Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Biteko aitupia jicho wizara yake matumizi nishati safi

Muktasari:

  • Wizara ya Nishati, taasisi zake zatakiwa kuwa mfano, kutohubiri habari ya ubaya wakati wao wanautenda.

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameagiza majengo ya wizara hiyo na taasisi zilizo chini yake kuweka miundombinu ya umeme wa jua kupunguza gharama za nishati.

Dk Biteko amesema hayo leo Septemba 13, 2024 jijini Dodoma alipozindua jengo la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na utiaji saini mikataba sita ya kuwezesha miradi ya nishati safi ya kupikia.

“Sisi Wizara ya Nishati ambao tunawaambia watu kila siku tutumie nishati safi hivi ni kwa kiasi gani katika ofisi zetu tunafanya hivyo? Kwa kuanzia tu, ofisi zetu tunatumia nishati safi?” amehoji.

Amesema amefurahi katika jengo jipya la REA amejibu swali hilo kwa kuwa wataweka miundombinu ya umeme wa jua, hivyo kutaka majengo yote ya wizara yake kuweka miundombinu hiyo.

Amewataka kuanza kwa kuweka miundombinu hiyo ili wawe mfano kwa taasisi nyingine za Serikali, hivyo kutokuwa wahubiri habari ya ubaya wakati wao wanautenda.

“Majengo yote ya Wizara ya Nishati yawe na provision ya solar (miundombinu ya umeme wa jua), ili tuweze kutumia nishati safi ya sola  kwa bei nafuu na tuanze kubadilisha mindset (fikra) maana kuna watu wanaamini umeme wa sola siyo umeme, nataka niwahakikishe ni umeme kama mwingine,” amesema.

Ameagiza majengo yote yanayojengwa na wizara yake na taasisi zilizo chini yake kuwekwa miundombinu hiyo.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko ametaka inapotokea jambo linalohusu umeme, hasa kukatika lazima wananchi wapate taarifa mapema kuna shida gani na ni wapi.

“Na ule ubwanameza wa kukaa mezani Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) unapungua kila siku, kila wakati wanakuwa wepesi kuwahudumia Watanzania,” amesema.


Kuhusu miradi

Dk Biteko amesema itakuwa aibu baada ya muda Watanzania wasione matokeo ya miradi ya kuwezesha nishati safi ya kupikia iliyosainiwa katika hafla hiyo.

“Imani yangu na imani yetu sote tuliokuja kushuhudia jambo hili, tumesaini hapa na tena mbele ya vyombo vya habari tukiamini kile tulichokisaini hapa, hichohicho ndicho kitakachotokea tena kwa uharaka zaidi,” amesema.

Amesema nishati safi ya kupikia si ajenda tu ya Rais Samia Suluhu Hassan bali ni ya kuokoa maisha ya watu.

Amesema Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliwapa maelekezo ya kuangalia katika kila fursa ya kufanya nishati safi iweze kupatikana itumike ili Watanzania waipate.

Amesema wakati mwingine watakutana na ugumu wa watu wengine kuonyesha hofu, watasema ajenda hiyo haiwezekani kwa kuwa bei ni kubwa.

“Ni kweli bei ni kubwa lakini nataka kuwaambia kuwa Serikali inafanya kila namna kushusha bei na kuifanya nishati hiyo iweze kupatikana kwa bei nafuu katika maeneo yote,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ngen’da amesema mashine tatu katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) zimeanza uzalishaji wa umeme, huku ya nne ikiwa mbioni kuwashwa.

“Baada ya kuwasha mashine hizo matumizi ya gesi yalibidi yapungue, lakini gesi ipo. Asilimia 60 ya gesi iliyokuwa inatoka imesitishwa kwa sababu tu, tumewasha umeme hatuwezi kuendelea kutumia wa gesi wakati wa maji upo ambao ni nafuu sana kwa Tanesco,” amesema.

Amesema baada ya kupata taarifa hiyo, kamati ilitoa wito wa kuongeza kasi ya matumizi ya gesi katika nishati safi ya kupikia na kuendeshea magari (CNG), akieleza magari mengi yamefungwa mifumo kwa ajili ya kutumia gesi hiyo.

Amesema utiaji saini wa mikataba hiyo unaonyesha jinsi wizara ilivyo makini katika matumizi ya gesi na nishati nyingine mbadala zinatumika kwa manufaa ya nchi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema kwa sasa vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia kwa vyakula vya wafungwa na mahabusu ni kuni ambazo ni asilimia 98, mkaa mbadala asilimia 0.9, gesi asilimia 1.1.

Amesema kuni kwa ajili ya kuandaa chakula cha wafungwa na mahabusu nchini hupatikana katika misitu ya asili iliyopo katika misitu ya magereza, ya kupandwa, matawi ya miti yanayopunguzwa katika maeneo mbalimbali na nyingine za kununua.

Amesema kwa kutambua nishati safi, Jeshi la Magereza, lilianzisha matumizi ya majiko banifu yaliyosaidia kupunguza matumizi ya kuni kwa asilimia 40.

Sillo amesema kati ya magereza 129 yaliyopo Tanzania Bara, matatu yana gesi vunde, vituo vinavyotumia gesi ya LPG vinne, magereza mawili yanatumia gesi asilia.

“Kupitia programu ya matumizi bora ya nishati safi ya kupikia ambayo itatekelezwa katika vituo 211 itahusisha magereza 129. Gharama za mradi huu ni Sh35.2 bilioni, REA watachangia Sh26.57 bilioni na Jeshi la Magereza Sh8.66 bilioni,” amesema.

Akimwakilisha Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Suma JKT, Brigedia Jenerali Petro Ngata ameahidi watatekeleza miradi hiyo kwa weledi kwa ajili ya manufaa ya JKT na Taifa.

Katika mkataba wenye thamani ya Sh5.75 bilioni, REA watatoa Sh4.36 bilioni, huku JKT ikitoa Sh1.39 bilioni. Pia kutajengwa mitambo ya biogasi na ujenzi wa mifumo ya kupikia inayotumia LPG.

Mkurugenzi Mtendaji wa REA, Hassan Sadi amesema wakala umesaini mikataba na kampuni nne za Manjis, Oryx, Lake Gas na Taifa Gas ili kusambaza mitungi ya kilo sita pamoja na vichomeo takriban 450,000 kwa wananchi maeneo ya vijiji na pembezoni mwa miji kwa gharama ya Sh8.64 bilioni.

“Katika mradi huu, Serikali kupitia REA itatoa ruzuku ya hadi asilimia 50 kwa wananchi ili kuwezesha kununua mitungi ya gesi,” amesema.

“Tunaanza kusaini mikataba ya kuwezesha nishati safi ya kupikia na kazi hii itaendelea mpaka tutimize ndoto za Rais Samia kuona Watanzania wote wanapata fursa ya kutumia nishati iliyo salama kupikia,” amesema.

Utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi 2024 hadi 2034 ambao unaelekeza ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Uzinduzi wa mkakati huo, ulifanywa na Rais Samia Mei 2024, hatua iliyokuja miezi michache baada ya kuongoza mkakati kwa nchi kwa nchi za Afrika kuwawezesha wanawake barani Afrika kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Rais Samia alifanya hivyo aliposhiriki Mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) uliofanyika Dubai.


Jengo la REA

Sadi amesema ujenzi wa jengo la REA lenye ghoroga tano umechukua miezi 18 kukamilika na gharama iliyotumika ni Sh9.8 bilioni.

Amesema katika ujenzi huo wakala uliokoa Sh3.8 bilioni kwa kuwa lilipangiwa kutumia Sh13 bilioni.

Amesema ujenzi pia umeokoa Sh7.8 bilioni zilizokuwa zikitumika kulipia kodi ya pango la ofisi tangu mwaka 2008 hadi mwaka 2024.