Chato kutumia fedha za Tamasha kuboresha shule

Muktasari:

  • Wilaya ya Chato mkoani Geita imeandaa tamasha la utalii la Burigi-Chato litakalosaidia kuhamasisha utalii, sambamba na kukusanya fedha zitakazotumika kuboresha miundombinu ya shule za msingi.

Dar es Salaam. Uongozi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita, umeandaa tamasha la utalii litakalokusanya fedha zitakazotumika kuboresha huduma za jamii ikiwemo miundombinu ya shule.

Tamasha hilo litakalohamasisha utalii katika ukanda huo kupitia kivutio cha kisiwa cha Rubondo na Hifadhi ya Burigi- Chato  litafanyika uwanja wa John Magufuli wilayani humo kuanzia  Novemba 26 hadi Disemba 3 mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale ameeleza hayo leo Jumatano Oktoba 4,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamasha hilo, akiambatana na Mkuu wa Hifadhi ya Burigi -Chato, Ismail Ismail.

“Baada ya tamasha hili tunatarajia Chato kunufaika hasa katika elimu, mwaka huu tumepanga fedha zote zitakazopatikana kuelekezwa katika elimu kwa sababu tuna upungufu wa madawati.

“Chochote kitakachopatikana katika tamasha hili tutakipeleka katika ununuzi wa madawati ili kuboresha mazingiria mazuri ya wanafunzi kujifunza na kujifunzia,” amesema Katwale.

Kwa mujibu wa Katwale Chato inakabiliwa na upungufu wa madawati 29,000, akisema fedha zitakazopatikana zitaelekezwa katika ununuzi wa madawati 605 waliopanga mwaka huu na kupelekwa katika shule za msingi.

Katwale amesema malengo mengine ya tamasha hilo ni kutoa nafasi kwa wananchi kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii, biashara wilayani humo  na mkoa wa Geita. Pia kutangaza fursa za utalii ili kuvutia watu kuwekeza Chato.

“Tamasha hili litahusisha mchezo wa mpira wa miguu kati ya mashabiki wa Yanga na Simba, pia ndondi ambapo kutakuwapo bondia Karim Mandonga sambamba ngoma za utamaduni,” amesema Katwale.

Kwa upande wake, Ismail amesema kwa mwaka kuna wastani wa watalii kutoka nje 78 na ndani 585, wanaotembelea vivutio hivyo huku akisema malengo yao kuongeza namba hadi kufikia 500 wanaotoka nje na wa ndani 1,000.

“Tuna mikakati ya kufungua barabara ili ziwe nyingi, kuongeza miundombinu ya kisasa, wanyama. Hadi sasa tunahitaji aina 41 za wanyama, hivyo tamasha hili litatusaidia sana,” amesema Ismail