Chuo chabuni mbinu kuhamasisha somo la sayansi

Thursday November 25 2021
mbinupic
By Hawa Mathias

Mbeya. Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (Must) mkoani Mbeya kimebuni mbinu ya kutumia wanataaluma wa kike kutembelea Shule za Sekondari kuhamasisha masomo ya Sayansi ili kuwezesha Serikali kupata wataalam wa nyanja mbalimbali.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Aloyce Mvuma amesema leo Alhamis Novemba 25, 2021 kwenye mdahalo wa kujadili changamoto na mafanikio kwa taasisi za elimu ya juu kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru ikiwa ni mwendelezo wa mdahalo wa siku tatu  unaofanyika chuoni hapo.

Amesema  kuna changamoto kwa wanafunzi wa kike kutopenda masomo ya Sayansi wanapoingia kidato cha tano na sita pasipo kujua kuwa masomo hayo yana fursa kubwa za ajira ambazo  zimepewa kipaumbele cha  katika vyuo vya elimu ya Juu.

''Sisi kama uongozi wa chuo lengo ni kufikia asilimia 50 ya wanafunzi wa kike watakao soma masomo ya Sayansi na ndio sababu ya kuunda kikosi cha wataalam ambao wanazunguka katika Shule za Msingi ,Sekondari kuhamasisha vijana ili kuwezesha chuo kufikia malengo kwa kuwajengea misingi ya kuwa wabunifu ambao utaleta tija kwa Taifa katika kuelekea uchumi wa viwanda'' amesema.

Ameongeza kuwa awali wakati chuo hicho kikianza mwaka 1986 kilikuwa na wanafunzi 120 ambapo tangu Serikali ikipandishe hadhi kuwa chuo kikuu udahili umeongezeka mpaka kufikia wanafunzi 6,800 kati ya hao wasichana ni 1,510 jambo ambalo la kujivunia katika miaka 60 ya Uhuru.

Mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini , Oran Njeza amezitaka Taasisi za elimu ya Juu kuandaa vijana kulingana na ubunifu wa ushindani wa mataifa mengine ili kuitangaza  Tanzania kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Advertisement


Advertisement