Cheed aeleza BSS ilivyompa kiu ya kusaka mafanikio

Muktasari:
Cheed aliichukua changamoto ya kukataliwa na majaji wa shindano la BSS kama njia ya kutafuta mafanikio yake kwa kupambana kwa bidii na sasa ni miongoni mwa wasanii walio katika lebo ya Kings Music chini ya uongozi wa Ali Kiba.
Dar es Salaam. Cheed, mmoja wa wasanii wanaounda kundi la Kings Music linaloongozwa na Ali Kiba, amesema aliposhiriki shindano la BSS alielezwa na majaji kuwa si mzuri katika uimbaji.
Akizungumza na Mwananchi, Cheed amesema hatosahau kauli hiyo mwaka 2015 aliposhiriki shindano hilo la kuibua vipaji nchini Tanzania.
Amesema ilikuwa katika ufukwe wa Coco Beach katika Bahari ya Hindi alikokwenda kufanya usaili ili kuwa miongoni mwa wasanii watakaochaguliwa kuingia katika kinyang’anyiro cha kusaka mshindi.
“Yaani nilivyofika mbele ya majaji hata hawakutaka kunisikiliza sana wakaniambia sasa wewe mbona unaimba kama mwanamke, utaenda wapi na sauti yako hiyo na kunitaka niondoke,” amesema.
“Hata hivyo nashukuru jambo lile halikunikatisha tamaa lilinipa nguvu ya kuendelea kupambana mpaka nilipokutana na Ali Kiba ambaye alinisajili katika lebo yake na sasa natamba na kundi hili la Kings Music.”
Cheed amewashauri vijana wanaochipukia katika uimbaji na kushiriki mashindano mbalimbali kutokata tamaa, “wanatakiwa kufuata ushauri watakaopewa na majaji. Watafanikiwa kutimiza ndoto zao.”
Aliwatolea mfano wanamuziki Harmonize na Andrew Msechu waliowahi kushiriki BSS o mara mbili na kufanikiwa kupata mafanikio.
“Haya mashindano ni kitivo cha kuzalisha vipaji, ukishiriki ukakosolewa unajua nafasi yako ni ipi na unatakiwa ufanye nini ili usonge mbele, ”amesema.