CRDB yaja na kampeni kuhamasisha bima

Muktasari:

Katika Kuhamasisha watumiaji wa barabara kuwa na bima, Benki ya CRDB imeanzisha kampeni ya kufanikisha hilo.

Dar es Salaam. Ili kuhamasisha watumiaji wa barabara hasa bodaboda kuwa na bima za vyombo vya moto, Benki ya CRDB imeanza kampeni ya kutoa elimu kwa madereva wa vyombo hivyo.

Hatua hiyo inakuja, kipindi ambacho CRDB inaeleza kuwa kumekuwa na elimu duni kwa madereva kuhusu bima ya vyombo vya moto.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo iliyopewa jina la ‘Kuwa Shua’ Mkuu wa Kitengo cha Bima cha benki hiyo, Moureen Majaliwa amesema pamoja na mambo mengine hatua hiyo itawakinga watumiaji wa vyombo hivyo.


“Katika kipindi cha kampeni Maofisa wetu watatembelea wateja kuwapa elimu, pia tutatoa zawadi kwa wateja watakaokata bima kupitia Benki ya CRDB,” amesema.

Kulingana na ofisa huyo, mteja atakayekata bima kubwa kupitia benki hiyo atarudishiwa asilimia tano ya kiasi cha bima kabla ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kama mafuta katika vituo vya Oryx.

“Baada ya kulipia bima kupitia tawi la benki, CRDB Wakala au SimBanking, mbali na mteja kupokea ujumbe wa sera yake ya bima, vilevile atapokea ujumbe wenye nambari ya zawadi ambayo ataitumia kujaza mafuta katika vituo vya Oryx,” amefafanua.

Amesema kampeni hiyo pia inalenga kusaidia malengo ya Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ya kuongeza ujumuishi wa Watanzania katika huduma za bima kufikia asilimia 50 mwaka 2030.


Kadhalika, amesema benki hiyo imeandaa tamasha la elimu ya bima ya vyombo vya moto litakalofanyika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, Septemba 17 mwaka huu.

Amebainisha kuwa kampuni za bima, gereji, maduka ya vifaa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Msuluhishi wa Migogoro ya Bima na Jeshi la Polisi ni miongoni mwa wadau watakaokuwepo katika tamasha hilo.

Meneja Uendeshaji Huduma za Bima Benki ya CRDB, Tumaini Frank amesema madai ya wateja wa bima yatashughulikiwa siku hiyo.