Fisi aua mtoto wa miaka miwili Tabora

Muktasari:

Baada ya fisi kushambulia na kumuua mtoto huyo, taharuki ilitokea kila mwananchi  akidai kamuona fisi hadi askari wanyamapori walipomuua kisha wananchi kuoneshwa mzoga wake ndipo hali ikawa shwari.

Tabora. Mtoto wa miaka miwili, Eliud Jerome ameuawa na fisi wakati akiwa na wenzake wakitafuta kuni.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Aprili 7, 2023 Diwani wa Kata ya Zugimlole Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ambapo tukio hilo limetokea, Balikeka Ramadhan amesema Aprili 4, 2023 Saa moja jioni Eliudi akiwa na wenzake watatu ndipo fisi huyo aliwashambulia kisha kuondoka naye.

“Mtoto aliyeuawa ndiye alikuwa mdogo miongoni mwao, mkubwa akiwa na umri wa miaka saba,”amesema

Amesema walimtafuta usiku huo na kuamua kusubiri hadi kesho yake (Jumatano) ambapo walifuata alama za fisi nakuona sehemu za mwili alizokuwa anadondosha njiani ukiwemo utumbo wa mtoto.

Diwani huyo amesema baada ya mabaki kupatikana yalizikwa na wananchi huku akidai licha ya tukio hilo kuwa la kwanza kwa mwaka huu lakini kata yake imekuwa ikisumbuliwa sana na fisi.

Amesema mwaka jana fisi walijeruhi watu nane katika matukio mawili tofauti la kwanza, akijeruhi watu sita na la pili watu wawili waliokatwa vidole huku mwaka juzi mnyama huyo alishambulia mtoto na kumuua kisha nayeye kuuawa baada ya kukwepa risasi kadhaa.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao amesema baada ya fisi kumshambulia Eliud, askari wanyamapori walienda eneo la tukio na kufanikiwa kumuua fisi huyo.

Kata ya Zugimlole inapakana na hifadhi mbili za Luganjo Tongwe na Mto Ugalla ambazo zina wanyama mbalimbali wakiwemo fisi.