DC Ludewa ahimiza ushirikiano wataalamu, madiwani
Muktasari:
- DC Ludewa awataka wataalamu wa Halmashauri hiyo kuwapa taarifa za miradi na ushirikiano Madiwani ili waweze kuzi semea kwa wananchi.
Ludewa. Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Victoria Mwanziva awaomba wataalamu kushirikiana na Madiwani katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ameyasema hayo leo Mei 13, 2023 katika Baraza la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Mwanziva amesema madiwani ndiyo wenye wajibu wa kuzisemea taarifa za utekelezaji kwa wananchi hivyo ni haki yao kupewa taarifa zote kwa wakati.
“Tuongeze ushirikishwaji wa taarifa kwa waheshimiwa madiwani lengo ni kuwa na uelewa wa pamoja wa miradi ya maendeleo, kwa sababu madiwani ndio watakao zisemea hizi taarifa kwa wananchi,” amesema Mwanziva.
Pia amewataka wataalamu kutoa taarifa kwa madiwani wa maeneo husika kila wanapo kwenda kufanya shughuli za maendeleo.
“Ni marufuku kwa mtaalamu kwenda eneo fulani bila kutoa taarifa kwa diwani wa eneo husika ili mfanye kazi vizuri,” amesema Mwanziva.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Wise Mgina akiwawakilisha madiwani wenzake ameahidi kumpa ushirikiano wa kutosha.
“Waheshimiwa madiwani tutakupa ushirikiano wa kutosha kwa sababu wote tunajenga nyumba moja hatuna haja ya kugombaniana fito, na tunashukuru kwa ushirikiano ambao umekuwa ukitoa tokea ufike,” amesema Mgina.