Bweni la wavulana lateketea moto Ludewa

Muktasari:

  • Bweni la wanafunzi wa kiume Shule ya Sekondari Lugarawa wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe lateketea kwa moto usiku wa kuamkia Februari 15, 2023 na kusababisha uharibifu wa mali za wanafunzi.

Ludewa. Bweni la wavulana Shule ya Sekondari Lugarawa Wilayani Ludewa limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia Februari 15, 2023 na kupelekea uharibifu wa mali za wanafunzi na shule.

Akizungumza na Mwananchi Mkuu wa shule hiyo, Everine Somola amesema hakuna mwanafunzi aliyedhurika na janga hilo la moto zaidi ya vifaa vyao vya shule  kuteketea.

Amesema bweni hilo lilianza kuteketea saa tatu usiku huku chanzo cha moto huo kikisadikika kuwa ni hitilafu ya umeme.

“ Kwa mujibu wa maelezo ya wanafunzi walio shuhudia wamesema waliona moto unawaka kwenye (Main Switch ) huku kwingine ukiwa umetanda moshi,” amesema Somola.

Ameongeza kuwa moto huo ulibainika na wanafunzi waliokwenda kutazama usalama wa mali zao bwenini.

“ Tuna utaratibu tumeuweka wa wanafunzi kwenda kuangalia usalama wa mali zao bwenini kila baada ya saa moja, huwa wanatoka wanafunzi wawili kwenda kutazama,” amesema.

“ Wale watoto walipokwenda kutazama, ndipo walipo baini kuna moto bwenini kwao wakarudi halaka kuwataarifu walimu walio kuwa zamu na kwenda kuanza kuuzima kwa mchanga na maji,” amesema Somola.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Lugarawa, Erasto Mhagama amesema alipokea taarifa ya moto saa tatu usiku.

“ Nilipokea taarifa ya ajali hii ya moto saa 3 usiku, nikawapigia viongozi wenzangu tukaenda haraka kuuzima. Tulifanikiwa kuuzima lakini umeleta hasara kubwa kwa wanafunzi, vifaa vyao vya shule vimeteketea. Miongoni ni matandiko, mashuka, mablanketi na vitanda kwa asilimia kubwa,” amesema Mhagama.

Naye Sabinus Haule mkazi wa Kijiji cha Lugarawa, ameiomba Serikali kufanya maboresho ya mfumo wa umeme katika kata yao.

“ Tunaomba serikali iangalie huu umeme wa Kata ya Lugarawa umekuwa na matatizo kwa muda mrefu. Mfumo wa usambazaji sio mzuri, hii itakuja kuleta shida katika kata yetu na kata jirani zinazotegemea umeme kutoka kwetu,” amesema Haule.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi, Castory Kibasa amesema kwa tathmini ya haraka inahitajika Sh18 milioni kwaajili ya ukarabati na ununuzi wa vifaa vilivyoteketea kwa moto.

Ameongeza kuwa kwa hatua za awali halmashauri imenunua magodoro, mashuka na mablanketi kwaajili ya kuwasaidia katika maradhi wanafunzi hao huku hatua nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi.