Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Daraja lililokatika Butiama lakarabatiwa, barabara kufunguliwa kesho

Mafundi wa Tanroads Mkoa wa Mara wakiendelea na kazi ya kukarabati eneo la daraja la Mto Nyamika Wilaya ya Butiama lililokatika kutokana na mvua zinazoendelea maeneo mbalimbali nchini. Picha na Beldina Nyakeke 

Muktasari:

Huduma za usafirishaji kwa njia ya Barabara Kuu ya Sirari – Musoma -Mwanza kupitia eneo la Daraja la Nyamika Wilaya ya Butiama mkoani Mara zilizositishwa zitarejea kuanzia Jumamosi Mei 6, 2023 baada ya ukarabati wa eneo lililobomoka kukamilika.

Butiama. Huduma ya usafirishaji kupitia Barabara Kuu ya Sirari – Musoma - Mwanza zilizositishwa kwa muda baada ya daraja la Mto Nyamika iliyoko Wiaya ya Butiama kukatika unatarajiwa kurejea kuanzia kesho Jumamosi Mei 6, 2023.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanania (Tanroads) Mkoa wa Mara,  Vedastus Maribe ameiambia Mwananchi Mei 4, 2023 kuwa huduma hizo zitarejea baada ya kazi ya kukarabati eneo la daraja lililokatika kukamilika.

‘’Tuko kwenye hatua za mwisho za ukarabati wa eneo lililokatika kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha. Tunafanya kazi usiku na mchana na ninaamini kufikia Jumamosi Mei 5, 2023 kazi hii itakuwa imekamilika na magari kuruhusiwa kuanza kutumia barabara hii,’’ amesema Maribe

Barabara Kuu ya Sirari – Musoma – Mwanza imefungwa tangu Mei 3, 2023 baada ya daraja la Mto Nyamika kukatika kutokana na mvua zinazonyesha sehemu mbalimbali nchini.

Ili kupisha kazi ya kukarabati eneo hilo, vyombo vyote vya usafirishaji kwa njia ya barabara vinalazimika kuzungukia mjini Butiama, takriban umbali wa kilomita 30.

Kwa mujibu wa Maribe, Tanroads Mkoa wa Mara unaendelea na ukaguzi na ukarabati katika miundombinu yote kuhakikisha barabara zote za mkoa huo zinapitika kipindi chote cha mwaka, hasa kipindi hiki cha mvua.

Akizungumzia ukarabati wa eneo la daraja lililokatika, mmoja wa madereva wa magari makubwa yanayosafiri katika ya Musoma na Mwanza, Hassan Kasubi ameupongeza uongozi wa Tanroads kwa juhudi zinazofanyika kukarabati eneo hilo kuwezesha magari kuanza kupita badala ya kuzungukia mjini Butiama.

"Kwa hakika Tanroads wanastahili pongezi kwa jinsi walivyojitolea kufanya kazi usiku na mchana kurejesha huduma ya usafirishaji kupitia barabara hii. Nashauri kazi zote ziwe zinafanyika kwa kasi na moyo huu,’’ amesema Kasubi

Dereva mwingine, Jumanne Kabwogi amesema kurejea kwa huduma kutawapunguzia gharama za uendeshaji ikiwemo la kulazimika kuzunguka mjini Butiama kwenda na kurudi Mwanza, Musoma, Tarime au Sirari.

"Ukitoka pale Makutano ya Juu hadi  Butiama kisha Kiabakari ni kama kilomita 30 wakati kwa kupitia Barabara Kuu ni kilomita 10 pekee,’’ amesema Kabwigo.