Hali tete shule kongwe wilayani Rungwe
Muktasari:
- Mkakati wa kukarabati shule hizo umebainishwa wakati, baadhi ya madiwani wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya wakihoji ucheleweshwaji wake.
Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya imesema iko kwenye mchakato wa kutenga bajeti, kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule kongwe na chakavu zaidi ya 30 zilizojengwa tangu nchi ipate uhuru.
Hayo yameelezwa leo Agosti 22, 2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mpokigwa Mwankuga alipozungumza na Mwananchi.
Amesema ukarabati wa shule hizo ni miongoni mwa mikakati ya halmashauri ya Rungwe kuona wanafunzi wanakuwa sehemu salama.
Kauli ya Mwankunga imekuja kufuatia hoja walizotoa madiwani wiki iliyopita, wakitaka shule kongwe wilayani humo zikarabatiwe.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wiki iliyopita, Diwani wa Kata ya Matwebe wilayani humo, Samweli Mwakasege alihoji ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya elimu ya msingi kufuatia kuwepo kwa majengo chakavu yaliyojengwa enzi ya mkoloni ambayo yanavuja msimu wa mvua na wanafunzi kusoma kwa tabu.
"Tunaona Serikali inatenga fedha katika ujenzi wa vituo vya afya lakini kuna shule zina hali mbaya ikiwemo ya Igongwe ambayo ilijengwa tangu enzi za mkoloni, kwa sasa majengo ni mabovu yanavuja msimu wa mvua,’’ amesema.
Akizungumza leo na Mwananchi, Ofisa Elimu Wilaya ya Rungwe, Juma Mwajombe amekiri kuwepo kwa changamoto hizo kwenye shule zaidi ya 30, akisema kwa sasa kuna mradi wa Boost unaolenga kuzikarabati shule hizo.
"Kama ilivyoelezwa kuna shule zaidi ya 30 chakavu katika Wilaya ya Rungwe ambazo zinavuja hali ambayo watoto wanasoma katika mazingira magumu, lakini serikali imeleta fedha kupitia mradi wa Boost ambazo malengo yake ni kujenga vyumba vya madarasa vipya na sio ukarabati," amesema.
Amesema ujio wa mradi wa Boost ni suluhisho kubwa kwa kujenga miundombu mipya ya vyumba vya madarasa, huku halmashauri ikiweka mipango mikakati ya kuboresha.