Edda Sanga: Udhalilishaji mitandaoni unaathiri wanawake

Muktasari:
- Mwanahabari wa kituo cha Habari cha Taifa (TBC) zamani Radio Tanzania (RTD), Edda Sanga amekemea vitendo vya udhalilishaji wanawake kupitia mitandao ya kijamii akisema inajenga taswira kuwa mwanamke hafai katika ngazi ya uongozi.
Dar es Salaam. Muasisi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Edda Sanga amesema udhalilishaji unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya wanawake wanasiasa, unajenga taswira kuwa mwanamke hafai katika ngazi ya uongozi.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni Rais wa kwanza mwanamke ambaye Tanzania inajivunia kuwa na kiongozi wa juu mwanamke na tangu aingie madarakani amefanya mambo makubwa kila mmoja anayaona.
Sanga ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 26, 2025 katika mahojiano maalumu wakati Tamwa ikitarajia kufanya mkutano wake mkuu wa mwaka kuanzia kesho Ijumaa Juni 27 na 28, 2025.
Mkutano huu utabebwa na kaulimbiu isemayo: “Tunajenga Tanzania ya heshima, usawa na siasa safi bila kejeli.”
Muasisi huyo wa Tamwa ambaye pia amewahi kuwa mwanahabari wa kituo cha Habari cha Taifa (TBC) zamani Radio Tanzania (RTD) amesema kuna haja ya jamii nzima kuelimishwa jinsi ambavyo udhalilishaji huu unavyoathiri juhudi za asasi za kiraia, zilizofanywa.
Hiyo inalenga kuhakikisha mwanamke anapewa sura ya mama, mama mwenye maadili, mama anayeongoza familia.
“Kama udhalilishaji huu unakwenda hivyo unavyokwenda, bado tutaendelea kumuona mwanamke hafai katika ngazi ya uongozi ambayo sio sahihi, kwa sababu tumepigania kwa miaka yote hii kuona mwanamke anafaa kuwa pale,” amesema.
Amesema jamii inapaswa kuelewa kuwa kudhalilishwa mwanamke mmoja, ni kudhalilisha jamii na ni kudhalilisha watoto.
“Basi jamii ikubali hili ni suala linalotakiwa kupewa uzito wa hali ya juu na vyombo vya habari vihakikishe yale mabaya yasionyeshwe, sisi tulio katika vyombo vya habari tunapoona mambo haya yanaonyeshwa kweli tunajisikia vizuri? Je ni sahihi kuruhusu vitu kama hivyo viende, si sahihi,” amehoji.
Akizungumzia nguvu ya mitandao ya kijamii na jinsi inavyotumika kusambaza chuki, Edda amesema iwapo inatumiwa kusambaza ajenda kuwa mwanamke Rais ndiyo mbaya kuliko wote siyo sawa.
“Mbona tumeona wanaume wanafanya mabaya kuliko hayo tunayoyaona na bado wapo madarakani. Kama kuna makosa, tusahihishe kwa namna ambayo ni chanya, kwa kujenga hoja na sio kwa namna hasi na katika kuharibu, unadhani unamharibia mmoja kumbe unaharibia taifa, kwa hiyo inakwenda kuleta taswira mbaya kwa taifa zima,” amesema.
Kwa mwaka huu, Mkutano Mkuu wa Tamwa pia unabeba ajenda ya kupinga lugha za matusi na kejeli dhidi ya wanawake katika siasa.
Hiyo ikilenga kuchochea mjadala mpana na kuibua mikakati madhubuti ya kupambana na matumizi ya lugha za kudhalilisha, kubeza au kuwatisha wanawake wanaojihusisha na siasa, hali ambayo bado ni changamoto kubwa inayowarudisha nyuma wanawake wengi katika uongozi.
Kwa upande wake, Mwanachama wa Tamwa, Lilian Timbuka amesema udhalilishaji wanawake mitandaoni haikubaliki na ndiyo husababisha wanawake kushindwa kuomba nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema hali hiyo inaweza kudhibitiwa pale ambapo asasi za kiraia, serikali kuendelea kutoa elimu namna ya kuhimili mikikimikiki ambayo hujitokeza kipindi hiki cha uchaguzi.
“Wengi wenye tabia ya kudhalilisha wanawake mitandaoni wakiona wamemsema sana mwanamke ambaye hajibu na anaendelea na juhudi zake za kusaka uongozi wanaamua kukaa kimya.
Tutiane moyo wanawake na pale inapoonekana udhalilishaji unatokea mtandaoni dhidi yake tusimame na kumtetea na kumtia moyo kuwa hali hii ipo si Tanzania tu bali duniani kote,” amesema Lilian ambaye ni Mhariri wa Siasa na Dawati la Uchaguzi wa Mwananchi.