CCM Tanga yaanza ‘kutroti’ uchaguzi serikali za mtaa 2024

Makamu wa pili wa Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ambaye pia ni mlezi wa Chama Cha mapinduzi mkoa wa Tanga Hemed Suleiman Abdulla. Picha na Raisa Said
Tanga. Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ametoa maagizo matatu kwa viongozi na wanachama wa Chama cha mapinduzi CCM Mkoani Tanga ikiwemo kuhakikisha ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.
Abdulla ambaye pia ni Mlezi wa Chama hicho mkoani hapa ametoa maagizo hayo mara baada ya kuwasili mkoani Tanga kwa ziara ya siku tano ya kuimarisha uhai wa Chama hicho katika ngazi ya mashina na matawi.
Maagizo hayo aliyoyatoa ni pamoja na kuweka mikakati kwa ajili ya kuhakikisha wanashinda katika chaguzi zijazo za serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
"kauli mbiu yetu mkoa wa Tanga tuko tayari kwaajili ya uchaguzi wa mwaka 2024,"amesema.
Agizo jingine ni kuwataka viongozi wa ngazi zote kuendelea kuzidisha umoja na mshikamano baina yao wenyewe kabla ya kwenda kwa wananchi nakwamba watakapo shikamana wanakwenda kwa wananchi wakiwa na lugha moja ya ushindi wa chama chao.
"Nikuombeni viongozi wa Mkoa wetu wa Tanga na wilaya zote Pale ambapo pana changamoto na sintofahamu za hapa na pale tuwekane sawa tuondoshe tofauti zetu twende tukasimame kwenye mstari ambao utawaongoza wanachama wetu kuelekea kukipigia kura chama chetu kwa ngazi zote nakuhakikisha tunashinda kwa kishindo," Amesema Mlezi huyo wa CCM mkoa wa Tanga
Mlezi huyo alisisitiza kuwa uchaguzi wa mwaka 2024 utawapa picha ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 nakuongeza kuwa mwenyekiti yoyote anayehisi kwenye kata yake atashindwa awasamehe mapema sababu hawako tayari kupoteza chochote katika uchaguzi huyo.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajabu Abrahaman amempongeza mlezi huyo kwa kufika mkoa wa Tanga nakusema mkoa huo hawata kubali kitongoji wala Kijiji kwenda upinzani nakwamba hata uchaguzi wa mwaka 2025 kata zote 245 na majimbo 12 ya uchaguzi yote yatakuwa chini ya CCM huku Rais Samia Suluhu watampa kura nyingi kuliko mkoa mwingine wowote.
Mwenyekiti huyo amesema kwa Sasa wanaendelea kukiimarisha chama chao kwanzia ngazi zote za mashina na matawi ndani ya mkoa huo.
Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa chama hicho wamesema wanamatarajio makubwa na ziara ya mlezi wao nakwamba itazidi kuwaimarisha .
Hata hivyo, mlezi huyo wa chama hicho mkoani hapa anatarajia kutembelea wilaya nane zilizopo mkoani Tanga kwa kufanya mikutano ya ndani ikiwemo kuongea na viongozi wa mashina na matawi wa Chama hicho.