Chadema yataka bajeti ihusishe mchakato Katiba mpya

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Vhadema, John Mnyika amesema bajeti iliyosomwa hivi karibuni bungeni jijini Dodoma haijaeleza lolote kuhusu utekelezaji wa takwa la Katiba mpya.

Dar es Salaam. Baada ya Serikali kuomba kuidhinishiwa Sh41.4 trilioni ikiwa ni bajeti ya mwaka 2022/23, Chadema imesema bajeti hiyo haiakisi mahitaji ya wananchi, kwa kutotenga wala kugusia mchakato wa Katiba Mpya ambalo ndilo hitaji la wengi.

  

Kauli hiyo imetolewa leo, Juni 19, 2022 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akichambua bajeti ya Serikali Makao Makuu ya chama hicho.

Mtendaji Mkuu huyo wa Chadema amesema, “Hii ni bajeti ya mwaka wa fedha unaoanza Julai mosi, 2022 hadi Juni 30 2023, tafsiri ya bajeti kutokuwa na vifungu maalumu vya kuendeleza na kukamilisha mchakato huo, maana yake kipindi chote hicho hakutakuwa na hatua za maana za kuufufua na kuukamilisha mchakato huo.”

Amefananisha mchakato huo ni sawa na daraja litakalofanikisha utawala bora na uimarishwaji wa demokrasia na kusisitiza kuwa Katiba mpya inapaswa kuingizwa kwenye bajeti kama mradi maalumu.

Hata hivyo, ameongeza kuwa matarajio ya wananchi yalikuwa ni hatua zaidi ya zilizoanza kufanywa juu ya kupunguza ukali wa gharama za maisha, lakini hilo halikutekelezwa zaidi ya kuendelezwa hatua ndogondogo zilizotangulia kuchukuliwa.

“Kwa tathmini yetu, Serikali imeamua kuendelea kuchukua hatua ndogo ya kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta na sio hatua zaidi,” amesema.

Amebainisha kuwa bado kilio cha tozo katika bidhaa ya mafuta kimeendelea na bajeti hiyo imeeleza juu juu kwamba itazipunguza bila kuonyesha mbinu na uhalisia wa utekelezaji wa hilo.

Mathalani, katika petrol, amesema tozo ni Sh920.68, dizeli Sh813 na mafuta ya taa ni Sh577, akibainisha kuwa hiyo inaondoa maana ya kubana matumizi kulikoelezwa na Serikali.