Danadana majaribio treni ya SGR Dar - Moro

Muktasari:

  • Danadana zimeendelea kutawala juu ya kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar – Morogoro, baada ya kuahirishwa mara kadhaa kwa majaribio yaliyopangwa kufanyika mwaka huu.


Dar es Salaam. Danadana zimeendelea kutawala juu ya kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar – Morogoro, baada ya kuahirishwa mara kadhaa kwa majaribio yaliyopangwa kufanyika mwaka huu.

Mradi huo uliokusudiwa kutekelezwa kwa miezi 30, ulitakiwa kukamilika Novemba 2019, lakini uliongezewa muda wa miezi 18 na hivyo ukatakiwa kukamilika Aprili 2021.

Ucheleweshaji huo wa awali wa miezi 18, uliongeza gharama za ziada kiasi cha Sh26 bilioni, kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyoishia Juni 30, 2020.

Kipande hicho chenye urefu wa kilomita 300 ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa nchini na uliozinduliwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli Aprili 12, 2017 na hadi sasa haujakamilika.

Mkandarasi, kampuni ya Yapi Merkezi kwa kushirikiana na kampuni ya Mota Engil wanaendelea na ujenzi wa kipande cha kwanza ambacho inaelezwa kimekamilika kwa zaidi ya asilimia 90, ingawa kuna baadhi ya maeneo ambayo yanaonekana hayajaunganishwa, yakiwemo ya jijini Dar es Salaam.

Awamu ya pili ya mradi huo ni kipande cha Morogoro - Makutupora chenye urefu wa kilomita 442 na ujenzi wake ulizinduliwa pia na hayati Magufuli Machi 14, 2018, hadi sasa ujenzi wake unaendelea.

Awamu ya tatu, kipande cha Makutupora - Tabora (kilomita 294) na awamu ya nne kutoka Tabora – Isaka (kilomita 130) bado hazijaanza kujengwa, lakini awamu ya tano, ambayo ni kipande cha Isaka – Mwanza (kilomita 249) tayari kimepata mkandarasi na ujenzi umeanza.

Wakati ujenzi wa kipande cha Dar – Morogoro ulitakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 30 baada ya kuzinduliwa, na muda huo umepita, haifahamiki sababu za kuchelewa kwake wala siku ya kuanza kutumika.

CAG Charles Kichere alibainisha katika ripoti yake ya miradi ya maendeleo ya mwaka 2019/20 kwamba Serikali imelipa zaidi ya Sh2.9 bilioni kama riba ya ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi na Sh26 bilioni kama ucheleweshaji wa mradi hadi kufikia Aprili 2020.

Alipotafutwa kuzungumzia maendeleo ya mradi huo na lini majaribio yatafanyika, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRC), Masanja Kadogosa hakutaka kulifafanua suala hilo.

“Mbona tulishatoa taarifa kuhusu hilo, niko barabarani, nipigie kesho (leo) tuzungumze,” alijibu Kadogosa na hata alipotafutwa siku iliyofuata hakupokea simu yake wala kujibu ujumbe mfupi wa simu aliotumiwa.

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ambaye alisema alipoingia wizarani, aliambiwa majaribio ya reli ya kisasa yatafanyika Desemba inayoanza leo.

“Majaribio ninavyojua mimi ni Desemba, nilivyoambiwa baada ya kuingia hapo wizarani… tusubirie halafu mtuulize, itabidi tutafute sababu nyingine lakini tutakuja na sababu ya msingi. Lakini tunaamini Desemba kama nilivyoambiwa, itakuwa imekaa vizuri,” alisema Profesa Mbarawa.

Ahadi za viongozi

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa Serikali wamekuwa wakieleza matumaini ya kuanza kwa majaribio katika kipande hicho ili wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro waanze kutumia treni ya kisasa itakayokwenda umbali wa kilomita 160 kwa saa.

Novemba 19, 2020, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea mradi huo Morogoro na akaeleza kuridhishwa na ujenzi wa kipande hicho ambacho wakati huo alisema umefikia asilimia 90 na aliwaahidi Watanzania kwamba njia hiyo ingepitisha treni ya kwanza Aprili 2021.

Ilipofika Aprili 20, 2021, Waziri Mkuu alitangaza tarehe nyingine, akisema treni hiyo ya kisasa ingeanza kufanya majaribio kuanzia Agosti mwaka huu katika kipande cha kutoka Pugu hadi Morogoro.

Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi wa SGR kuanzia stesheni Gerezani mkoani Dar es Salaam ambapo kumejengwa kituo cha kisasa cha abiria.

Aliipongeza TRC kwa kazi nzuri ya kusimamia mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki na kwamba ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ulikuwa umefikia asilimia 91.

Katika ziara hiyo, Kadogosa alimweleza Waziri Mkuu kwamba walikuwa wanatarajia Julai 2021 mabehewa na vichwa vya treni vingewasili kwa ajili ya majaribio, lakini walikuwa wakiangalia uwezekano vije kabla ya mwezi huo.

Machi 15, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho, akiwa Morogoro, naye alisema treni ya kisasa ingeanza kufanya kazi Agosti mwaka huu na kwamba walikuwa wakifanya jitihada kukamilisha baadhi ya kazi zilizokuwa zimesalia.

“Baadhi ya maeneo ambayo bado hayajakamilika, mfano kwenye sehemu za kuunganisha madaraja ya reli na barabara na sehemu nyingine miundombinu ya umeme, vyote hivyo tutavikamilisha ndani ya muda mfupi ili mwezi wa saba (Julai 2021) tufanye majaribio na mwezi wa nane treni ianze kufanya kazi,” alisema Chamuriho.

Mbali na viongozi hao, Msemaji wa Serikali wakati huo, Dk Hassan Abbas, Februari 16 wakati wa mahojiano yake na Mwananchi, alibainisha kwamba treni ya majaribio ingewasili nchini muda wowote na baada ya hapo mabehewa ya abiria na mizigo yatawasili na watu wataanza kupanda treni hiyo.

“Kipande cha Dar – Moro, mwaka huu watu wataonja treni. Mwaka huu, Dar – Morogoro Watanzania wataonja treni ya umeme ikoje, wataligusa behewa la umeme likoje. Infact, hapa tunapozungumza kuna mabehewa ya majaribio yako njiani,” alisema.

Ripoti ya CAG

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2019/20 inabainisha kwamba kuna udhaifu katika kusimamia mkataba wa ujenzi wa mradi huo, hususan katika usimamizi hafifu wa muda wa kumaliza mradi.

CAG anabainisha kwamba mkataba kati ya TRC na kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkezi yenye ubia na kampuni ya Mota Engil, ulihitaji usanifu na ujenzi wa SGR kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kukamilika ndani ya miezi 30 kuanzia Mei 2017 hadi Novemba 2019.

Hata hivyo, CAG anabaini kwamba kufikia Desemba 2019, maendeleo ya mradi yalikuwa asilimia 88.39 dhidi ya asilimia 95.96 iliyopangwa.

Pia, alibaini kuwa kipande cha pili kilitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36 kutoka Aprili 2018 hadi Februari 2021. Pamoja na hayo, ukaguzi wa ripoti ya maendeleo ya mradi ulionyesha kuwa, hadi Desemba 2020 mkandarasi alifikia asilimia 52.2 badala ya asilimia 98.7 kama ilivyopangwa.


Kuongezeka kwa riba

Ripoti hiyo inabainisha kwamba kwenye maeneo ya utoaji wa fedha na matumizi, ulipaji fidia, kodi ya zuio na urejeshaji fedha na marejesho ya kodi kulikuwa na udhaifu. Katika ukaguzi wake, amebaini kuwa makandarasi walikuwa hawalipwi ndani ya muda uliokubaliwa wa siku 56 baada ya mhandisi mshauri kupokea nyaraka za madai na vielelezo vya malipo. “Riba iliyotozwa na mkandarasi kwa kucheleweshewa malipo ilikuwa Dola za Marekani 1,286,913.23, sawa na Shilingi za Tanzania 2,983,064,867.1410 ambazo ziliidhinishwa na Shirika la Reli kulipwa kama malipo ya riba ndani ya hati ya malipo namba 41 (IPC 41),” anabainisha CAG.

CAG anaongeza kwamba shughuli za ujenzi wa kipande cha kwanza zilitakiwa kuchukua miezi 30 kuanzia Mei 2, 2017 na kuisha Novemba Mosi, 2019. Pia, kutokana na ucheleweshaji wa muda wa utekelezaji, tarehe ya kukamilisha mradi ilibadilishwa hadi Aprili 21, 2021 ambayo ni nyongeza ya miezi 18.

“Ongezeko la miezi 18 limepelekea gharama ya ziada ya mhandisi mshauri kufikia Dola za Marekani 11,222,653.00 (sawa na Sh26 bilioni),” amebainisha CAG katika ripoti yake ya Miradi ya Maendeleo.

Macho na masikio ya Watanzania yanasubiri kukamilika kwa mradi huo ambao umeshachelewa kwa miezi 25, sawa na miaka miwili na mwezi mmoja.