DC Gairo azitaka taasisi ‘kausha damu’ zisajiliwe
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabiri Makame akizungumza na wadau wa taasisi za kifedha, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi na kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo kuhusu kuibuka kwa taasisi maarufu kama 'kaushadamu' zinazofanyakazi kinyume cha sheria. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Baada ya kuibuka kwa taasisi nyingi za kifedha zinazotoa mikopo wilayani Gairo baadhi ya taasisi hizo maarufu kama kausha damu zimekuwa zikifanya kazi kinyume cha sheria ikiwemo kutokuwa na leseni kutoka taasisi zinazosimamia sekta ya fedha.
Gairo. Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabiri Makame ametoa mwezi mmoja kwa taasisi zote za kifedha zisizokuwa na leseni za BoT, FCC na Brela kuhakikisha wanakuwa na leseni hizo huku akisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa taasisi zitakazoshindwa kutimiza masharti hayo.
Akifunga mkutano wadau wa sekta ndogo ya fedha uliolenga kujadili changamoto za utendaji kazi wa utasisi hizo, Makame amesema kufuatia uchunguzi uliofanywa na kamati ya usalama ya wilayani humo imegundulika kuwa zipo baadhi ya taasisi maarufu kama 'kausha damu' zimekuwa zikitoa mikopo kinyume cha sheria na hivyo kusababisha malalamiko mengi kwa wananchi.
"Baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na watumishi ambao wamekuwa wakichukua mikopo kutoka taasisi hizi, kamati yangu ya usalama niliipa kazi ya kuzichunguza hizi taasisi. Nilipogundua kuwa zipo baadhi ya taasisi ambazo zina kasoro ikiwemo ya kufanya kazi bila kuwa na leseni kutoka taasisi zinazosimamia Sekta ya Fedha ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Tume ya Ushindani (FCC) na BRELA," amesema Makame.
Aidha amesema kuwa zipo baadhi ya taasisi zimekuwa zikikwepa kulipa ushuru wa Halmashauri, Mikataba kandamizi kwa wateja, baadhi ya taasisi kuchukua kadi za benki za wateja na namba za siri kinyume na Sheria.
Kasoro nyingine ni kuwa na watumishi wasiokuwa na sifa na kutoza riba kubwa kinyume na maelekezo ya BoT.
Kufuatia dosari hizo Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali ingependa kuona taasisi hizi zinakuwa ili ziendelee kuchangia ukuaji wa uchumi na kutoa ajira.
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuilea sekta binafsi ili iweze kukua. Hivyo amezitaka taasisi zote kurekebisha dosari mbalimbali zilizobainika.
Mmoja wa wananchi kutoka wilayani humo Magreth Mkombozi amesema kuwa mikopo inayotolewa na baadhi ya taasisi za fedha imekuwa ni chanzo cha umasikini kwa wananchi kwani wamekuwa wakichukua mali za wanaoshindwa kurejesha mikopo.
"Hizi taasisi zimekuwa zikipiga mufilisi hata wale wadhamini na wamekuwa wakichukua vyombo vya ndani yakiwemo madumu na majaba ya kuhifadhia maji," amesema Magreth.
Mkutano huo umehudhuriwa na wataalamu kutoka BoT ambao walimwakilisha Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, wataalamu kutoka Tume ya Ushindani (FCC), Maafisa wa TRA, Brela, taasisi za fedha 25 zilizopo Wilaya ya Gairo, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi, viongozi wa sekta binafsi, vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa wananchi.