Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Charles Hillary: Wawekezaji wazawa wamenirudisha TZ

Charles Hilary  akisisitiza jambo wakati wa mahojiano na mwandishi wa gazeti la Mwananchi .Picha na Venance Nestory

Muktasari:

Ziko redio nyingi zilizowahi kutangaza fainali hizo kwa Kiswahili, lakini zote zilifanya hivyo kwa kuangalia mechi hizo kwenye runinga na si kutokea uwanjani.

Dar es Salaam. Ilitokea, lakini haikuandikwa. Charles Hilary ndiye Mtanzania wa kwanza kutangaza kwa Kiswahili mechi za fainali za Kombe la Dunia akiwa uwanjani.

Ziko redio nyingi zilizowahi kutangaza fainali hizo kwa Kiswahili, lakini zote zilifanya hivyo kwa kuangalia mechi hizo kwenye runinga na si kutokea uwanjani.

Hilo ndilo linalomtofautisha mtangazaji huyo mkongwe wa zamani wa Redio Tanzania na watu wengine wote kwenye fani hiyo. Charles alikuwa ameshikilia microphone akiwa viwanjani.

Rekodi yake inanogeshwa na ukweli kwamba hata fainali hizo za Kombe la Dunia zilikuwa za kwanza kufanyika barani Afrika baada ya taifa la Afrika Kusini kupewa uenyeji wa michuano hiyo mikubwa katika mchezo wa soka duniani.

“Ilikuwa ni furaha zaidi kwangu,” anasema Hilary akikumbuka fainali hizo ambazo hushirikisha timu za taifa za wawakilishi wa mabara yote duniani.

“Mwaka 2010 ndiyo fainali za Kombe la Dunia zilifanyika kwa mara ya kwanza Afrika. Mimi nilikuwa Mtanzania pekee niliyepata nafasi ya kutangaza ‘live’ kwa Kiswahili. Sikutarajia. Hiki ni kitu cha furaha sana kwangu.

“Hakuna Mtanzania mwingine aliyewahi kutangaza ‘live’ na sijui kama itatokea tena hivi karibuni. Kwa kuweka kumbukumbu ya furaha hiyo nilinunua na kurejea na vitu mbalimbali ikiwamo mavuvuzela, nembo za timu za taifa ambazo manahodha wa timu hubadilishana na vitu vingine vingi.”

Hilary anaweza kutangaza vipindi vingine vingi, lakini anajulikana zaidi kutokana na umahiri wake wa kutangaza mpira, kuelezea mwenendo wa mchezo, kueleza haiba za wachezaji, lakini zaidi ana msamiati mkubwa, sitiari na misemo inaomtofautisha na watangazaji wengi wa enzi zake, akiwaacha mbali zaidi watangazaji vijana wa sasa.

Lakini gwiji huyo, ambaye baada ya kufanya kazi Ujerumani na Uingereza amerejea na kujiunga na Azam Media, sasa anasema wakati wake wa kuonyesha umahiri wake kwenye utangazaji mpira, umeisha.

“Mie tena, wakati wa mpira umefika ukingoni. Nimestaafu kutangaza soka, ila sasa nataka kufundisha vijana kutangaza,” anasema Hilary.

“Nilipokuwa Uingereza nilikuwa nawafuatilia (watangazaji mpira wa sasa). Wengi hawatangazi vizuri na sasa nimerudi jukumu langu ni kuwafundisha, sifa nilizopata kwa utangazaji kwa miaka 33 zinatosha,” anasema Hilary, mmoja wa watangazaji wa kwanza wa kituo cha Radio One Stereo alichojiunga nacho mwaka 1994.

“Tatizo katika utangazaji ni radio binafsi kutaa faida ya haraka. Hata hao wanaotangaza mpira ni juhudi zao, hawana A, B, C (mafunzo) za utangazaji; ni vurugu mechi. Wanazungumza sana, wanataka kuwa wachambuzi zaidi badala ya kutangaza.

“Lakini si kosa lao, kosa la wamiliki hawakuwatafuta watangazaji wakongwe kuomba ushauri ili kutoa maelekezo. Lakini sasa nipo Azam, ingawa kazi zinanibana, mtu akinitafuta nipo tayari. Ninawakaribisha, hata wakinipigia simu nitawaeleza cha kufanya.”

Hilary anaona kuwa wamiliki wa vyombo vya habari, hasa radio, wana wajibu wa kukuza ujuzi wa vijana angalu kwa kuwapeleka kwenye mafunzo kila baada ya miezi sita au mwaka, ndani hata nje ya nchi badala ya kujali faida.

Pia anaona watangazaji wengi vijana wanabweteka badala yake kujitahidi kujifunza kwa wengine ambao ni wakongwe kwa kuwa wana safari ndefu.

Hilary, ambaye pia aliasisi kipindi cha Charanga Time kilichomzidishia umaarufu akiwa Radio One Stereo, alizaliwa Zanzibar miaka 56 iliyopita eneo la Jang’ombe. Aliwahi kunusurika kuuawa kwa risasi mwaka 1964, siku moja baada ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoundoa utawala wa Sultan na kuiweka Serikali ya Watu wa Zanzibar.

Charles alikutwa na tukio hilo Januari 13 wakati akiwa na umri wa miaka mitano.

Mwaka 1968 alihamia jijini Dar es Salaam na kujiunga na Shule ya Msingi ya Ilala Mchikichini. Alijiunga na Redio Tanzania mwaka 1981 na kukitumikia chombo hicho cha umma hadi mwaka 1994 alipojiunga na kituo binafsi cha Radio One Stereo kinachomilikiwa na IPP.

Mwaka 2003 aliondoka nchini na kujiunga na Radio Deusch Welle na miaka mitatu baadaye alijiunga na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC akiwa Idhaa ya Kiswahili.

Akieleza sababu za kuondoka BBC kurejea nchini, Hilary anasema ni umakini wa wamiliki wazawa wa vyombo vya habari.

“Kilichonisukuma kuja hapa ni umakini wa wamiliki na jinsi Watanzania wenzetu walivyojitoa kuwekeza fedha nyingi kwenye mradi huu. Mimi nimekuja kusaidiana nao ili kuipa hadhi kubwa Azam katika habari za televisheni na redio itakayoanza Julai mwishoni na mimi ndiye mkurugenzi wake,” alisema mkongwe huyo.

“Wamiliki ni wazalendo, wapo serious (makini), hiyo imenivuta. Hebu fikiria nimekaa mika 15 nje ya Tanzania, miaka mitatu nilikaa Ujerumani Redio Deusch Welle na miaka tisa BBC, sasa nimevutika kwa Azam.”

Wakati mgumu michezoni

Miaka zaidi ya 30 kwenye tasnia ya habari haiwezi kupita bila ya matatizo, na Hilary alikumbana na hali ngumu kwenye kazi yake ya utangazaji.

“Kuna mengi lakini hasa siku ambayo Arsenal ilifungwa magoli 8-2 na Manchester United (katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza). Mechi hiyo nilitangaza miye, ulikuwa wakati mgumu sana, sana, sana,” anakumbuka.

“Ingawa niliumia, sikuonyesha katika utangazaji wangu. Hiyo ni moja ya sifa anazotakiwa kuwa nazo mtangazaji wa mpira, hata kama unapenda timu fulani, ikifungwa hupaswi kujionyesha.”

Ni mpenzi wa Arsenal, lakini Hilary anasema hapa nchini hakupenda kuingia kwenye ushabiki wa Yanga na Simba.

“Kwa hapa Tanzania nilikuwa naipenda klabu ya Mlandege ya Zanzibar. Sikupenda mambo ya usimba na uyanga. Niliipenda klabu hiyo pia kwa sababu kuna mdogo wangu alikuwa akiichezea anaitwa Shem Frank, alikuwa nahodha.

“Lakini nje ya Tanzania, mimi ni mshabiki wa Arsenal, tena sana sana, tena sana.”

Kuanzisha Radio One Stereo

Moja ya kazi ngumu alizokumbana nazo ni kuanzisha kituo cha redio cha Radio One Stereo.

“Nakumbuka tulipewa jukumu la kuanzisha Radio One, wakati huo nikiwa na Brother Mikidadi Mahmoud na Julius Nyaisanga (marehemu). Hilo ndilo jambo gumu zaidi nililokutana nalo,” anasimulia.

“Tulikesha ili kufikiri namna bora ya kuendesha redio hiyo iliyokuwa ya kwanza binafsi nchini. Sote tulitoka Radio Tanzania, hivyo ugeni wa jukumu ulitufanya kulala wakati mwingine saa 8:00 usiku tukijaribu kupanga kipindi hiki kiende wapi, kile kitoke saa ngapi.

“Nakumbuka tulifanya kazi kwa ushirikiano sana pia na Taji Liundi, Rankim Ramadhan na Flora Nducha. Hakika ilikuwa ni kipindi kigumu.”

Historia ya utangazaji

Mbali na yote hayo Charles anakumbuka kwamba akiwa RTD, kwa mara ya kwanza alisoma taarifa ya habari ya saa 7:00 mchana mwaka 1981, ingawa hakumbuki siku wala mwezi.

“Nakumbuka pia mechi yangu ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakati huo kutangaza ilikuwa kati ya Yanga na Coastal Union, hiyo ilikuwa mwaka 1982. Nilikuwa na walimu wangu Salim Mbonde na Ahmed Kipozi,” anasema.

Ilikuwaje?

Charles anaeleza kuwa siku hiyo akiwa bado kijana mdogo alikwenda uwanjani na wakongwe hao na kwa kawaida wanafunzi walipewa dakika tano za kujifunzia.

“Kipozi akanipa ‘mic’ nikaanza kutangaza, nilipokamilisha dakika zangu tano, nikataka kurudisha kipaza sauti, lakini Kipozi akaninong’oneza akisema; “endelea”. Hiyo iliashiria naweza na tangu siku hiyo nikawa natangaza mpira,” anasema Charles.