Chadema bado yakomaa madai ya Katiba mpya

Mwanza. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesisitiza umuhimu wa Katiba mpya itakayounda vyombo na taasisi huru, ikiwemo tume ya uchaguzi.

“Nimesikia wengi wakizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025, swali ninalojiuliza ni chaguzi hizo zitafanyika chini ya wasimamizi walewale waliowaengua wagombea wetu, utafanyika kwa sheria zilezile na Katiba ile ile?’’ alihoji Lissu.

Lissu alisema hayo jana alipohutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, Benson Kigaila aliunga mkono hoja ya Katiba mpya itakayowapa Watanzania haki ya kuchagua viongozi wao na kuondoa umasikini uliokithiri katikati ya utajiri wa rasilimali.

"Tunataka viongozi wanaotokana na kura za wananchi katika maeneo yao; mwenyekiti wa kitongoji, kijiji, diwani, mbunge na Rais watokane na kura. Hiyo itawezekana tu kwa kuwa na Katiba mpya na tume huru,’’ alisema Kigaila.

Mbowe na elimu

Nje ya Katiba, viongozi wa chama hicho, walizungumzia masuala mbali, huku Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akijikita katika suala la elimu hasa lugha ya kufundishia.

Alisema Kiingereza kinapaswa kuwa lugha ya kufundishia katika shule za umma na binafsi kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu.

“Kiswahili ni lugha ya Taifa kwa sababu inatuunganisha sote kwa umoja wetu… lakini kamwe hatutakiwi kupuuza Kiingereza kwa sababu ndicho Kiswahili cha dunia; ndiyo lugha inayounganisha dunia nzima na hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusisitiza hilo,’’ alisema Mbowe.

Alitoa mfano akisema Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda, licha ya kutumia lugha nyingine zikiwemo za asili na Kifaransa, pia zinatilia mkazo Kiingereza kuwezesha wahitimu wao kumudu ushindani katika soko la kimataifa.

‘’Sote tunashuhudia magari ya shule zenye rangi za njano ambazo ni maalumu kwa ajili ya watoto ambao wazazi wao wana uwezo kifedha ambao wanasoma kwenye shule za michepuo ya Kiingereza,’’ alisema.

Mbowe alisema matabaka kwenye sekta ya elimu yanaminya fursa ya ajira kwa wanafunzi wanaosoma shule za umma za msingi na sekondari katika mashirika na taasisi za kimataifa kwa kukosa ujuzi wa lugha hiyo.

Alisema Chadema inatambua juhudi zinazofanywa na Serikali kuboresha elimu ikiwemo mabadiliko ya sera, lakini yanapaswa kujikita kwenye lugha ya kufundishia itakayoweka usawa kwa wahitimu katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Heche, IGP Wambura na uhaini

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilius Wambura kuacha kuibua hofu miongoni mwa Watanzania kwa sababu hakuna chama wala kundi lolote lenye lengo ya kufanya vitendo vya uhaini wa kuiangusha Serikali, badala yake, Watanzania wataiondoa CCM madarakani kupitia sanduku la kura.

‘’Chadema hakina lengo la kumfanyia uhaini Rais Samia Suluhu Hassan, badala yake tutaing’oa CCM kupitia uchaguzi mkuu mwaka 2025,’’ alisema mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini akijibu tamko la Polisi kuhusu wanaotaka kuiangusha Serikali.

Kauli ya Heche alitokana na tamko la IGP Wambura la kuwaonya aliodai wanalenga kufanya uhaini kwa kuiondoa Serikali madarakani kwa njia ya maandamano.

Alitaja ukosefu wa ajira kwa vijana na umasikini uliokithiri miongoni mwa Watanzania katikati ya utajiri wa rasilimali ni moja ya sababu kuu za umma kuiondoa CCM madarakani kuanzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2025 na uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025.

Kaimu Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Sharifa Sulleiman aliutumia mkutano huo kuuasa uongozi wa Bavicha kuendelea kutekeleza wajibu wa kuwajenga na kuwalea vijana kuwa viongozi bora, imara, wenye weledi na uzalendo kwa Taifa lao.

"Vijana tutambue hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania. Ni lazima tuilinde na kulinda rasilimali zake kwa wivu mkubwa,’’ alisema Sharifa

Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu alitaja kero tatu zinazowakabili vijana nchini kuwa ni ukosefu wa ajira, matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali ikiwemo kuikabidhi mikononi mwa wageni kupitia uwekezaji na kukosekana kwa mfumo bora wa upatikanaji wa haki unaosababisha wasio na hatia kutiwa hatiani huku wenye hatia wakiachiwa huru.