CCM yataka korosho zisafirishwe kupitia bandari ya Dar es Salaam

Sunday October 31 2021
roshopic
By Mwanamkasi Jumbe

Mtwara. Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mtwara imeiagiza Serikali kuruhusu usafirishaji wa korosho kupitia bandari ya Dar es saalaam.

Taarifa hiyo ya CCM iliyotolewa jana Oktoba 30 baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa (NEC) kilichoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa wa Mtwara Yusuf Nannila, imesema kuwa jumla ya tani 45,000 zimeshanunuliwa zikisubiri meli ya mizigo inayotarajiwa kufika Mtwara kuanzia Novemba 7.

Aidha, Chama hicho pia kimeiagiza serikali kupitia mamlaka ya mapato nchini, TRA kuondoa tozo ya asilimia 2 kwa wakulima ambayo imetangazwa katika siku za hivi karibuni. 

Maagizo ya CCM Mkoa huo yametokana na malalamiko yaliyotolewa na vyama vikuu vya ushirika vinanyohudumia zao la korosho vya Tandahimba na Newala (Tanecu), Ruangwa na Nachingwea na Liwale (Runali), Masasi na Mtwara (Mamcu) na Lindi Mwambao hivi karibuni.

Taarifa ya maamuzi hayo ya halmashauri kuu CCM Mkoa imetolewa na Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa Mkoa wa Mtwara, Selemani Sankwa.

Itakumbukwa kuwa mnamo Juni 06, 2021 Serikali kupitia Waziri Mkuu ilielekeza kuwa korosho zote zinazozalishwa katika Mikoa ya Ruvuma, Lindi and Mtwara kusafirishwa kupitia bandari ya Mtwara kwa lengo la kuchagiza matumizi ya bandari hiyo ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Mkoa huo.

Advertisement

Maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa Bandari ya Mtwara yamegharimu kiasi cha Sh157.8 billioni, yakijumuisha ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa mita 385 na kuifanya kuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye urefu wa hadi mita 220 na uwezo wa kuhudumia shehena ya hadi tani milioni 1 kwa mwaka.

Ilitarajiwa kuwa bandari ya Mtwara ingesafirisha jumla ya tani 250,000 kati ya tani 280,000 zinazotarajiwa kuzalishwa katika msimu huu wa 2021/2022.

Advertisement