DC atoa angalizo ushuru wa maegesho

DC atoa angalizo ushuru wa maegesho

Muktasari:

  •  Hatimaye ule mfumo wa ukusanyaji ushuru wa maegesho kwa njia ya kielektroniki (TeRMIS), unaanza rasmi kutumika, huku Mamlaka ya Barabara Vijijini na Mjini(Tarura), wakishauriwa kuweka alama maeneo ya maegesho yao kuepusha migogoro.



Dar es Salaam. Hatimaye ule mfumo wa ukusanyaji ushuru wa maegesho kwa njia ya kielektroniki (TeRMIS), unaanza rasmi kutumika, huku Mamlaka ya Barabara Vijijini na Mjini(Tarura), wakishauriwa kuweka alama maeneo ya maegesho yao kuepusha migogoro.

Wito huo umetolewa leo Jumanne Novemba 30, 2021 na  Mkuu wa Wilaya  ya Kinondoni, Godwin Gondwe katika mkutano wa viongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo wakiwamo madiwani, Meya na watendaji  na Tarura katika kupewa elimu kuhusu mfumo huo utakavyofanya kazi na faida zake.

Mfumo huu unaanza kazi tena ikiwa imepita miezi miwili tangu serikali ulipousitisha baada ya kutokea changamoto mbalimbali katika utekelezaji wake ikiwamo bei kubwa ya maegesho  na faini kubwa ambazo wanachi walipaza sauti zao kutoridhika nazo na kwa kuanzia utafanya kazi  katika mikoa mitano ikiwamo Iringa, Dodoma, Dar es Salaam, Singida na Mwanza .

Katika kikao hiko, Gondwe amesema uwekaji wa vibao kuonyesha hapa ni maegesho ya Tarura, utasaidia kuepusha misuguano isiyo ya lazima kati ya wateja na wahudumu wa Tarura.

"Tarura mnapaswa kuepuka migogoro isiyo ya lazma kwa kuweka vibao kujulisha wananchi kuwa hilo eneo mtu ukiegesha gari lako jua utalipa ili mtu ajue kabisa, badala ya kusubiri ameshaegesha ndio unakuja kumuwekea risiti na wakati mwingine mtu huyo utakuta hachukui hata sekunde kadhaa," amesema Gondwe.

Hata hivyo  Mkuu huyo wa Wilaya amesema pamoja na yote, Wilaya inaunga mkono ubunifu huo wa ukusanyaji mapato,na kueleza kuwa fedha ambazo zimekadiriwa kukusanywa kupitia utaratibu huo mpya, zitasaidia kujenga barabara na huenda Kinondoni na nchi kwa ujumla siku za usoni ikawa na barabara za lami zote.

"Katika kuhakikisha mfumo huu unakuwa na matunda,tutahakikisha tunafuatilia hata kila baada ya miezi mitatu kujua umekusanya kiasi gani na kimengia nini ili hata tunapowaelemisha wananchi umuhimu wake waelewe na kutoa tozo hiyo isiwe adhabu kwao bali waone fahari ," amesema Gondwe.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Tarura, Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Lutufya Mwakigonja,  amesema mkutano huo ni mwendelezo wa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu mfumo huo ambao bado ni mgeni hapa nchini huku akieleza kuwa wamejipanga katika kufanyia kazi ushauri na changamoto zozote zitakazojitokeza na  kwa wakati.


Kwa upande wake mtaalamu wa kitengo cha Tehama wa Tarura, Shedrak Mahege, aliwatahadharisha wanaohusika katika kutoa huduma ya kuweka risiti kwenye magari kuepuka kutumia lugha mbaya kwa wateja kwa kuwa vitendo hivyo havitafumbiwa macho na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.


Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti akiwamo Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge, amesema wana imani mapato yatakayokusanywa kwa Wilaya yao, yatafanyia shughuli za maendeleo ya Kinondoni ukizingatia ndio wenye kuchangia kwa kiasi kikubwa mapati ya Jiji la Dar es Salaam.


Wakati diwani wa Mbweni,Single Mtambalike, amesema elimu hiyo anaona kama ilichelewa kutolewa na ndio maana hata wakati inaanza wananchi wengi walionekana kuimpinga na kuongeza kuwa iendelee kutolewa kwa watu mbalimbali mpaka hapo watakapouelewa vizuri.


Katika mfumo huo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, atakayegesha gari kwa saa atapaswa kulipa Sh500,kwa siku Sh2500 na kama utafikisha siku 14 hujalipa tozo hiyo utatozwa faini ya Sh10,000.