Dulla Makabila, Barnaba kutumbuzia tamasha la Sauti za Busara

Dulla Makabila, Barnaba kutumbuzia tamasha la Sauti za Busara

Muktasari:

  • Dulla Makabila na Barnaba ni miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha la Sauti ya Busara litakalofanyika Zanzibar Februari, 2021.

Dar es Salaam. Dulla Makabila na Barnaba ni miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha la Sauti ya Busara litakalofanyika Zanzibar Februari, 2021.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Januari 20, 2021 na mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmoud na kubainisha kuwa vikundi saba kutoka nje ya nchi pia vitatumbuiza pamoja na vingine saba vya nchini.

Amesema  sababu za kumchagua Makabila ni kutokana na kuimba nyimbo zenye vionjo vya muziki wa Afrika akisisitiza ni kati ya sifa za washiriki wa tamasha hilo.

"Mwaka jana tuliona pia msanii wa mtindo wa singeli alifanya vizuri tulipomualika kwenye tamasha hili ambapo watu walionekana kumpenda, mwaka huu tukaona tusimuache msanii wa singeli na tukamchagua Dulla kwani naye anafanya vizuri kwenye muziki huo na siku hiyo atauimba live," amesema.


Amesema tamasha hilo linalofanyika kwa mara ya 18 sasa kauli mbiu yake ni 'Mazingira Yetu Maisha Yetu.'

Kwa upande wake Makabila amesema kuchaguliwa kwake ni matokeo ya muziki huo kupendwa, “nitaweza kukutana na wasanii wengine wa kimataifa naaamini nitapata uwanja mpana wa kuutangaza muziki huu nje ya nchi.”

Vikundi vitakavyoshiriki tamasha hilo na nchi vinapotoka ni Yugen Black rock (Afrika Kusini), Moreleraba (Lesotho), Djam (Algeria), Sika Kokoo Kokoo (Ghana), Dawda Jobarten (Gambia), Siti Muharam (Zanzibar), Sandra Nankoma (Uganda), Stone Town Rockwrz (Zanzibar), Richie Lumambo (Tanzania) na Dogo Fire (Reunion)

Kiingilio katika tamasha hilo kwa watanzania na watu kutoka nchi za Afrika Mashariki kwa siku zote mbili ni Sh10,000 na siku moja ni Sh6000.