Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Faida, hasara za Rais Samia, Dk Nchimbi kuwa wagombea nje ya utamaduni CCM

Muktasari:

  • Uamuzi huo wa Mkutano Mkuu Maalumu umeondoa mchakato wa kawaida wa chama na kupunguza gharama, lakini pia umeminya fursa za kidemokrasia.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaanza kuendeshwa kwa “mizuka” au ni uthibitisho wa mahaba makubwa ambayo wajumbe wa Mkutano Mkuu wanayo kwa Mwenyekiti wao, Rais Samia Suluhu Hassan?

Januari 18 na 19, 2025, CCM waliandaa Mkutano Mkuu Maalumu. Ajenda zilikuwa mbili; kupitisha na kulipigia kura jina la Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, vilevile kupitia utekelezaji wa ilani ya chama.

Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara alipatikana. Ni Stephen Wasira, aliyechukua nafasi ya Abdulrahman Kinana, aliyeomba kustaafu. Mapitio ya utekelezaji wa ilani yalifanyika. Hata hivyo, ajenda iliyopamba Mkutano Mkuu ni iliyoingizwa kama wazo, lakini ikabadili upepo wote.

Matarajio yalikuwa baada ya Mkutano Mkuu wa CCM, jina ambalo lingefuatiliwa kwa ukaribu ni la Wasira. Imekuwa tofauti; majina yanayozungumzwa ni Rais Samia na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.

Mkutano Mkuu wa CCM umefanya uamuzi wenye mshangao mkubwa. Ni kuingiza hoja, ambayo baadaye iliundiwa azimio la kumpitisha Rais Samia kuwa mgombea urais wa CCM katika Uchaguzi Mkuu 2025.

Azimio likaruhusu mchakato. Zikapigwa kura. Wajumbe 1,924 waliohudhuria Mkutano Mkuu Maalumu walipiga kura za “ndiyo” Rais Samia kuwa mgombea urais. Kisha, Rais Samia akamteua Nchimbi kuwa mgombea mwenza.

Uamuzi huo wa Rais Samia unatoa majibu kuwa endapo atashinda kuendelea kwa muhula wa pili, atakuwa na makamu tofauti. Ni Dk Nchimbi, na siyo tena Dk Phillip Mpango, aliye ofisini kwa sasa.

Katiba ya CCM, ibara ya 104 (12)(b), Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, imepewa mamlaka ya kupitisha majina matatu wanaowania urais ili yapelekwe Mkutano Mkuu kwa ajili ya uchaguzi na kumpata mgombea mmoja.

Katiba ya CCM, ibara ya 105 (7)(b), imeipa mamlaka Kamati Kuu ya kupitisha majina matano ambayo yatawasilishwa Halmashauri Kuu ili kuchujwa; halafu watatu ndiyo wanapelekwa Mkutano Mkuu.

Mapitio hayo ya Katiba ya CCM yatakuonyesha kuwa Mkutano Mkuu umepoka shughuli za Kamati Kuu na Halmashauri Kuu. Hata hivyo, Katiba ya CCM, ibara ya 100 (2), inatamka kuwa Mkutano Mkuu ndiyo kikao kikuu cha chama kuliko vingine vyote, na uamuzi wa Mkutano Mkuu ni wa mwisho.

Kwa mantiki hiyo, uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM Januari 19, kuunda azimio, kisha kupiga kura za kishindo, ni halali na Rais Samia na Dk Nchimbi wana uhalali wa kuwakilisha chama chao kwenye kinyang’anyiro cha urais wa 2025.

Katiba ya CCM, ibara ya 103 (12)(c), inaeleza kuwa Halmashauri Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kumchagua mgombea urais wa Zanzibar. Siku zote, utamaduni wa CCM umekuwa kutekeleza utaratibu wa kikatiba kimchakato.

Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM ulimpitisha pia Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kuwa mgombea urais wa Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025. Kwa mara nyingine, Mkutano Mkuu ulipoka mamlaka ya Halmashauri Kuu, lakini Katiba ya CCM imekabidhi uamuzi wa mwisho kwa Mkutano Mkuu.


Faida ni zipi?

Maandalizi ya Mkutano Mkuu hugharimu fedha nyingi. Kiutamaduni, Sekretarieti ya CCM ingepaswa kuandaa kalenda ya uchaguzi, kutengeneza fomu za wagombea na kufungua dirisha ili wenye nia ya kugombea wajitokeze.

Kamati Kuu ingeketi, halafu Halmashauri Kuu ya Taifa, kabla ya Mkutano Mkuu. Kwa CCM kufanya uamuzi wa kumpitisha Rais Samia kuwa mgombea urais na Dk Nchimbi mgombea mwenza, maana yake hawahitaji tena vikao hivyo wala mchakato wa uchaguzi. Hiyo inasaidia kubana matumizi.

Inampunguzia Rais Samia hekaheka za kuomba idhini ya CCM: kuchukua fomu, kujaza, kuzungusha fomu kutafuta wadhamini, kisha kwenda kujieleza kwenye Mkutano Mkuu ili kuomba kuchaguliwa.

Inawezekana wangetokea wana-CCM wengine ambao wangetaka kumpa changamoto Rais Samia, hivyo mchakato ungekuwa mrefu kuanzia Kamati Kuu, Halmashauri Kuu hadi Mkutano Mkuu. Hivyo, uamuzi wa Mkutano Mkuu umeondoa hekaheka kwenye chama na umempunguzia ratiba ndefu Rais Samia.

Hata Rais Mwinyi naye ameondolewa presha za mchakato wa ndani ya chama. Angalau ana uhakika kuwa hana mpinzani kwenye chama chake. Anasubiri tume iitishe uchaguzi ili ashindane na wapinzani watakaojitokeza kutoka vyama vingine.


Hasara zake

Uchaguzi ni fedha. Chama kinapotengeneza fomu za wagombea, watia nia huzilipia. Kwa Mkutano Mkuu kuamua kwa kauli moja kuwapitisha Rais Samia na Mwinyi kuwa wagombea wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, vilevile Dk Nchimbi kuwa mgombea mwenza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maana yake hakutakuwa na ingizo la fedha za fomu.

Mkutano Mkuu umeminya fursa ya kidemokrasia. Pengine kuna wana-CCM waliokuwa na nia ya kujitokeza kuwania urais, wakiwa na hoja pamoja na ajenda zenye nguvu ambazo zingewezesha chama kuwa na upana wa machaguo kuelekea uchaguzi.

CCM wametengeneza mwanzo ambao miaka ijayo wanaweza kujuta. Kama ilivyotokea safari hii, nyakati zijazo anaweza kutokea kiongozi, kwa kuhofia kupingwa au kushindwa kwenye mchakato ndani ya chama, akaamua kuitisha Mkutano Mkuu na kurubuni wajumbe wapige mayowe ili ateuliwe nje ya utamaduni wa kikatiba.

Maana yake ni kwamba uamuzi wa kuwapitisha Rais Samia, Dk Mwinyi na Dk Nchimbi kuwa wagombea ni halali, bila wasiwasi kabisa. Wajumbe 1,924 waliohudhuria mkutano wanakidhi matakwa ya Katiba. Wajumbe wanne tu ndiyo waliokosekana. Pamoja na hivyo, gharama inaweza kuwa kubwa miaka ijayo.


Hatua za Nchimbi

Nchimbi, mtoto wa familia ya CCM. Baba yake, John Nchimbi, alikuwa ofisa wa polisi, aliyepanda ngazi hadi cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP). Kipindi cha chama kimoja, John Nchimbi alikuwa Mjumbe wa NEC – CCM, akiwakilisha majeshi.

Mzee John Nchimbi

Nchimbi (Emmanuel), ni mwajiriwa wa zamani wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuanzia mwaka 1998. Ajira ya Nchimbi NEMC ilikoma mwaka 2003, alipoteuliwa na Rais wa tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda.

Mwaka 2005, Nchimbi aliingia bungeni aliposhinda jimbo la Songea Mjini. Baada ya hapo akateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, akahamishwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, kisha Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Cheo cha naibu waziri katika wizara hizo tatu tofauti, Nchimbi alikitumikia kuanzia Januari 2006 mpaka Oktoba 2010. Novemba 2010, Nchimbi aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, kisha Mei 2012, alihamishwa kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Kashfa kubwa iliyoikumbuka Serikali kupitia Oparesheni Tokomeza Ujangili, majeshi ya nchi yalipopiga, kutesa na kunyanyasa raia, haikumwacha salama Nchimbi. Kama mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, inayoliongoza Jeshi la Polisi, alilazimika kujiuzulu. Ilikuwa Desemba 2013.

Jambo moja halina kazi kubwa kulithibitisha kuhusu Nchimbi ni kwamba ni mtu wa siasa za ushindani, anajiamini na anaweza kuzungumza fikra zake bila hofu. Anajua kutofautisha nyakati za kufanya siasa na kujenga nchi.

Kipindi ambacho Taifa lilinusa harufu ya mgawanyiko, baina ya wanasiasa wawili mashuhuri, Rais wa nne, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa nane, Edward Lowassa, minong’ono ikawa mingi kuhusu mafahari hao wawili, kila hatua, Nchimbi alibaki kuwa mtu pendwa kwa wote wawili. Lowassa wake, hivyohivyo Kikwete.

Lowassa alipokatwa jina kabla ya kufika Kamati Kuu CCM, kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya kuwa mgombea urais CCM, Uchaguzi Mkuu 2015, Nchimbi alikuwa mmoja wa wajumbe watatu, waliotokeza mbele ya vyombo vya habari na kueleza kutokukubaliana na uamuzi uliofanyika.

Nchimbi, aliongozana na makada wengine waandamizi CCM, Sophia Simba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake CCM (UWT) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa. Nchimbi alisema kwa niaba ya wenzake: “Tunajitenga na uamuzi wa Kamati Kuu kwa sababu kuna majina yaliondolewa kabla ya  kufika kwenye kikao.”

Hakutaja jina la Lowassa, ila alisema kilichofanywa kilikiuka Katiba ya CCM na kanuni za chama hicho, alichagiza kwa kusema, wao kama wajumbe wa Kamati Kuu, hawakukubaliana na uamuzi uliofanywa kwa sababu uliminya wanaokubalika kwa manufaa ya wasiokubalika.

Mwenyekiti wa CCM alikuwa Kikwete. Ndiye aliyeweka kanuni mpya zilizowezesha Lowassa kuondolewa kabla ya kufika Kamati Kuu. Kikwete aliongoza mkutano wa Kamati Kuu ambao Nchimbi, Sophia na Kimbisa, walitangaza kujitenga uamuzi wake.

Hicho ni kipimo kuwa Nchimbi hana hofu linapokuja suala la kuzungumza fikra zake. Alifanya hivyo dhidi ya Kikwete. Tafsiri za wengi zimebaki kuwa Nchimbi, Sophia na Kimbisa, walifikia uamuzi huo kwa sababu walimtaka Lowassa. Kauli “kuminya wanaokubalika”, ilimaanisha Lowassa ndiye alikubalika.

Msimamo wake huo ulimgharimu. Chupuchupu afukuzwe uanachama. Alipewa onyo kali na Halmashauri Kuu CCM. Kisha, akateuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, baadaye Misri, halafu alirejeshwa nchini na kukaa bila kazi kwa kipindi kirefu.

Januari 2024, Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu CCM, na sasa kinachoombwa ni uhai na afya, kisha wapeperushe bendera ya chama chao na kushinda uchaguzi. Baada ya hapo, Nchimbi atakula kiapo kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchimbi, kijana wa chama na alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) kwa mihula miwili. Ni mwanadiplomasia pia. Pengine historia yake ndiyo imemvutia Rais Samia kusimama naye.