Daladala wagoma tena Arusha, wamwangukia Rais
Baadhi ya abiria wakisubiria usafiri jijini Arusha
Muktasari:
- Wakati madereva wa daladala zifanyazo kazi jijini Arusha wakigoma kupinga kuingiliwa na bajaji katika njia zao, Mkuu wa Mkoa huo, John Mongela amesema timu yake inashughulikia suala hilo.
Arusha. Mgomo wa daladala umerudia tena jijini hapa, huku madereva wa magari hayo wakimwomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati mgogoro uliopo kati yao na madereva wa pikipiki za matairi matatu maarufu kwa jina la Bajaj.
Mgomo huo unafanyika leo Agost 14 ikiwa ni mara ya tatu mfululizo, ukiwemo mgomo uliofanyika Julai Mosi na mwingine ukafuatia wa Julai 3 mwaka huu, ambapo madereva daladala wamekuwa wakishinikiza kuondolewa kwa usafiri wa bajaji katika barabara wanazohudumu kwani zinawanyima biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, mmoja wa madereva daladala Herman Elias amesema katika mgomo wao wa pili, Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela aliitisha kikao cha madereva hao na kusikiliza madai ya daladala na Bajaji na kuahidi kuchukua hatua ya utatuzi.
"Mkuu wa mkoa alisema atatusaidia kuondoa Bajaji kwenye ruti zetu lakini hadi leo hakuna kinachoendelea, sasa tumeamua kusitisha huduma watoe hao wanaowakumbatia" amesema.
Kwa upande wake dereva wa daladala Simon Laizer amesema kuwa bajaji zimekuwa nyingi mjini zikifanya shughuli nje ya kanuni zao za kukodiwa kama taksi badala yake wanaokota abiria na kupita zile ruti ambazo wanapita wao.
"Tumeamua kuitisha mgomo usio na kikomo hadi tupate suluhisho na kwa sababu mfupa huu umekuwa mgumu kwa mkuu wa mkoa, sasa tunaomba Rais Samia aingilie kati tuambiwe hawa bajaji wana nguvu gani hadi wanavunja sheria bila kuchukuliwa hatua," amesema.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa, John Mongela akizungumzia na Mwananchi leo amesema kuwa bado timu yake anashughulika na utatuzi na baadae wataweka wazi kilichofanyika.
"Sio suala kubwa kubwa kama inavyochukuliwa, na timu yangu iko kazini kuhakikisha tatizo linapata Suluhu hivyo subirini mtapata taarifa nzuri baada ya mda," amesema.
Uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Arusha ulipotafutwa kuhusu suala hilo, haukuwa tayari kuzungumzia.
Hata hivyo, mwezi mmoja uliopita Ofisa Mfawidhi wa Latra, Amani Mwakalebela alisema wanaandaa utaratibu wa kuhakikisha wanazihakiki bajaji za ndani ya jiji a Arusha na kuzipunguza.
Amesema kuwa ndani ya Arusha kuna zaidi ya bajaji 2,000 zinazofanya kazi, wakati zilizosajiliwa hazizidi 350.
"Kama mnavyojua awali waliokuwa wanatoa lesseni za usafirishaji ni halmashauri ya Jiji la Arusha, lakini tangu mwaka jana tulikaa na tukaamua tufunge Usajili mpya baada ya kuonekana zimekuwa nyingi lakini nashagaa pamoja na kufunga bado kuna baadhi ya wafanya biashara wameendelea kuzinunua na kuziingiza katika mzunguko," amesema.
Akizungumzia mgomo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro (AKIBOA), Locken Adolf amesema kuwa utitiri wa bajaji umeathiri biashara ya daladala hivyo wanaiomba serikali kuzipunguza
"Kwa ukubwa wa eneo la Arusha, hazitakiwi kuzidi zaidi ya 100 lakini sasa zimekuwa nyingi na zimekuwa kero sana kutokana na zimeteka ruti zote za daladala na zinafanya biashara ya kuokota abiria kama wanavyofanya wenzao jambo ambalo sio makubaliano wakati zinaingia mjini," amesema.
Amesema kuwa wamebaini bajaji nyingi ndani ya jiji la Arusha hazina leseni lakini zinaruhusiwa kufanya kazi tofauti na daladala ambazo zimekuwa zikipigwa faini kila hatua.
"Tunataka kujua anaeendesha usimamizi wa hizi bajaji ni nani na ana sauti gani kwenye mamlaka za serikali zinazosimamia usafirishaji maana wao wanafanya kazi kinyume na Sheria, taratibu na makubaliano lakini hawafanywi chochote wanazidi kupeta tu," amesema.
Mmoja wa abiria aliyezungumza na Mwananchi, Amina Hassan amesema kuwa mgomo huo ulianza leo alfajiri umesababisha mateso makubwa kwa wakazi wa Jiji la Arusha pamoja na wanafunzi wanaotumia usafiri huo kuwahi makazini na shuleni.
"Tunaomba Serikali itafute suluhu la jambo hili kwani tunaoteseka ni wananchi na hili jambo la daladala kugoma imekuwa sio mara moja," amesema.