Gwiji wa soka duniani, Maradona afariki dunia

New Content Item (1)
Gwiji wa soka duniani, Maradona afariki dunia

Muktasari:

GWIJI wa soka duniani raia wa Argentina anayekumbukwa kwa bao lao la mkono katika Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1986, Diego Maradona amemaliza mwendo duniani, baada ya kufariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo (cardiac arrest).

GWIJI wa soka duniani raia wa Argentina anayekumbukwa kwa bao lao la mkono katika Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1986, Diego Maradona amemaliza mwendo duniani, baada ya kufariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo (cardiac arrest).

Mauti yamkuta staa huyo wa duniani ambaye hawakuwahi kuishiwa vituko, wiki mbili mbili tangu aliporuhusiwa kutoka hospitalini alipofanyiwa upasuaji wa kichwa kuondoa damu iliyoganda kwenye ubongo.

Maradona aliyekuwa na umri wa miaka 60, anakumbukwa na wapenzi wa soka na kutajwa kama mtu aliyekuwa akichukiwa na Waingereza kutokana na tukio lake la mwaka 1986 alipoisaidia nchi yake ya Argentina kuing'oa England katika hatua ya robo fainali na kwenda kubeba ubingwa.

Katika mchezo huo ambao England ililala mabao 2-1, Maradona alifunga mabao yote mawili, moja la dakika ya 51 likiwa la mkono alililoita 'bao la mkono wa Mungu' na jingine akisepa na kijiji dakika nne tu baada ya kuwatia hasira kwa bao hilo lilimpa umaarufu mkubwa duniani.

Katika fainali hizo zilizofanyikia Mexico, Argentina walitwaa ubingwa kwa kuwafunga Ujerumani (enzi hizo Ujerumani Magharibi) kwa mabao 3-2.

Enzi za uhai wake, Maradona alianza kuwika katika kikosi cha Argentinos Juniors na kucheza michezo 167 huku akifunga mabao 116 kuanzia mwaka 1976–1981.

Timu nyingine alizowahi kuzichezea ni Boca Juniors aliyostaafuia mwaka 1997, lakini akitamba na Barcelona, Napoli, Sevilla na Newell's Old Boys.

Pia Maradona alikuwa kocha wa kikosi cha Argentina wakati wa Kombe la Dunia Afrika Kusini mwaka 2010 na kuishuhudia Hispania ikitwaa ubingwa na mara ya mwisho alikua akiifungisha Klabu ya Gimnasia de La Plata kuanzia mwaka jana.

Kwa taarifa zaidi usikose Mwanaspoti la kesho Alhamisi.