Familia ya Sauli yaeleza miradi watakavyoisimamia, watoto watakavyoishi
Muktasari:
- Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabhila unazikwa leo Jumatano, Agosti 7, 2024 nyumbani kwao, Kijiji cha Godima, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya
Chunya. Familia ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabhila imesema kumpoteza mpendwa wao huenda baadhi ya miradi ikayumba hususan ya mabasi huku ikisisitiza imejipanga kusimamia vyema migodi ya dhahabu ili kuwasaidia watoto wake.
Mwalabhila maarufu kwa jina la Sauli, alifariki dunia Agosti 4, 2024 kwa ajali ya gari maeneo ya Mlandizi Mkoa wa Pwani na mwili wake ulisafirishwa jana Jumanne kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) hadi Songwe, Mkoa wa Mbeya.
Baada ya kuwasili, mwili huo ulisafirishwa kwenda wilayani Chunya mkoani humo kwa mazishi yanayotarajia kufanyika leo Jumatano,Agosti 7, 2024 nyumbani kwao Kijiji cha Godima huku msiba ukiwa nyumbani kwake Kibaoni.
Asubuhi ya leo Jumatano, Mwananchi imezungumza na Osward Mwasenge ambaye ni binamu wa marehemu anayesimamia machimbo ya madini, akisema yapo maeneo walimtegemea zaidi Sauli, hivyo ipo hofu ya baadhi ya miradi kuyumba.
Amesema sehemu ya mabasi walimtegemea yeye, lakini upande wa migodi watatumia njia alizokuwa akipita kuweza kuziendeleza kwa manufaa ya watoto wake takribani 10.
"Watoto wake bado wanahitaji msaada kwakuwa wakubwa wawili Octavian na Gravian Sauli ndio wamemaliza kidato cha nne na wengine bado wadogo, ni pigo kubwa kwa kuwa kuna miradi alitegemewa yeye hasa upande wa magari," amesema Mwasenge.
"Kwa upande wa migodi ninaposimamia mimi kwa miaka 10 sasa, sitarajii itetereke kwa kuwa alishatupa njia na tutatumia uzoefu kuweza kulinda rasilimali hii na kila kitu kitakuwa wazi kwa ustawi wa familia."
Mwasenge amesema: “Mabasi ya biashara yalikuwa manne japokuwa yalisimama kutoa huduma hivi karibuni ila alikuwa akishughulikia yarejee, mengine manne yalikuwa ya kutembelea ila moja ndilo limeharibika baada ya ajali, hivyo jumla yanabaki saba," amesema Mwasenge.
Binamu huyo ameongeza enzi za uhai wa Sauli, alipenda na kuwaamini sana ndugu zake ndio maana miradi yote aliikabidhi katika ukoo, hivyo kifo chake kimekuwa pigo na simanzi kubwa.
"Alikuwa mpenzi sana na watoto wake, ndio maana hata kwenye ajali alikuwa na mwanaye mdogo ambaye alijeruhiwa kidogo, tutakaa kikao kuamua nani aweze kuwa msimamizi mkuu wa familia na mali kwa jumla," amesema Mwasenge.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali kutoka msibani hapo.