DC Sabaya apiga marufuku maiti kuzuiwa hospitali kwa sababu ya madeni
Muktasari:
- Uongozi wa hospitali na vituo vya afya wilayani Hai mkoani Kilimanjaro umetakiwa kuacha kuzuia maiti kutokana na ndugu wa marehemu kushindwa kulipa gharama za matibabu.
Hai. Uongozi wa hospitali na vituo vya afya wilayani Hai mkoani Kilimanjaro umetakiwa kuacha kuzuia maiti kutokana na ndugu wa marehemu kushindwa kulipa gharama za matibabu.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Januari 29, 2021 na mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na kubainisha kuwa hospitali husika zinatakiwa kuchukua taarifa za ndugu wa marehemu na kufuatilia malipo baada ya mazishi.
Alieleza hayo alipofanya ziara katika hospitali ya Machame iliyopo wilayani humo baada ya kupata malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusu maiti kuziwa hadi madeni yalipwe na kumuagiza mganga mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha maiti hazizuiwi iwe katika hospitali za Serikali au binafsi.
"Mwishoni mwa mwaka nana na Januari mwa mwaka huu nimepata malalamiko kwa wananchi kuhusu Hospitali hii kuzuia ndugu kuchukua miili ya wapendwa wao. Naelekeza isitokee mtu kuzuia mwili kuchukuliwa.”
“Chukueni taarifa za ndugu wa marehemu ili mkubaliane nao namna ya kulipa. Huwezi kuzuia mwili kwa sababu yoyote ile ,kama ameshakufa wapeni ndugu wakazike na wakishindwa kulipa pelekeni serikalini mkamueleze mganga mkuu wa wilaya ili sisi wenyewe tutaweza kulipa madeni hayo kwa sababu ni mtu wetu,” amesema.