Gharama za matibabu sababu wengi kuishi na maradhi
Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Vulfrida Kyara, akimpima presha ya macho mkazi wa Mjimpya, Hamis Kamchoche (65), wakati wa kambi ya siku tano ya huduma ya matibabu ya macho bure inayoendelea katika Kituo cha Afya cha Al-Jamih for Mother and Child Health Care, Msamvu Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Muktasari:
- Zaidi ya wananchi 942 wamejitokeza siku ya kwanza ya kambi ya matibabu ya macho bure, huku wagonjwa 50 wakifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho.
Morogoro. Gharama kubwa za matibabu zimeendelea kuwa kikwazo kwa wananchi wengi, hali inayowalazimu kuishi kwa miaka mingi na maradhi yanayoweza kutibika kwa urahisi iwapo wangepata huduma za afya kwa wakati.
Hali hiyo imejidhihirisha katika kambi ya matibabu ya macho bure inayoendelea Morogoro, iliyoratibiwa na Taasisi ya Islamic Foundation kwa kushirikiana na Mercy Outreach Global ya Tanzania Cataract Surgery katika Kituo cha Afya cha Al-Jamih for Mother and Child Health Care, Msamvu.
Siku ya kwanza ya kambi hiyo, wananchi 942 walijitokeza kupata huduma. Kati yao, wagonjwa 892 walifanyiwa uchunguzi, kupatiwa dawa na miwani, huku 50 wakifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho.
Wananchi kutoka Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Mtwara, Manyara na Dodoma walifika kupata huduma hizo ambazo wengi wamesema zimekuwa nje ya uwezo wao wa kifedha.
Daktari wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Mashaka Matundwe, akimweka dawa mkazi wa Mtaa wa Shule, Kata ya Chamwino, Eliza Mgoa, wakati wa kambi ya siku tano ya huduma za matibabu ya macho bure inayoendelea katika Kituo cha Afya cha Al-Jamih for Mother and Child Health Care, Msamvu Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Mkazi wa Kijiji cha Manka, Korogwe mkoani Tanga, Sofia Kihiyo (65) amesema aliishi kwa muda mrefu na tatizo la kuona hafifu kabla ya kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho uliomrejeshea uwezo wa kuona.
“Nilikuta mamia ya wananchi tayari wamefika tangu asubuhi. Hii inaonyesha wazi kuwa watu wenye matatizo ya afya ni wengi, lakini wengi wao wanakosa uwezo wa kupata matibabu kwa wakati,” amesema Sofia.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), Zainabu Issa (21), amesema aliishi na uvimbe wa jicho kwa zaidi ya miaka mitano kabla ya kufanyiwa upasuaji ulioboresha hali yake.
Naye Eliza Mgoa wa Chamwino, Dodoma, amesema alikuwa akiugua mtoto wa jicho kwa zaidi ya miaka sita kabla ya kufanyiwa upasuaji uliorejesha uwezo wake wa kuona.
Kwa upande wake, Halima Ally (88) wa Kiteto, Manyara, amesema sasa anaweza kujihudumia mwenyewe baada ya kufanyiwa upasuaji.
Daktari wa Macho katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Mashaka Matundwe, amesema mtoto wa jicho ni miongoni mwa visababishi vikuu vya upofu lakini unatibika kwa upasuaji, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kufanya uchunguzi wa macho mara kwa mara.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Islamic Foundation, Mussa Buruki, amesema kambi hiyo iliyoanza Juni 15 na itakayomalizika Juni 20,2026 inalenga kuwafikia wananchi 2,000. Kupitia ufadhili kutoka Uingereza, zaidi ya miwani 1,500, dawa za macho na huduma za upasuaji zinatarajiwa kutolewa.
“Tunataka kuwafikia maelfu ya wananchi ambao hawana uwezo wa kupata huduma hizi kwa urahisi na kuchangia kupunguza tatizo la upofu unaozuilika nchini,” amesema Buruki.