Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Salmin aliondoa pasipoti kwa Wabara

Dodoma. Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya mfululizo wa makala zinazohusu uongozi wa Serikali ya awamu ya tano wa Serikali ya Zanzibar chini ya Dk Salmin Amour Jumaa ‘Komandoo’ kwa kuangalia mambo alivyoimarisha Muungano, ikiwamo kuondoa sharti la hati za kusafiria kwa raia wa Tanzania Bara kwenda visiwani, kuifungua Zanzibar kiuchumi hadi kuitwa Dubai ndogo na namna sakata la OIC lilivyotikisa nchi na utawala wake.

Licha ya Zanzibar kuwa ndani ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Watanzania kutoka Bara waliendelea kuingia visiwani humo kwa kutumia pasipoti, hadi sharti hilo lilipoondolewa na utawala wa Awamu ya Tano chini ya Rais Dk Salmin Amour.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokea Aprili 26, 1964, ukawa mwanzo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hata hivyo uliendelea kuwa na baadhi ya vikwazo (kero), mojawapo likiwa ni sharti la matumizi ya pasipoti ndani ya nchi.

Masharti ya ya kutumia pasipoti yaliwahusu Watanzania Bara wanaposafiri kwenda Zanzibar, hayakuwagusa Wazanzibari wanaposafiri kuingia Tanzania Bara.

Hali hiyo ilizusha malalamiko kwa kuwa sheria ya uraia inatakaza utaratibu huo ndani ya Jamhuri moja.

Dk Salmin aliondoa hati hiyo kwa sheria haikuwa haikuwa inataka hivyo, bali ulikuwa utaratibu uliokuwa umewekwa na baadaye ukaonekana hauna sababu ya kuendelea kuwapo ndani ya nchi zilizoungana na kuwa kwenye Jamhuri ya Muungano.

Mbali na kuondoa pasipoti, Dk Salmin alifungua milango kwa madhehebu mbalimbali ya dini kuingia Zanzibar ikiwamo kutoa viwanja kwa madhebu ya dini nyingine, mbali na Uislamu. Wazanzibari wengi ni waumini wa dini ya Kiislamu.

Wakati wa Dk Salmin ndiyo nafasi ya Makamu wa Rais wa Muungano iliyokuwa ikitolewa kwa Rais wa Zanzibar iliondolewa.

Dk Salmin katika kuimarisha Muungano, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mara ya kwanza iliingia Zanzibar na kuunganisha mapato ya nchi.

Pia, chini ya uongozi wake, alitilia mkazo maeneo huru kiuchumi, bandari huru na kampuni nyingine za kibiashara ikiwa ni njia ya kujinasua na hali ngumu ya uchumi.


Sakata la kujiunga na OIC

Mwaka 1992, wakati Dk Salmin akiwa na miaka miwili madarakani kulitokea hoja ya Serikali ya Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya kimataifa ya Kiislamu (OIC).

Hoja hiyo ilizua mvutano ndani ya Bunge la Jamhuri ikielezwa Zanzibar imevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku kundi la wabunge 55, maarufu G-55 wakiongozwa na Njelu Kasaka wakidai Serikali ya Tanganyika.

Wakati huo Bunge lilikuwa linakaa Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Karimjee, Agosti 23, 1993 Njelu Kasaka aliwasilisha hoja binafsi bungeni ya kutaka kuundwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.

Pamoja na hoja hiyo kuwa 'nyeti' na yenye kuhatarisha kuuvunja Muungano, Spika wa Bunge Adam Sapi Mkwawa aliiruhusu kujadiliwa kwa uwazi na wabunge wote huku vikao vyote vikiongozwa na Naibu wake, Pius Msekwa kutokana na Spika Sapi kukabiliwa na matatizo ya kiafya.

Suala la Zanzibar kujiunga na OIC lilisababisha Bunge kuingia kwenye mjadala mgumu wa kitaifa ulioitikisa nchi mpaka kuhatarisha kuuvunja Muungano.

Mtafaruku huo wa Serikali ya Zanzibar chini ya Dk Salmin kujiunga na OIC ulisababisha Rais wa Muungano, Ali Hassan Mwinyi kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri na kumuondoa aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Horace Kolimba.


Kuanzishwa Ofisi ya Mufti

Dk Salmin kwenye utawala wake kwa kutumia Amri ya Rais mwaka 1992 alinzisha Ofisi ya Mufti wa Zanzibar na baadaye ikaanzishwa upya kwa Sheria ya Mufti Namb. 9 ya mwaka 2001.

Kabla ya kuanzishwa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar baadhi ya kazi za msingi hasa utatuzi wa migogoro na kutoa miongozo mbalimbali zilifanywa na mashekhe kadhaa. Kwa upande wa Serikali, Mahakama ya Kadhi Mkuu ilikuwa ikitumika kwa madhumuni hayo.


Mahakama ya Ardhi

Vilevile, Dk Salmin kwenye uongozi wake alishughulikia migogoro ya ardhi na Februari 24, 1995 alitia saini Sheria iliyoanzisha Mahakama ya Ardhi Zanzibar, yenye lengo la kutatua migogoro ya ardhi visiwani humo kwa kusikiliza na kutoa maamuzi kwa haraka na ikiwezekana kwa njia ya usuluhishi.

Awali, mashauri ya ardhi yalikua yakisikilizwa na Mahakama za kawaida Unguja na Pemba, ambako ilionekana kuwa, kesi hizo za ardhi zilikuwa zinachelewa kusikilizwa na kutolewa maamuzi kiasi cha kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Uamuzi wa Dk Salmin uliwezesha mahakama za ardhi kuchukua mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ardhi yaliyokua yakisikilizwa na mahakama za kawaida Unguja na Pemba, ambapo ilionekana kuwa, kesi hizo za ardhi zilikuwa zikichelewa kusikilizwa na kutolewa maamuzi kiasi cha kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Awali, Sheria ya Mahakama ya Ardhi ya mwaka 1994, ilitambua, kuwepo kwa hakimu mmoja tu wa kuhukumu kesi za ardhi Unguja na Pemba ambaye aliitwa Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi.

Hali ya kuwepo kwa hakimu (mwenyekiti) mmoja wa kusikiliza na kutolea maamuzi mashauri ya ardhi Unguja na Pemba, pamoja na ongezeko kubwa la kesi kwenye Mahakama ya Ardhi, kulisababisha kuchelewa kutatuliwa kwa mashauri ya ardhi.

Sheria mpya iliruhusu kuanzishwa kwa mahakama za ardhi katika mikoa yote ya Zanzibar.