CEOrt yataka sekta binafsi kuonesha njia utekelezaji Dira 2050
Muktasari:
- Wito huo umetolewa katika mkutano wa kimkakati wa CEOrt uliokuwa na kaulimbiu "Zaidi ya Biashara Kimazoea: Kufikiria Upya Uongozi, Ubunifu na Mustakabali wa Tanzania," ambapo taasisi hiyo pia ilizindua mkakati wake mpya wa miaka mitano baada ya kukamilisha Mpango Mkakati wa 2022 hadi 2025.
Dar es Salaam. Jukwaa la Wakurugenzi Watendaji Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania – CEOrt) limeitaka sekta binafsi kuchukua nafasi kubwa katika kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Limeeleza ushiriki wa wafanyabiashara na wawekezaji utakuwa nguzo muhimu ya kufanikisha azma ya Tanzania kufikia uchumi wa thamani ya dola za Marekani trilioni moja.
Wito huo umetolewa jioni ya Julai 14, 2026 katika mkutano wa kimkakati wa CEOrt uliokuwa na kaulimbiu "Zaidi ya Biashara Kimazoea: Kufikiria Upya Uongozi, Ubunifu na Mustakabali wa Tanzania."
Aidha, taasisi hiyo ilizindua mkakati wake mpya wa miaka mitano baada ya kukamilisha Mpango Mkakati wa 2022 hadi 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Benson amesema mkakati huo mpya unaanza kutekelezwa wakati Tanzania imeanza safari ya utekelezaji wa Dira ya 2050, ambayo inaitazama sekta binafsi kama mhimili wa ukuaji wa uchumi.
Amesema matarajio ya sekta binafsi kuchangia takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa dira hiyo yanahitaji viongozi wa biashara kuacha kutoa ahadi pekee na kuanza kuweka mikakati itakayozalisha matokeo yanayopimika.
"Kumekuwa na kauli nyingi zenye matumaini kuhusu sekta binafsi kuchangia asilimia 70 katika uchumi wa Tanzania ifikapo mwaka 2050 na kusaidia kujenga uchumi wa dola trilioni moja. Swali ni je, tunaelewa kwa kina kinachohitajika kufanikisha azma hiyo na wajibu unaotutegemea," amehoji Benson.
Amesema viongozi wa biashara wanapaswa kufanya tathmini ya mchango wao katika kuongeza ushindani wa uchumi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuunga mkono sera zitakazochochea ukuaji endelevu.
Kwa mujibu wa Benson, mkakati mpya wa CEOrt umejikita katika vipaumbele sita vinavyolenga kuongeza thamani kwa wanachama, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika majadiliano ya sera, kukuza biashara zenye uwajibikaji na kupanua fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana.
Akizungumza katika mkutano huo, mwanzilishi wa kampuni ya magari ya umeme ya Kaypee Motors, Ali Masoud, maarufu Kipanya, amesema Tanzania inapaswa kujenga mazingira yatakayowawezesha wananchi kupata fursa za maendeleo ndani ya nchi badala ya kutegemea kuzitafuta nje.
Amesema mjadala unaoendelea duniani kuhusu uhamiaji wa kutafuta fursa unapaswa kuifanya Tanzania kujiuliza namna ya kuboresha mifumo yake ya kiuchumi na huduma ili kuwavutia na kuwabakiza wananchi wake.
"Pale Watanzania wanapoondoka kwenda kutafuta fursa katika nchi nyingine, tunapaswa kujiuliza kwa nini. Kama nchi nyingine zina mifumo bora na fursa nyingi zaidi, basi nasi tunapaswa kufanya nini ili Tanzania iwe mahali ambapo wananchi wanaweza kufanikiwa," amesema.
Masoud amesema jukumu lililopewa sekta binafsi kupitia Dira ya 2050 linapaswa kuwa chachu ya viongozi wa biashara kutafakari namna wanavyoendesha biashara zao na jinsi zinavyochangia ustawi wa taifa.
Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya CEOrt, David Nchimbi, amesema mkutano huo umetumika kutathmini utekelezaji wa mpango wa miaka minne uliopita na kuweka msingi wa mkakati mpya utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kupitia mkutano huo, wanachama na wadau wamepata fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kubadilishana uzoefu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha nafasi ya sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi.
Nchimbi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) amesema CEOrt itaendelea kuimarisha uongozi wa biashara, kuendeleza majadiliano kati ya Serikali na sekta binafsi na kuhamasisha biashara zenye uwajibikaji ili kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.