CWT waendelea kupinga kuanzishwa bodi ya walimu

CWT waendelea kupinga kuanzishwa bodi ya walimu

Muktasari:

  • Chama cha walimu Tanzania (CWT) kimesisitiza uamuzi wake wa kupinga  kuanzishwa kwa  bodi ya kitaaluma ya walimu.

Dodoma. Chama cha walimu Tanzania (CWT) kimesisitiza uamuzi wake wa kupinga  kuanzishwa kwa  bodi ya kitaaluma ya walimu.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Aprili 13, 2021 rais wa chama hicho,  Leah Ulaya amesema bodi hiyo ililenga kumkandamiza mwalimu badala ya kumsaidia.


Ulaya amesema chama hicho kimekataa uanzishwaji wa bodi hiyo kwa sababu ya kupunguza utitiri wa vyombo vinavyomsimamia  mwalimu na sheria  kama kuhuisha leseni ya mwalimu kila mwaka kwa pesa yake na akishindwa kufanya hivyo basi atapoteza sifa ya kufundisha  jambo ambalo linamkandamiza.


Amesema usikilizwaji wa mashauri ya nidhamu yanasikilizwa kwa fedha ya mwalimu huku akitakiwa kulipia leseni na ada ya mwaka ambayo si chini ya Sh50,000.


Ulaya amesema mwaka 2019, walikataa kutoa maoni juu ya uanzishwaji wa bodi hiyo baada ya kuzisoma sheria na kuona zinamkandamiza mwalimu ambaye hadi sasa anadai mshahara alio nao haukidhi gharama za maisha.


Aprili 12,2021 chama hicho kilialikwa na katibu wa Bunge kukutana na kamati ndogo kwa ajili ya sheria na kanuni za uendeshwaji wa bodi hiyo, ndipo walipoonesha msimamo wao wa kuikataa tena bodi hiyo.


“Sisi kama CWT na walimu wote wa Tanzania wa umma na binafsi, tunaendeleza msimamo wetu wa kupinga uanzishwaji wa bodi ya walimu Tanzania,” amesema Ulaya.


Mwenyekiti wa chama cha walimu Mkoa wa Dodoma, Clement Mahemba amesema kama kulikuwa na upungufu kwenye tume ya utumishi wa walimu yangefanyiwa marekebisho badala ya kuongeza vyombo vinavyomsimamia mwalimu.