Choo cha wanafunzi Shule ya Sekondari Mashati chajaa
Muktasari:
Mkuu wa shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 600 asema choo kinachotumika kinaweza kuleta magonjwa
Rombo. Zaidi ya wanafunzi 600 wa Shule ya Sekondari Mashati wilayani hapa wanakabiliwa na changamoto ya choo chao kujaa.
Akizungumza na gazeti hili, mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Mrosso alisema licha ya choo hicho kilichoanza kutumika zaidi ya miaka 30 kujaa, wanafunzi walikuwa wakiendelea kukitumia.
“Shule hii ina zaidi ya wanafunzi 600 na choo kinachotumika ni kibovu na kimejaa; kinaweza kuleta magonjwa na madhara makubwa kwa wanafunzi hawa, maana hawana sehemu nyingine ya kujisaidia. Tulipewa miezi mitatu kujenga choo kingine lakini bado hatujakamilisha,” alisema mwalimu Mrosso
“Tumepewa miezi mitatu choo hiki kibomolewe maana kinaweza kuleta madhara makubwa kwa wanafunzi kutokana na hali hii, baadhi ya wananchi wameanza kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa choo kingine lakini kasi ya uchangiaji ni ndogo.”
“Tunawaomba wadau popote pale walipo watusaidie hata wale waliosoma hapa kama hali zao ni nzuri waje watuachangie tukamilishe ujenzi huu wa choo cha wanafunzi, maana muda unaenda na shule ziko mbioni kufunguliwa, tunaomba pia Serikali iingilie kati tukamilishe ujenzi huu mapema ili wanafunzi watakaporudi wapate sehemu za kujihifadhi,” alisema mwalimu mkuu huyo.
Diwani wa Katangara Mrere, Venance Mallel alisema baada ya hali hiyo, wananchi wanaendelea kutoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa choo hicho ili kunusuru maisha ya wanafunzi yao.
“Nawaomba wananchi wangu muendelee kuchanga kwa ajili ya ujenzi wa choo hiki, juhudi za kuanza kukijenga zimeshaanza tayari, ili wanafunzi wetu watakaporudi Januari angalau tuwe tumesogea kidogo maana hali ni mbaya,” alisema Mallel.
“Nawashukuru wale wote ambao mmeanza kuchanga kwa kunusuru maisha ya watoto wetu, sisi ni wazazi na tunajua ili mwanafunzi afanye vizuri, ni lazima apate sehemu nzuri ya kujihifadhi, kinyume na hapo hataweza kufanya vizuri darasani.”
Kutokana na hali hiyo, mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda alilazimika kutumia sikukuu ya Krismasi kutembelea shule hiyo na kuwataka wote waliosoma shule hiyo na wako maeneo mbalimbali ya nchi kujitokeza kuisaidia shule hiyo na kuacha kutegemea Serikali kwa kila kitu.
“Serikali yetu imeendelea kuwekeza sana Rombo, mpaka sasa imetoa Sh70 milioni kwa ujenzi wa majengo ya utawala wa shule hii, nitoe wito kwa wananchi tusitegemee kila kitu Serikali tutachelewa kufika kwa kasi tunayotaka.
“Wananchi tuendelee kuchanga fedha ili kuzisaidia shule zetu, changamoto ni kubwa sana kwenye shule zetu hasa suala la vyoo,” alisema Profesa Mkenda.
“Tutaendelea kufanya kazi karibu na Serikali kuhakikisha tunapata fedha kwa ajili ya kuendeleza majengo ya shule hii, lakini niwaombe wote waliomaliza katika shule hii mjitokeze.”