Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Slaa: Serikali isitumie nguvu vuguvugu la uraia pacha

Balozi Wiliblod Slaa akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na wahariri wa kampuni ya Mwananchi Communication nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Sakata la uraia pacha limeendelea kugonga vichwa, baada ya Balozi Willibrod Slaa kuibuka na kuitaka Serikali kuwashirikisha watu wenye nasaba na Tanzania wanaoishi nje (diaspora) badala ya kutumia “mabavu mabavu” katika mambo yanayohitaji majadiliano.

Balozi Slaa ametoa angalizo hilo siku moja baada ya Serikali kueleza kuwa inakamilisha mchakato wa kutoa hadhi maalumu kwa diaspora ifikapo Desemba badala ya uraia pacha ambao umekuwa kilio chao cha muda mrefu.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Mbweni jijini Dar es Salaam, Dk Slaa, aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Sweden alisema upinzani unaoibuka unatokana na kutoshirikishwa kwa diaspora katika mchakato huo.

Balozi Slaa alisema malalamiko ya diaspora kwenye mchakato wa kutoa hadhi maalumu ni kutoshirikishwa kwao.

Hilo linathibitishwa na kile alichokieleza kuwa pamoja na Serikali kutoa hadhi maalumu, haieleweki kuna nini ndani yake.

“Kuna mtu anajua, Serikali iliwashirikisha? Iliwahoji? Kila kitu tunachofanya sisi ni mabavu mabavu, naamini watu wangeshirikishwa kusingekuwa na kelele zinazopigwa sasa,” alisema.

Kilichopaswa kufanyika, Dk Slaa alipendekeza ni Serikali kujadiliana na watu wake, wapange pamoja, watafute njia rahisi itakayokubalika na wote na kuwalinda kwa uhakika.

“Tatizo ninaloliona Serikali haijajadiliana na watu wake, haijataka kukaa chini na watu wake. Matatizo mengine Serikali inajitafutia yenyewe kwa kutowashirikisha watu,” alisisitiza.

Mwanadiplomasia huyo aliyeiwakilisha Tanzania katika mataifa ya Denmark, Norway, Sweden, Finland na Iceland alisema wakati mwingine Serikali inashindwa kufikia malengo tarajiwa kwa kutojiandaa vizuri.

“Matatizo yapo kwetu, tunashindwa kujiandaa vizuri kabla ya kufanya jambo tunalotaka kulifanya. Nia inaweza kuwa njema, lakini kwa kukosa umakini tunashindwa kufikia malengo tarajiwa,” alisema Dk Slaa.

Suala la uraia pacha, alisema halipaswi kuwa mjadala kwa kuwa waliokwenda nje ya nchi wamefuata maisha na Serikali ilikiri faida iliyopatikana kutoka kwao.

“Serikali yenyewe imetamka kwamba kwa mwaka uliopita diaspora wameleta zaidi ya Sh2 trilioni. Duniani hakuna kitu chenye manufaa kama fedha zinazotoka kwa watu wanaoishi nje ya nchi,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk Slaa, aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema, safari ya watu kutoka katika mataifa yao kwenda kwingineko inatokana na nchi zao kushindwa kuwapatia mahitaji muhimu, ikiwemo ajira.

“Hapa mwananchi anapoteza uraia wa nchi yake aliopewa na Mungu kwa kuukana kwenye karatasi, lakini babu na bibi zake wapo Tanzania, hata kama wamekufa makaburi yao yapo hapa.

“Sasa unawaondoaje hawa ambao vitovu vyao vilizikwa hapa Tanzania, labda Serikali haijafanikiwa kujadiliana na raia wake ili kufikia muafaka unaotakiwa,” alisema.

Kinachoelezwa na Dk Slaa kinaungwa mkono na raia wa Tanzania aliyepo Uingereza kwa sasa, Tito Magoti aliyesema kweli kumekuwa na uhaba wa mazungumzo kati ya Serikali na diaspora, hatua iliyosababisha kukosekana kwa muafaka.

“Bahati mbaya Serikali inaona kwamba imewashirikisha na kuna watu hawakubaliani na hilo, ilivyo ni kama Serikali ilikuwa na maoni yake na haikuhitaji ya watu wengine.

“Diaspora wanashangaa wanaambiwa wameshirikishwa, wapi na lini,” alihoji.

Hata hivyo, Magoti alisema mahitaji ya uraia pacha yanalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma, hususan kwa wananchi wazawa.

Lakini, hadhi maalumu alisema inapora haki ya kuzaliwa na kwamba upembuzi unaoelezwa kuwa hilo ni jambo lenye manufaa zaidi ni maoni ya Serikali, si ya diaspora wenyewe.

“Kama mataifa mengine hawana uraia pacha, isitumike kuwaadhibu wengine wanaohitaji kufurahia haki yao ya kuzaliwa katika taifa fulani,” alisema Magoti.

Mtazamo wa Magoti hauko mbali na wa Dk Shaban Fundi, katibu wa Baraza la Watanzania waishio Marekani (Dicota), aliyesema ushirikishwaji “ulikuwa wa kuchagua makundi”.

“Sasa kuna makundi mbalimbali huku, kuna makundi yako karibu na Serikali na makundi ambayo hayako karibu, yawezekana Serikali ilifanya na makundi iliyo karibu nayo,” alisema.

Dk Fundi, ambaye ni mtengenezaji wa mitalaa ya elimu za sekondari katika mji wa Atlanta, Jimbo la Georgia alisema kwenye utafiti uliofanyika, “kila jimbo huku (Marekani), Watanzania wengi wanataka uraia pacha na si kufungua milango kwa kila mtu, bali kwa waliozaliwa Tanzania wasipoteze Utanzania wao.”

Kuhusu faida za diaspora alisema, kuna faida nyingi, kwani, “sisi tunapotuma fedha, zinapitia Benki Kuu ya Tanzania na zinaingia kama fedha za kigeni, halafu aliyetumiwa anachukua fedha za ndani. Sasa hapo nchi inapata fedha za kigeni bila kuuza bidhaa nje, jambo ambalo lina faida kwa nchi.”

Mtanzania mwingine anayeishi nchini Marekani, Liberatus Mwang’ombe alisema ushirikishwaji uliofanywa ulihusisha watu wachache na si kundi la diaspora wote.

“Kama tungeshirikishwa tusingekubali hadhi maalumu hata kidogo, nakumbuka kuna ofisa wa Serikali alikuja Washington mwaka jana na alizungumza na watu wachache sana, lakini kundi kubwa hatukushirikishwa,” alisema.

Hata hivyo, alisema takriban diaspora 600 wamechanga Sh50 milioni kumpa wakili kwa ajili ya kufungua shauri mahakamani kuhitaji tafsiri ya uraia.

“Hadhi maalumu haikidhi matakwa ya diaspora kwa sababu haimhakikishii haki ya kuwa Mtanzania, tumefungua shauri kujua tafsiri ya raia ni ipi,” alisema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Klabu ya Diaspora Tanzania (TDC), Kelvin Nyamori aliunga mkono hatua inayotarajia kuchukuliwa na Serikali ya kutoa hadhi maalumu kwa raia wake.

Alipoulizwa kuhusu kushirikishwa, alisema Serikali imefanya hivyo kupitia kwa taasisi zinazowaunganisha diaspora.

Alipotafutwa kuzungumzia suala la ushirikishwaji, Waziri Tax alisema Serikali imezungumza na diaspora si wa nchi moja pekee, bali dunia nzima.

Alisema hilo limefanyika kupitia wawakilishi wa vyama vya diaspora, waliokutana nao na wametoa maoni yao.

“Tumewashirikisha kikamilifu, hao wanaolalamika ni wale wachache wanaoona hizo fursa za hadhi maalumu si zile wanazozihitaji, wanataka nyingine wanazotaka wao, sijui ni zipi,” alisema.

Utaratibu wa kukutana nao, alisema ulifanyika kupitia wawakilishi mbalimbali wa Serikali, akiwemo yeye na hata Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, alitaka wanaokataa kupewa hadhi maalumu waeleze wanawakilisha kundi la watu wangapi, ikiwezekana wawasilishe majina yao, kisha watoe mapendekezo yao ya wanachohitaji.

Soma sehemu ya pili ya mahojiano na Dk Slaa kesho