Familia yatoa msimamo ndugu aliyekufa kwa kubanwa 'nyeti’, kuchomwa kisu na mkewe

Watoto wa marehemu Julius Lubambi wakiangua kilio wakati wa kuaga mwili wa baba yao, leo Alhamisi Aprili 4, 2024. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Ofisa kilimo anayedaiwa kuuawa na mkewe azikwa, familia yaiachia Serikali kuchukua hatua dhidi ya mtuhumiwa.

Mwanza. “Hatuwezi kusumbuana na mtu asiyetambua alichokifanya, tunaiachia Serikali.” Ni kauli ya Nicolaus Mzee, msemaji wa familia ya aliyekuwa Ofisa Kilimo Kata ya Neruma Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Julius Lubambi (39), anayedaiwa kufariki dunia kwa kubanwa nyeti na kuchomwa na kitu chenye ncha kali mwilini.

Julius ambaye ni mtoto wa tatu kati ya watoto 13 wa familia ya mzee Lubambi, anadaiwa kutendewa kitendo hicho na mke wake wa ndoa, Elizabeth Steven (30), Aprili 2, 2024.

Maziko ofisa kilimo huyo yamefanyika leo Alhamisi Aprili 4, 2024 katika makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwao Mtaa wa Isela Kata ya Usagara wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, huku maelfu ya wananchi wakiungana na ndugu kuhitimisha safari yake ya mwisho hapa duniani.

Mwili wa aliyefariki kwa kubanwa nyeti na kuchomwa kisu na mkewe ukizikwa

Mwili huo umezikwa kando mwa kaburi la mama yake na kaburi la mkewe wa kwanza aliyezaa naye watoto wawili, kabla ya kufunga ndoa na mtuhumiwa (Elizabeth), Oktoba, 2023 katika Kanisa la PAG Tanzania lililoko Usagara mkoani Mwanza. 

Akizungumza baada ya kuaga mwili huo, msemaji wa familia, Mzee ameliambia  Mwananchi Digital kuwa msimamo wao ni kutoendelea kumfuatilia mwanamke anayetuhumiwa kutekeleza kitendo hicho na badala yake wanakabidhi suala hilo kwa mamlaka zinazohusika.

Mzee amesema Julius tangu afunge ndoa na mwanamke huyo, hakuwahi kutoa taarifa ya kukwazana naye kimahusiano hadi pale walipopigiwa simu juzi kuwa amefariki kwa kushambuliwa na mkewe.

“Tumeamua, hatuna sababu ya kuendelea kuhangaika na mtu ambaye hajui analolifanya, Serikali ndiyo itakayoamua ifanye nini. Hatukutegemea mkwe wetu angefanya alichokifanya,” amesema Mzee.

Hata hivyo, amesema suala la usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 nalo huchangia kwa baadhi ya wanawake wasio na uelewa kutekeleza mauaji na ukatili kwa wanaume.

“Mke angetambua ana wajibu wa kumheshimu na kumtii mmewe, asingetekeleza shambulio hilo hata kama angepata taarifa ya mumewe kupata mtoto nje ya ndoa. Serikali isaidia kuelimisha jamii,” amesema Mzee.


Waombolezaji wakiaga mwili wa Julius Lubalmbi. Picha na Mgongo Kaitira.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi mkoani humo, Kashinje Masanja ambaye ni rafiki wa marehemu, mbali na kulalamikia sera ya usawa wa kijinsia kuchangia kupunguza utii wa baadhi ya wanawake kwa wenza wao, ametoa wito kwa wanaharakati kujitokeza hadharani kulaani mauaji hayo.
“Yawezekana kuna mahali tumekosea, ingekuwa mwanamke amekufa leo pangekuwa na kelele nyingi sana mitaani na mitandaoni, lakini kwa kuwa ni mwanaume, wako kimya, tumeumia sana. Nilikuwa namuita ‘Podolski’ kwa kweli alikuwa mcha Mungu sijui imekuwaje, mtuombee,” amesema Masanja.
Kauli ya Masanja inaungwa mkono na Mchungaji wa Kanisa la PAG Tanzania, Amos Festo aliyewataka ndugu wa marehemu kumuombea kwa kile alichodai kuwa mtuhumiwa ameondoa uhai wake, lakini si roho yake, huku akiwataka waombolezaji kumrudia Mungu.
Pia, ameiomba jamii na ndugu wa marehemu kutolipiza kisasi, badala yake waiachie Serikali, mamlaka za uchunguzi na kisheria kuchukua hatua stahiki kwa mtuhumiwa.
“Mauaji haya yameanza kuibua hisia kwamba Mkoa wa Mara ni wa watu wakatili, kitu ambacho siyo sahihi…shetani ndiyo chanzo cha yote haya, akiingia ndani ya mtu anaivaa roho yake haijalishi anasali au hasali,” amesema Mchungaji Festo.
 

Kauli ya Serikali

Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Pereus Kyaruzi amesema Julius baada ya kuhitimu Chuo cha Kilimo na Ushirika Ukirigulu mkoani humo, aliajiriwa mwaka 2012 katika halmashauri hiyo kama ofisa kilimo daraja la tatu.
Kyaruzi amesema alihudumu katika wadhifa wa ofisa kilimo Kata ya Namibu kabla ya kuhamishiwa Neruma wilayani Bunda mkoani humo na alitarajiwa kupandishwa cheo hadi Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi Mei, mwaka huu.

“Alikuwa mchapa kazi, pamoja na kuwa alikuwa anasimamia idara ya kilimo kata ya Neruma, lakini alikuwa anakaimu na Kata ya Chitengule, nadhani mnaweza kuona alikuwa mchapakazi wa aina gani. Tutamkumbuka na kuikumbuka familia yake,” amesema Kyaruzi kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia, marehemu, Julius Lubambi alizaliwa Januari 25, 1985, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kisha kuhamia Usagara mkoani Mwanza kabla ya kuanza elimu yake ya msingi wilayani humo na kujiunga sekondari ya Geita mkoani Geita mwaka 2005.

Baada ya kuhitimu elimu ya Sekondari mkoani Geita, mwaka 2010 alijiunga na kusoma Astashahada ya Kilimo katika Taasisi ya Kilimo na Ushirika Ukiriguru iliyopo Misungwi mkoani Mwanza hadi alipohitimu na kuajiriwa kama Ofisa Kilimo daraja la kwanza Januari 23, 2012 katika Kata ya Namibu wilayani Bunda.

Anasema marehemu kutokana na utendaji kazi wake alikuwa akipandishwa cheo mara kwa mara kwa mujibu wa sheria, ambapo taarifa ya mwajiri wake inaeleza kwamba Mei, mwaka huu alitarajiwa kupandishwa cheo hadi kuwa Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi.