Chadema waitwa kesi ya kina Mdee

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Tanzania imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufika mahakamani kesho katika kesi ya Halima Mdee na wenzake 18 wanaopinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho itakayotajwa mbele ya Jaji Cyprian Mkeha.


Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufika mahakamani kesho katika kesi ya Halima Mdee na wenzake 18 wanaopinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho itakayotajwa mbele ya Jaji Cyprian Mkeha.

Mdee, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake walifungua shauri hilo Julai 21 mwaka huu, ikiwa ni siku 13 baada ya kupata ridhaa ya mahakama hiyo.

Katika shauri hilo, wabunge hao wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 kuwavua uanachama, kwa utaratibu wa mapitio ya mahakama.

Juzi mahakama hiyo ilitoa hati ya wito ikiwataka wadaiwa katika shauri hilo kufika mahakamani kesho wakati shauri hilo litakapotajwa kwa ajili ya maelekezo muhimu, ikiwa ni hatua ya maandalizi ya usikilizwaji wake.

Mbali na Chadema kupitia Bodi yake ya Wadhamini waliosajiliwa, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye pia anasimama kwa niaba ya Bunge la Tanzania na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wakili wa kina Mdee, Ipilinga Panya, aliieleza Mwananchi juzi jioni kuwa walipata hati hiyo ya wito jioni kwa ajili ya kuwafikishia wadaiwa hao.

“Kwa hiyo kesho (jana) tutawa-serve (tutawapelekea hati ya wito) Chadema, AG na NEC,” amesema wakili Panya.

Katika shauri hilo namba 36 la mwaka 2022, Mdee na wenzakeo wanaowakilishwa na mawakili Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashi, wanaiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi wa Chadema kuwafukuza kisha itoe amri tatu.

Amri hizo ni kutengua mchakato na uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama, kuilazimisha Chadema kutimiza wajibu wake kisheria wa kuwapa haki ya kusikilizwa na amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuliwa.

Uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema ulitokana na rufaa walizozikata kina Mdee kupinga uamuzi wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu ya chama hicho, Novemba 27, 2020, iliyowatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu, bila ridhaa ya chama.

Katika shauri hilo, kina Mdee pamoja na mambo mengine wanadai kuwa mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama haukuzingatia matakwa ya kisheria na misingi ya haki, wakidai kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa, kuanzia Kamati Kuu mpaka Baraza Kuu walikokata rufaa.

Pia wanadai kuwa walifukuzwa kwa makosa yasiyo na maana na yasiyoweza kuthibitika, kuwa walikula njama kujiteua mwenyewe na kuapa kuwa wabunge wa viti maalumu.

Katika kiapo chake, Mdee anadai kuwa mara tu baada ya kula kiapo, Novemba 24, 2020 Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alimtaja yeye na wenzake kama wasaliti, huku wakiitwa Covid-19 na kwamba walishahukumiwa na viongozi wa chama hicho hata kabla ya vikao vya vyombo husika.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Esther Matiko na Ester Bulaya; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara na Cecilia Pareso.

Katika orodha hiyo, wamo pia Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.