Chama cha NRA chaita vijana kugombea nafasi za uongozi

Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha NRA, Hassan Almas (wa pili kutoka kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu chama chake kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 2025. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Wanawake wa chama hicho, Rachel Balama.
Muktasari:
- Chama cha NRA kimetangaza kutoa fomu za kugombea nafasi ya ubunge, udiwani na uraisi kwa wanawake na watu wenye ulemavu, zitatolewa bure bila malipo yoyote.
Dar es Salaam. Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) kimewataka vijana wenye nia ya kugombea wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
Chama hicho kimewatahadharisha wanachama wake na jamii kwa ujumla kujiepusha na unyanyasaji pamoja na vitendo vinavyosababisha uvunjifu wa amani ya nchi.
Katika chama hicho fomu za kugombea nafasi ya ubunge, udiwani na uraisi kwa wanawake na watu wenye ulemavu, zitatolewa bure bila malipo yoyote.
Katibu wa Mkuu wa NRA Taifa, Hassan Almas, amesema hayo, Mei 4, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu chama chake kushiriki uchaguzi mkuu sambamba na tamko kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Okotoba 2025.
“Tunaomba watazania kusikiliza viongozi wa kisiasa na kuwa makini kuchagua viongozi ambao watatua changamoto na kero za wananchi” amesema Almas na kuongeza,
“Wanachama wenzangu najua uchaguzi ni wa kistaarabu, hivyo mjiepushe na rushwa, unyayasaji na pia nawaomba kuheshimu katiba, sheria, taratibu za nchi, vyombo vya halali vya nchini na kujiandaa na kuwa wastaarabu katika kushiriki uchaguzi mkuu.”
Amesema kuwa chama hicho kinatakiwa kuwa tayari kupokea matokeo yatakayotokana na sanduku la kura.
Awali, Mwenyekiti wa Wanawake wa NRA, Rachel Balama, aliwataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa NRA Tanzania Bara, Mohamed Majaliwa amesema kipenga kimeshalia hivyo, yoyote anaweza kugombea achukua fomu ya kugombea nafasi mbalimbali.
“Zoezi la uchaguzi sio maigizo na sio kamari kwa sababu ndio zoezi ambalo mtu anatakiwa kuwa makini ili kupata viongozi bora na sio bora viongozi,” amesema Majaliwa.
Mwenyekiti wa Jumiuya ya watu wenye ulemavu, Nasra Kimo amesema yeye kama kiongozi wa watu wenye ulemavu anawataka watu wenye hali kama yake kujitokeza kwa kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali kwa kuwa chama kimewapa upendeleo mkubwa wa kupewa fomu za kugombea bure bila malipo yoyote.
Tayari chama hicho kimefungua pazia la kutoa fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenda kuchukua fomu ofisi kwao kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali.