Dosari alizozibaini CAG benki ya kilimo
Muktasari:
- Wakati wakulima wadogo wakikosa mikopo kutoka kwenye benki na mifuko ya Serikali, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imetoa mikopo yenye thamani ya Sh14.1 bilioni kwa wakulima 71.
Dar es Salaam. Wakati wakulima wadogo wakikosa mikopo kutoka kwenye benki na mifuko ya Serikali, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imetoa mikopo yenye thamani ya Sh14.1 bilioni kwa wakulima 71.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini hilo kwenye ripoti ya ukaguzi wa ufanisi na usimamizi wa fedha na programu za Serikali iliyotolewa mwaka huu.
Ripoti hiyo imebaini kuwa katika Mpango wa Udhamini wa Mikopo ya wakulima wadogo umewekwa ukomo wa kupata Sh50 milioni kwa kila mkulima, kitu ambacho kimeonekana kukiukwa na TADB iliyokopesha zaidi.
“Kulingana na uchambuzi uliofanywa inaonesha wakulima wadogo 71 walipata mikopo iliyozidi kiwango kilichowekwa kwenye muongozo cha Sh50 milioni kwa kila mmoja,” ripoti inasema.
“Kutokana na hilo, uchambuzi pia unaonesha wakulima hao 71 walipata hadi Sh2.5 bilioni kinyume na mahitaji ya muongozo wa mikopo hiyo,” inasema ripoti ya CAG.
Hata hivyo, maofisa wa TADB walieleza kwa mkaguzi huyo kuwa miongozo hiyo inaruhusu kutoa mikopo zaidi ya kiwango kama ina tija na mradi husika una umuhimu kwenye maendeleo ya sekta ya kilimo.
“Miongozo inaruhusu kutoa fedha za mikopo zaidi ya kiwango kilichopangwa, endapo tu mradi husika wa kilimo utakuwa na umuhimu mkubwa, tija na athari chanya kwenye kilimo na mnyororo wa thamani,” inasema TADB.
Kwa upande wake, ripoti ya CAG inaeleza kuwa mikopo hiyo iliyozidi kiwango cha muongozo ilitolewa na TADB kama mikopo ya kawaida (isiyovuka kiwango) na bila kuwepo kwa masharti maalumu.
“Mapitio ya rekodi za uidhinishaji yalionyesha kuwa, idhini ilitolewa kwa maombi ya mikopo ya kawaida lakini sio kama mikopo inayozidi kiwango kilichowekwa,” ripoti ya CAG.
“Mikopo hiyo haikuwa na umuhimu wa kutolewa zaidi ya kiwango, hivyo kusababisha idadi kubwa ya wakulima wadogo kukosa mikopo iliyochukuliwa na wachache,” ameongeza CAG kwenye ripoti yake hiyo.
Aidha, ripoti hiyo ya CAG inataja wazi kuwepo kwa ugawaji wa mikopo hiyo ya wakulima wadogo kwa ambao, hawana vigezo hivyo kuwafanya wakulima kukosa mikopo hiyo.
Sh47.1 bilioni kwa wajasiriamali wasiostahili
Ripoti imeonyesha vikundi vya wajasiriamali (SMEs) na ushirika ambavyo havikukidhi vigezo vya kupata fedha vilipewa Sh47.1 milioni. Kwa mujibu wa CAG, vyama vidogo na SMEs vinaweza kudhaminiwa kwa kiasi cha mkopo cha hadi Sh1 bilioni au zaidi, ikiwa wanaweza kuonyesha uhusiano na wakulima wadogo au mashirika ya wakulima.
Vigezo hivyo ni kama kuchukua mazao ya wakulima wadogo chini ya kilimo cha mkataba, kuwapa wakulima wadogo pembejeo na teknolojia, kutoa msaada wa kiufundi, kukodisha vifaa vya kilimo, kushiriki katika kilimo cha msingi au mpango wa wakulima wa nje, na kutumia fedha hizo kupanua biashara zao na wakulima wadogo. Mapitio ya CAG yalibaini licha ya vyama kushindwa kukidhi vigezo hivyo, vipo ambavyo vilikopeshwa hadi Sh9.2 bilioni.
Riba kubwa, mikopo isiyo na wadhamini
Licha ya kutakiwa kutoza mikopo yenye riba zisizozidi asilimia 16, CAG alibaini TADB walitoza riba zilizokuwa kwenye uwiano wa asilimia mbili hadi 30.
Kwa mujibu wa CAG, lengo la mikopo halikufikiwa: “Lengo la jumla la Mpango wa Udhamini wa Mikopo kwa Wakulima Wadogo lilikuwa kuondoa umaskini kwa kuongeza kipato cha wananchi wa vijijini na kuwahakikishia usalama wa chakula kwa muda mrefu”.
Vilevile CAG alibaini uwepo wa madai ya Sh87 milioni kutoka kwa Wateja Wasiokuwa na Udhamini. “Kwa mujibu wa maofisa wa TADB, hakuna madai yoyote yaliyokuwa yamelipwa hadi wakati wa ukaguzi huu”.
Dosari za GFPs
Upande wa Programu za Mifuko ya Serikali (GFPs) ambayo imepewa dhamana ya kutoa mikopo na kusimamia urudishwaji kwa makundi maalumu kwenye jamii, CAG pia amegundua uwepo wa program za mfuko wa Serikali 52, kati ya hizo 46 zinaendelea kutoa mikopo na misaada mbalimbali, lakini sita ambayo ni sawa na asilimia 12 zinapambana kurudisha madeni ya mikopo waliyotoa awali, hivyo hawatoi tena mikopo mipya.
Ripoti ya ‘National Economic Empowerment Council (NEEC)’ ya 2020 inaonesha kuwa mifuko tisa kati ya 12 inatoa mikopo kwa wanufaika wa kundi moja, kitu ambacho kinasababisha mtu mmoja kupata mikopo mingi kwenye mifuko tofauti.
“Kuna uwezekano kwa mtu mmoja kupata mikopo kwenye zaidi ya mfuko mmoja, kwa mfano, mwanamke ambaye ni mlemavu na anafanya biashara ya kilimo na yuko chini ya miaka 35 anaweza kukopa fedha kwenye mifuko tisa,” ripoti ya CAG.
Kwa upande mwingine, mkaguzi aligundua kuwepo kwa mikopo chechefu yenye thamani ya Sh47.4 bilioni kwenye mifuko ya AGITF, SELF MF, na TIB (KKCF) ambayo ni sawa na asilimia 48 ya mikopo yote.
Hii inamaanisha kati ya watu wawili waliokopa kwenye mifuko hiyo ni mmoja pekee alifanikiwa kulipa deni.
Kati ya mifuko hiyo yenye mikopo isiyorejeshwa, mfuko wa Benki ya Uwekezaji (TIB) uliweka rekodi ya asilimia 80 ya mikopo yake kutorudishwa.
Mfuko huo ulitoa mikopo ya wastani wa Sh34.07 bilioni ambapo kati ya hiyo, Sh27.24 bilioni bado haijarudishwa na wanufaika.