Gaddafi alivyompindua Idris akiwa na miaka 27

Friday October 22 2021
gadaffpic
By William Shao

Wakati akipanga njama za kuipindua Serikali ya Mfalme Idris, Muammar Gaddafi alinusurika kukamatwa mara kadhaa.

Pia tarehe ya kufanya mapinduzi nayo iliahirishwa mara kadhaa na mara nyingi kati ya hizo ni kwa sababu baadhi ya vitengo vyake havikupokea maagizo kwa wakati. Mwisho tarehe mpya ilipangwa ambayo ni Jumatatu ya Septemba 1, 1969 kwa sababu kadhaa na ikaamuliwa kuwa kutokana na sababu hizo, hakuna tena kurudi nyuma lazima kazi ifanyike.

Kwanza, waliopanga mapinduzi walijua kuwa mamlaka ilikaribia kuwagundua na kuwakamata kabla ya kufanikisha malengo. Pili, majaribio yao mengi ya kufanya mapinduzi yalishindwa kabla hayajaanza. Tatu, baadhi ya vijana walioandaliwa walikuwa wanaanza kukata tamaa na Nne, katika tarehe hiyo maofisa wengi jeshini walikuwa wamepangwa kutumwa kwenda Uingereza kwa mafunzo mwanzoni mwa Septemba.

Tangazo la kwamba maofisa hawa walikuwa karibu kupelekwa nje ya nchi lilizua hofu kati ya wanamapinduzi. Gaddafi alijua kwamba ikiwa hatachukua hatua haraka, angepoteza ndoto yake hiyo aliyoiota kwa muda mrefu.

Akiwa kama vile anakaribia kupatwa na wazimu, yeye na baraza lake la mapinduzi walianza kujiandaa. Waliandika mipango yao na kuweka katika bahasha ambazo zilifungwa kwa nta nyekundu na kusambazwa kwa viongozi wa vikundi vidogo vidogo vya siri alivyounda.

Gaddafi na wenzake walitumia siku kadhaa mwishoni mwa Agosti 1969 wakizunguka nchi nzima, wakiwajulisha wanamapinduzi wenzao kuwa wakati umefika.

Advertisement

Katika mkesha wa mapinduzi, Gaddafi alisisitiza kwamba wanamapinduzi watekeleze majukumu yao kama kawaida na kutoonyesha dalili yoyote itakayodokeza kuna jambo litataokea. Wakati mmoja Gaddafi alikumbuka: “Sikuruhusu shauku au woga kujionyesha.”

Usiku wa Agosti 31, 1969, baada ya maandalizi yote kukamilika yeye na mmoja wa washirika wake katika mapinduzi Mustafa Kharroubi, walilala kitanda kimoja katika chumba chake na kusikiliza redio ya ‘Sauti ya Waarabu’ kutoka Cairo wakingojea itimie saa 8.30 usiku. Kituo hicho cha redio kilirusha aya kadhaa za Korani. Aya moja ilisema: “Mwenyezi Mungu hatawanyima waaminifu tuzo yao.”

Akiichukulia hii kama ishara njema, Gaddafi alisema: “Aya hizi zilitufanya tujisikie salama na watulivu. Tuliambiana kuwa ‘Msaada wa Mwenyezi Mungu unatutosha. Yeye ndiye mlinzi bora’ na tulipata uhakika wa kufanikiwa.”

Jambo la kwanza walilopanga kufanya ni kuteka vituo ya redio hususani cha Tripoli ambacho aliyepangwa kukiteka ni Khweildi Al-Humaidi na kile cha Benghazi kingetekwa na Gaddafi mwenyewe.

Kama ilivyotarajiwa, wanamapinduzi hawakupata upinzani mkubwa, ni kama vile Serikali ya Mfalme Idris ilikuwa imepigwa ganzi. Kikosi cha Ulinzi cha Cyrenaican, ambacho ni cha wasomi kilichoundwa na Mfalme Idris kuulinda ufalme wake, kilishindwa kwa urahisi baada ya kamanda wake Brigedia Sanussi Fezzani kukamatwa akiwa nyumbani kwake amelala kitandani.

Hata mkuu wa jeshi la Libya, Kanali Abdul Aziz Al-Shelhi, hakuleta upinzani wowote. Wakati Al-Meheishi na Abu Bakr Younis walipokwenda nyumbani kwake kumkamata, mkuu wa jeshi la Libya alijizamisha kwenye dimbwi lake la kuogelea akiwa amevalia nguo zake za kulalia. Alipotafutwa hakugundulika haraka alikokuwa amejificha hadi asubuhi iliyofuata.

Wakati huo huo Mfalme Idris alikuwa nje ya nchi kwa mapumziko.

Aliposikia habari za mapinduzi, Idris alidaiwa kuwa alipuuzia akisema hilo ni “jambo la uongo” na akaahidi kurudi nchini mwake kuendelea na majukumu. Ni wazi alitegemea msaada wa Waingereza. Siku moja baada ya mapinduzi alituma ujumbe maalumu kwenda London ili kuomba msaada. Hata hivyo, hakuelewa kuwa nyakati zimebadilika. Hakupata msaada aliouomba. Bila msaada wowote wa ulinzi kutoka nchi yoyote ya kigeni, utawala wa Kifalme wa Libya ulianguka haraka sana na hakukuwa na umwagaji damu mkubwa. Hata jeshi la kifalme lililoitwa Cyrenaica halikuweza kupambana kwa jinsi lilivyoshtukizwa.

Hii ilidhihirisha ukweli kwamba kufikia 1969 kulikuwa na ombwe kubwa la kisiasa lililokuwa likisubiri kujazwa. Ingawa kufanikiwa kwa mapinduzi kulitokana na udhahifu wa utawala wa Mfalme Idris, Gaddafi na wafuasi wake walikuwa wamezisoma alama za nyakati, hususani walipoona maandamano ya kuupinga ufalme wa Libya yaliyofanyika katika mitaa ya Tripoli na Benghazi. Pia walionekana kama wanaokuja kukidhi haja za Walibya wengi waliotaka utaifa wa Kiarabu, badala ya kuegemea nchi za Magharibi.

Ilipofika saa 12:30 asubuhi ya Septemba 1, 1969, Walibya waliamshwa na sauti isiyo ya kawaida ya Gaddafi kupitia redio ya nchi hiyo. Katika tangazo lenye msisimko, ambalo alidai kuwa limeandikwa katika dakika za mwisho kabisa, Gaddafi ambaye wakati huu alikuwa na umri wa miaka 27, kwa kujigamba alitangaza:

“Watu wa Libya! Kwa hiari yetu wenyewe, tukitimiza matakwa yetu ya dhati, kujibu mahitaji yetu ya kudumu ya mabadiliko na kuzaliwa upya kwa Taifa la Libya na hamu yetu ya kufikia malengo haya; vikosi vyako vya jeshi vimechukua hatua ya kuuangusha utawala wa ovyo na ufisadi, uvundo ambao umetuuguza na kutuogofya sisi sote ...Tangu leo Libya ni jamhuri huru, inayojitawala ... Itasonga mbele kuelekea barabara ya uhuru, njia ya umoja na haki za kijamii, kuhakikisha usawa kwa raia wake wote na kufungua mbele yetu milango ya ajira na kufuta udhalimu na unyonyaji. Hakuna mtu atakayejiona kuwa bwana au mtumishi, na itakuwa nchi yenye uhuru. Tutakuwa ndugu ndani ya jamii ambayo kwa msaada wa Mungu, mafanikio na usawa vitatutawala sisi sote.”

Hatimaye kulipopambazuka asubuhi ya Septemba 1, Walibya hawakujua ni nani hasa aliyempindua mfalme wao. Lakini Baraza la Makomando wa Mapinduzi lilipotambulisha wajumbe wake kumi na mbili (RCC), ilidhihirika kuwa viongozi wapya wa nchi hiyo walikuwa wa kizazi tofauti sana na waliokuwa madarakani kabla ya kupinduliwa.

Kinyume kabisa na wale ambao walikuwa wamefanikiwa chini ya mfalme, viongozi wengi wa RCC walitoka katika makabila madogo na jamii ya chini katika familia masikini. Wengi walikuwa watoto wa wahamiaji au wakulima wa hali ya chini. Mara tu Gaddafi alipoiondoa madarakani serikali ya kifalme, alitangaza Jamhuri ya Libya. Kwa sababu ya asili ya mapinduzi ambayo hayakumwaga damu, mwanzoni aliyaita “Mapinduzi Meupe”, ingawa baadaye yalipewa jina “Mapinduzi ya Septemba Moja” kutokana na ukweli kwamba yalifanyika Septemba 1, 1969.

Alitangaza kuwa mapinduzi hayo yalimaanisha “uhuru, ujamaa na umoja”, na kwamba kwa miaka ijayo angetekeleza hatua za kulifanikisha hili.


Asili ya Gaddafi

Gaddafi alizaliwa na kulelewa na wazazi wake ambao walikuwa wafuga mbuzi, Mzee Abu Miniar na mkewe Aisha Ben Niran, wote wakiishi katika hali ya umaskini na wakati mwingine wakifanya biashara ya mahema.

Familia hiyo ilikuwa sehemu ya ‘Qaddadfa’, kabila la Kiarabu la Waberber linalojumuisha koo kadhaa ndogo ambazo zimeenea kote nchini Libya. Alipozaliwa alipewa jina la Muammar Mohammed Abu Minyar Gaddafi.

Itaendelea kesho

Advertisement