Chadema yaweka pingamizi maombi mapya ya kina Mdee

Muktasari:

Chadema imewawekea pingamizi akina Mdee katika maombi yao, ya amri ya muda ya mahakama kuizuia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Spika wa Bunge kuwavua ubunge baada ya chama hicho kuwavua uanachama.

Dar es Salaam. Chadema imewawekea pingamizi akina Halima Mdee na wenzake katika maombi yao, ya amri ya muda ya mahakama kuizuia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Spika wa Bunge kuwavua ubunge baada ya chama hicho kuwavua uanachama.

Pingamizi hilo la Chadema litasikilizwa Jumatano Juni 29, 2022 mchana.

Hata hivyo, Mahakama hiyo imetoa amri ya kuwa hadhi ya wabunge hao ibaki kama ilivyo mpaka siku ya usikilizwaji wa pingamizi hilo la Chadema.

Mdee na wenzake wamefungua maombi Mahakama Kuu dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema (iliyosajiliwa) wakiomba ridhaa ya kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema.

Sambamba na maombi hayo ya ridhaa namba 27 ya mwaka 2022, pia wamefungua maombi ya amri ya zuio dhidi ya NEC na Spika,  kutochukua hatua dhidi ya uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama.

Maombi hayo yaliyopangwa kusikilizwa na Jaji Mustapha Ismail  yametajwa leo Jumatatu Juni 27,2022, ndipo mawakili wa Chadema wakaibua pingamizi, dhidi ya maombi hayo ya zuio.

Katika pingamizi lake Chadema, inapinga usikilizwaji wa maombi hayo ikidai kiapo kinachoyaunga mkono kina kasoro za kisheria, huku wakibainisha hoja tatu za kasoro hizo.