Bulaya azipinga sheria, kanuni za mifuko ya hifadhi za jamii
Muktasari:
Mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya amedai Serikali ilikopa katika mifuko ya hifadhi za jamii Sh8 trilioni, kitendo cha kutolipa madeni hayo kinasababisha mifuko hiyo kushindwa kuwekeza
Dar es Salaam. Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya ameeleza namna machungu watakayoyapata watumishi baada ya utekelezaji wa Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ya Mwana 2017 na kanuni zake kuanza utekelezaji.
Kanuni hizo zilisainiwa Agosti 17 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama. Sheria ilianza kutumika Agosti Mosi baada ya Bunge kupitisha muswada ya kuiunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kubaki miwili ya NSSF na PSSSF.
Bulaya ambaye ni waziri kivuli wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu alizungumza na wanahabari kuhusu sintofahamu ya formula au kikokotoo cha 1/580 kilichopo kwenye kanuni za sheria hiyo.
Alisema kanuni hiyo inaeleza kila mstaafu atakuwa akilipwa asilimia 25 ya mafao kwa mkupuo na asilimia 75 inayobaki atalipwa kidogokidogo kila mwisho wa mwezi kama mshahara.
“Huku ni kuwavunja moyo wafanyakazi hasa wale wa madaraja ya chini. Hebu fikiria mtu unampa asilimia 25 unataka apate nini, wakati ile sheria ya mwanzo mstaafu alikuwa akikatwa asilimia 50 ya mafao na inayobaki analipwa kama mshahara hii sasa ni kiboko.”
Hata hivyo, Mwananchi linaelewa kuwa waliokuwa wanalipwa asilimia 50 ni watumishi wa Serikali tu kwani wale wa kampuni binafsi waliokuwa wakitumia NSSF walikuwa wakilipwa moja ya tatu kwa mkupuo, ambayo ilibadilishwa na kuwa asilimia 25 huku asilimia 75 ikibaki kwa ajili ya malipo ya kila mwezi.
Formula hii itafanya watumishi wa serikali na binafsi kutobaguliwa.
“Hatuwatendei haki wafanyakazi, nilikaa kimya muda mrefu bila kuzungumza hili nikajua Serikali itajirekebisha lakini mambo yamekuwa tofauti na nilivyotarajia,” alisema Bulaya.
Alisema kikokotoo hicho, kinawaweka katika sintofahamu watumishi, kinakandamiza na kuwaongezea uchungu kwa sababu wanakumbuka na changamoto mbalimbali ikiwemo kutopandishwa madaraja na mishahara.
Bulaya alimtaka Waziri Mhagama kujitokeza hadharani kuondoa sintofahamu ya suala hilo alilodai limewakumba na kuwachanganya wafanyakazi na wananchi.
Mwananchi lilimtafuta Waziri Mhagama kuhusu madai ya Bulaya lakini alisema yupo kikaoni na asingeweza kuongea lolote.
Pamoja na Waziri Mhagama kutakiwa kujitokeza kuzungumzia hatua hiyo, Bulaya alipendekeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo kutumia mamlaka yake ya kibunge kuziitisha haraka kanuni hizo ili kuhakikisha zinakidhi matakwa ya Katiba na zinazingatia maslahi ya nchi.
Katika mkutano huo na wanahabari uliofanyika makao makuu ya Chadema, Bulaya alidai Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii takribani Sh8 trilioni ambazo imezikopa kwenye mifuko hiyo.
Alisema deni hilo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambalo limetokana na Serikali na taasisi zake kukopa kwenye mifuko hiyo sanjari na kutopeleka michango ya wanachama.