwa niaba ya Serikali BRELA inatoa huduma bora kwao na umma kwa ujumla.
"Makampuni yana umuhimu mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi ambamo yanafanya kazi na hata uzoefu umeonyesha kwamba makampuni mengine yanatumika vibaya katika kufanya vitendo vya kihalifu visivyokubalika kwenye jamii ikiwa ni pamoja na utakatishaji wa fedha haramu, kufadhili vitendo vya
ugaidi, vitendo vya rushwa na hata ukwepaji wa kodi, hivyo tunawaomba sana wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja kwa sheria kali zitachukuliwa dhidi yao" amesema Nkindi.
Ameongeza ,Benki ya Dunia na Taasisi nyingine za Kimataifa zinazojihusisha na masuala ya kusaidia biashara zimejitolea kwa njia moja au nyingine kuleta mabadiliko ya hali hiyo kwa kuanzisha dhana ya Wamiliki Manufaa ambayo imeungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Uhamiaji mkoa wa Arusha, Beatrice Ngwijo amesema kupitia majadiliano hayo wameweza kujifunza kuhusu masuala mbalimbali kwani wamekuwa wakishirikiana na Brela katika kupata taarifa mbalimbali za watu wanaowapa kibali cha ukaazi kwa wawekezaji ambao ni wafanyabiashara.
Naye Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka, Eliainenyi Njiro amesema ofisi ya mashtaka ndiyo wanaohusika na kesi na wamebaini zipo kampuni zinazotumika kufanya udanganyifu hivyo kwa kutumia mafunzo hayo wataweza kuratibu upelelezi kwa weledi na kuweza kuzijua ni kampuni gani zifikiwe.
"Kupitia majadiliano haya tutaweza kuratibu upelelezi kwa weledi na kuhakikisha kuwa hakuna mtu yoyote atakayenufaika kupitia uhalifu kupitia makampuni yao," amesema Njiro.