Elizabeth II alitangazwa kuwa Malkia akiwa Kenya
Muktasari:
- Ni habari ambayo haijulikani sana, lakini ndiyo ukweli kwamba, miaka 70 iliyopita tangu Princess Elizabeth alipoambiwa kuhusu kifo cha baba yake, George VI akiwa safarini nchini Kenya katika hoteli ya Treetops.
Ni habari ambayo haijulikani sana, lakini ndiyo ukweli kwamba, miaka 70 iliyopita tangu Princess Elizabeth alipoambiwa kuhusu kifo cha baba yake, George VI akiwa safarini nchini Kenya katika hoteli ya Treetops.
Hoteli ya Treetops katikati mwa msitu wa Kenya inajulikana kama mahali ambapo Princess Elizabeth alipokea habari kwamba baba yake amefariki dunia na kwamba angekuwa Malkia wa Uingereza.
Wakati binti mfalme akiwa Treetops usiku ambao baba yake, George VI, alifariki dunia miaka 70 iliyopita, Jumatano ya Februari 6, 1952, hakuambiwa habari hizo hadi alasiri iliyofuata, wakati ambao alikuwa amerudi kwenye nyumba ya wavuvi iitwayo Sagana, umbali wa maili 20, ambayo alikuwa amepewa kama zawadi ya harusi.
Ilikuwa hapo, kando ya mkondo wa maji katika vilima vya Mlima Kenya, ambapo Prince Philip alitangaza habari hiyo.
Binti mfalme na mumewe walikuwa wamesafiri kwa ndege kutoka Heathrow hadi Kenya Alhamisi ya Januari 31 mwaka huo.
Wakati wakiondoka Uingereza waliagwa na mfalme, ambaye kwa wakati huo alikuwa mgonjwa sana akisumbuliwa na saratani ya mapafu kiasi cha kumfanya ashindwe kusafiri.
Umati ulimshangilia kwa huruma huku akisimama kwenye baridi kali ili kumuaga binti yake aliyekuwa akielekea Afrika katika nchi ya Kenya.
Ulikuwa ni wakati wa hatari katika koloni la Uingereza la Kenya. Kampeni ya Mau Mau ya kukabiliana na Wazungu ndiyo ilikuwa imeanza katika Nyanda za Juu walikoishi Wazungu.
Maofisa waliohusika na ziara ya binti huyu katika nchi za Kenya, Australia na New Zealand walihisi hawawezi kumhakikishia usalama alipokuwa Kenya.
Siku tatu baada ya wao kufika, Februari 5 wanandoa hao wa kifalme walisafiri hadi Sagana na kutoka huko walisafiri kwa gari baada ya chakula cha mchana hadi Treetops, nyumba ya wageni ya kutazama wanyama iliyojengwa kwenye miti.
Walikesha usiku kucha wakitazama wanyamapori, wakifurahia maisha kabla ya kuendelea na ziara yao.
Ingawa hoteli ya Treetops haikuwa maarufu sana tangu ilipoanzishwa mwaka 1932, ilianza kupata umaarufu mkubwa duniani miaka 20 baadaye, yaani 1952, baada ya Elizabeth kuwa malkia wa Uingereza akiwa katika hoteli hiyo.
Kuanzishwa hoteli hiyo lilikuwa ni wazo la Eric Walker, mmiliki wa hoteli ya Outspan huko Nyeri, na mkewe, Lady Betti, binti wa Earl wa Denbigh.
Walker alikuwa mfanyabiashara wa hoteli na mwanzilishi wa Hoteli ya Outspan na Treetops Hotel nchini Kenya.
Anakumbukwa kama mwenyeji wa Malkia Elizabeth II na Prince Philip walipotembelea Treetops mwaka 1952, muda mfupi kabla ya kupokea habari za kifo cha Mfalme George VI na kutawazwa kwa Elizabeth kwenye kiti cha enzi.
Wawili hao, Walker na Betti, walikuwa wenyeji wa ziara hiyo, pamoja na mwanasayansi wa asili Jim Corbett, ambaye hifadhi ya Kitaifa ya Corbett nchini India imepewa jina lake.
Akiwa amestaafu kutoka India, Corbett aliishi katika nyumba ndogo huko Outspan iliyokaliwa hapo awali na Lord Robert Baden-Powell ambaye alikuwa ofisa wa Jeshi la Uingereza, mwandishi, mwanzilishi na Skauti Mkuu wa kwanza wa Vuguvugu la Skauti duniani kote.
Walker alihusika kuwavutia familia ya kifalme ya Uingereza kwenda Kenya. Akihitaji pesa baadaye ili kumwoa Lady Bettie, alisafiri kwa boti nne zilizobeba pombe ya magendo hadi Marekani na akauza shehena yake kimagendo.
Wakati mmoja alipambana kwa kurushiana risasi na maofisa wa serikali ya Marekani, akalazimika kukimbilia Canada, ambako alimuoa Lady Betti na kuhamia Kenya, ambako alijenga hoteli ya Outspan.
Walker aliweka sheria kali za msingi kwa ziara ya Treetops. Hakuna waandishi wa habari walioruhusiwa, kwani iliaminika harufu ya watu wengi ingewatisha wanyamapori. Hata kamera hazikuruhusiwa pia, kwa sababu binti mfalme alihitaji mapumziko.
Walinzi waliokuwa na mikuki kwenye ukingo wa msitu waliwazuia wavamizi wakati familia ya kifalme ilipofika kwenye shimo la maji na kupanda ngazi iliyosonga hadi kwenye hoteli hiyo na kukaa kwenye vyumba vitatu.
Tembo aliyekuwa karibu alikuwa umbali wa mita chache. Kulikuwa na nyani, nguruwe na mbawala pia.
Binti wa mfalme alitumia muda mwingi wa alasiri akipiga picha kwa kutumia kamera yake ya sinema, akiwa amechanganyikiwa sana hivi kwamba akaomba apewe chai pale pale aliposimama akiwatazama wanyama badala ya kuingia ndani.
Chui walivamia Treetops baada ya giza kuingia na binti wa mfalme akiwa amekwenda kulala. Aliamka tena alfajiri. Baada ya kifungua kinywa, saa nne asubuhi familia ya kifalme ilirejea Sagana.
Huko Uingereza, wakati huo huo, katika eneo la ‘Hyde Park Corner’ kuna jambo lilikuwa likiendelea.
Ulikuwa ni mpango wa kificho kuhusu kifo cha mfalme. Katika ofisi nambari 10 jijini London, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill, aliarifiwa mara moja kwamba mfalme alifariki dunia akiwa usingizini huko Sandringham, lakini ilikuwa saa nne kabla ya habari kumfikia binti yake akiwa nchini Kenya.
Telegramu ilitumwa jijini Nairobi lakini haikuweza kufunguliwa mara moja.
Wakati wa chakula cha mchana mhariri wa gazeti la 'East African Standard' alimpigia simu msaidizi wa binti mfalme, Martin Charteris, aliyekuwa katika Hoteli ya Outspan, kuuliza ikiwa taarifa zilikuwa za kweli.
Akiwa ameshtuka, Charteris aliwasiliana na Sagana, ambapo Prince Philip alijibu kana kwamba alikuwa amepigwa na radi.
Akiwa anakimbia haraka, alimchukua mke wake mwenye umri wa miaka 25 kwa matembezi katika bustani ya Treetops Hoteli ambapo, saa 8.45 usiku wa Februari 6, alimwambia kwamba baba yake alikuwa ameaga dunia na sasa alikuwa Malkia na mkuu wa Jumuiya ya Madola.
Alikimbizwa hadi kwenye uwanja wa ndege wa karibu, ambapo ndege ya Jeshi la Uingereza ya 'Dakota' ilikuwa ikimngoja kumrejesha nyumbani kwake Uingereza.
Malkia alikuwa na msongo wa mawazo aliposhuka kutoka kwenye gari, lakini alimudu kutabasamu. Aliingia ndani ya ndege akiwa hana mbwembwe za kawaida na akaondoka mara moja nchini Kenya.
Elizabeth II alikuwa malkia wa Uingereza tangu mwaka 1952 hadi kufariki dunia Septemba 8, 2022. Alikuwa malkia kwa miaka 70 na siku 214. Katika historia yote ya dunia hakuna mtawala aliyedumu madarakani muda mrefu kuliko yeye.
Alizaliwa kwa jina la Elizabeth Alexandra Mary Windsor mjini London Aprili 21, 1926 kama mtoto wa kwanza wa mfalme George VI wa Uingereza na Elizabeth Bowes-Lyon.
Kiti chake kitarithiwa na mtoto wake, Charles III wa Uingereza.
Baba yake Elizabeth alikubali kiti cha enzi mwaka 1936 baada ya kaka yake, Mfalme Edward VIII, kutekwa nyara kimapenzi na mwanamke wa Kimarekani, Wallis Simpson, na kumfanya Elizabeth kuwa mrithi wa Ufalme wa Uingereza.
Utawala wa muda mrefu wa Malkia Elizabeth II ulijawa na hisia kuu za kuwajibika na kujitolea kwake maisha yake yote kwa cheo chake kama malkia na pia kwa watu wake.
Kwa watu wengi, yeye alikuwa kitu kimoja ambacho hakikubadilika ulimwengu ulipokuwa unabadilika kwa kasi na nguvu za Uingereza duniani kupungua.
Jamii ilibadilika pakubwa na majukumu na manufaa ya familia ya kifalme nayo yakaanza kutiliwa shaka.
Kufanikiwa kwake katika kudumisha pamoja familia ya kifalme katika kipindi hicho cha misukosuko kulikuwa jambo kubwa sana, hasa ikizingatiwa kwamba wakati wa kuzaliwa kwake, hakuna aliyetarajia kwamba angeishia kuwa malkia, na kwa muda mrefu.