Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatari matumizi ya dawa za kupunguza vitambi wanawake

Muktasari:

  • Kiribatumbo au kitambi, ni changamoto inayowanyima usingizi wanawake wengi, wakijikuta wakihaha namna ya kukabiliana nayo. Baadhi hulazimika kutumbukia kwenye matumizi ya dawa, kubana matumbo kwa mikanda maalumu, kujinyima ama kuacha baadhi ya vyakula kwa muda kwa madai wapo kwenye ‘diet’.

Kiribatumbo au kitambi, ni changamoto inayowanyima usingizi wanawake wengi, wakijikuta wakihaha namna ya kukabiliana nayo. Baadhi hulazimika kutumbukia kwenye matumizi ya dawa, kubana matumbo kwa mikanda maalumu, kujinyima ama kuacha baadhi ya vyakula kwa muda kwa madai wapo kwenye ‘diet’.

Pamoja na mbinu hizo, wengi wamekuwa wakiona tatizo likiongezeka, huku wengine wakikata tamaa juu ya mbinu wanazotumia kwa kukosa majibu ya yale yanayowasibu.

Licha ya mbinu hizo, bado wengi hawajafahamu chanzo kikubwa cha tatizo hilo ni aina ya vyakula wanavyokula, kunywa na kutozingatia mazoezi.

Ni kama anavyoeleza Monica Peter, mkazi wa Kimara ambaye hakosi kula chipsi pamoja na vinywaji vyenye sukari kila siku.

“Kuwa na kitambi inakera, hasa kwa wanawake, nipo kwenye ‘diet’, sili kwa kiwango ambacho nilikuwa nikifanya hivyo awali. Kula chipsi ni mara moja kwa siku na hii haiwezi kuwa sababu ya tatizo kwa kuwa situmii chakula hicho kila wakati,” anaeleza.

Kwa upande wake, Tahiya Shomari, anasema kuna wakati alikuwa akijinyima kula baadhi ya vyakula huku akitumia dawa zilizomfanya aharishe kwa ajili ya kupunguza kitambi, lakini alifanikiwa kwa muda, kwani sasa baada ya kuacha kitambi kimeongezeka maradufu.

“Nilitumia pesa nyingi kununua hizo dawa, matokeo niliyaona, lakini nilipoacha kuzitumia kitambi kilirudi. Niliamua kuacha kwa kuwa licha ya kutumia pesa nyingi nilijiona nakuwa mtumwa wa hizo dawa,” anasema.



Tatizo likoje

Upatikanaji wa vyakula vilivyoandaliwa kwa haraka, unywaji wa vimiminika ya viwandani na kutozingatia mazoezi unaweka shakani afya ya wanawake wa mijini ikilinganishwa na vijijini.

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS-MIS 2015-2016) unaonyesha asilimia 43 ya wanawake wa mijini ni wazito au wanene mara mbili ya wale wa vijijini.

Utafiti huo uliohusisha wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 ulionyesha, mwanamke mmoja kati ya 10 Tanzania ni mwembamba sana, lakini asilimia 28 ya wanawake wana uzito uliokithiri au wanene sana.

Mtaalamu wa Lishe Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji, anaungana na utafiti huo akionyesha utafiti walioufanya mwaka 2020 wakiangalia hali ya uzito mkubwa jijini Dar es Salaam.

Husna kupitia utafiti walioufanya wakishirikiana na wataalamu mbalimbali anabainisha utafiti huo ulihusisha watu 6,691 Dar es Salaam na ikabainika asilimia 67.2 walikutwa na uzito au unene kupita kiasi.

Waliohusishwa kwenye utafiti huo ni wenye umri kati ya miaka 43 na kuendelea, ambapo asilimia 54.2 walikuwa wanaume, lakini wengi waliobainika kuwa na uzito uliopitiliza ni wanawake.

Wengi waliobainika kwenye utafiti huo ni watumiaji wa pombe wa mara kwa mara, sigara na asilimia 88 hawakuwa wakiushughulisha mwili, yaani kushiriki mazoezi.


Kitambi ni tatizo

Husna anasema mtu anapokuwa na kitambi inaamanisha ana mafuta mengi yaliyohifadhiwa karibu na ogani muhimu mfano tumbo, ini, figo, kongosho na moyo.

Kuhifadhiwa kwa mafuta hayo ndiko anakotaja Husna kuwa humfanya mtu kuwa na umbo kama la tunda ‘apple’, akiongeza kuwa utafiti unaonyesha wenye umbo la ‘apple’ au kitambi wapo hatarini zaidi kupata magonjwa yasiyoambukiza, akitolea mfano shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani na unene kupita kiasi.

Anasema kumekuwa na ongezeko kubwa la vitambi kwa wanawake (hasa wanapofikia kipindi cha kukoma hedhi (menopause) kuliko wanaume hasa kwenye nchi zinazoendelea.

“Kinachosababisha kitambi ni mtindo mbovu wa maisha kama matumizi mengi ya vilevi na tumbaku, kutokuzingatia mlo kamili, kutokufanya mazoezi, pia shida za homoni ‘hormnal imbalance’ na matatizo ya ovari PCOS (polycytic ovarian syndrome) ambavyo vingi huwapata wanawake.


Njia zinazotumika

Husna anabainisha kuwa katika kukabiliana na tatizo la vitambi, wanawake wengi wamejikuta wakitumia njia au kanuni za lishe ambazo si sahihi na kuziita ‘diet’.

“Wengi tunazisikia hizi ‘diet’ kwani nyingi ni maarufu na huahidi matokeo makubwa ya kupungua ndani ya muda mfupi.

“Mfano kuacha kula kabisa baadhi ya makundi ya chakula, kula mlo moja bila kuzingatia uwiano katika sahani au kuacha kula na kitumia supplements. Diet hizi nyingi zinakuwa si salama na si sahihi kwa asilimia kubwa ya watu, kwani huwa hazizingatii virutubisho vyote, mtumiaji anakuwa hatarini kupata micronutrient diffieciency (upungufu wa virutubisho mwilini),” anasema.

Matatizo mengine anayotaja mtaalamu huyo ni upungufu wa damu, ngozi kusinyaa na kunyauka (kuwa kama mzee), udhaifu na kuchoka na kushindwa kuhimili mlo.


Hatari ya ‘diet’

Husna anataja hatari ya kile wengi wanasema kuwa wapo kwenye ‘diet’ kwamba, punde baada ya kuacha ‘diet’ yenyewe mtu huongezeka mara mbili zaidi ya awali.

“Kitambi ni tatizo kama tatizo lingine la afya, mhusika anahitaji msaada wa karibu zaidi kutoka kwa wataalamu wa lishe ambao hupatikana kwenye hospitali za wilaya, mikoa na Taifa kuhusu mlo kamili na mtindo bora wa maisha.

“Mahitaji ya mwili hutegemea zaidi umri, jinsia, hali ya afya kwa wakati husika na shughuli za kila siku, hivyo ni muhimu kuzingatia haya pia kwa mtu mwenye kitambi ili kuhakikisha anakabiliana na kuondoa kitambi, wakati huo huo anakuwa na hali nzuri ya lishe (kutokupata utapiamlo),” anaeleza.

Mtaalamu wa Lishe Manispaa ya Kinondoni, Janet Mzava anasema mrundikano wa mafuta mwilini usio na kazi ni kivutio cha magonjwa kama kiharusi na pia kisababishi cha mtu kuugua mara kwa mara, mfano kupata mzio (allegy), mifupa kuuma na tatizo la usagaji wa chakula.


Mambo ya kufanya

Janet anasema wanawake wengi wameonekana kuwa na vitambi kwa sababu ya ulaji usiozingatia mchanganyiko wa vyakula kutoka makundi matano, yaani kundi la nafaka mizizi na ndizi, mikunde, wanyama samaki na mazao kama mayai na maziwa.

Pia mboga mboga, matunda na kuweka umakini kwenye kundi la mafuta, sukari na pombe.

“Mafuta, sukari na pombe ndiyo yanaliwa zaidi na makundi haya, ndiyo yanasababisha mrundikano wa mafuta mwilini na huleta magonjwa,” anasema.

Kwa upande wake Husna anashauri watu kupunguza matumizi ya vyakula vya wanga vilivyokobolewa, matumizi ya sukari na mafuta hasa yatokanayo na wanyama, kuepuka vyakula na vinywaji vilivyosindikwa kwani huwa na mafuta na chumvi nyingi.

“Kuwa na ratiba sahihi ya kula chakula, pia kuepuka kuchelewa sana kula chakula usiku na kula chakula kingi, epuka matumizi ya tumbaku, sigara, shisha na matumizi ya pombe kupindukia na jenga tabia ya kufanya mazoezi walau dakika 150 kwa wiki,” anaeleza.


Uchunguzi wa afya

Husna anashauri mtu kujijengea tabia ya kufanya uchunguzi wa afya, hasa kutambua BMI (uwiano kati ya uzito na urefu wako), uwiano wa mzunguko wa kiuno na hips.

Anasema hiyo husaidia kujenga umakini na ongezeko lolote la uzito, hivyo kumfanya mtu achukue tahadhari mapema.

“Wengi kwenye hatua za awali za kitambi hawachukulii umakini hadi pale wanapokuwa tayari mtu kashaathirika na magonjwa mengine kama ya moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani,” anasema.

Husna anaeleza jamii ikiwa makini na lishe itaepuka matatizo na magonjwa mengi, hasa yasiyoambukiza.

“Isipozingatia lishe bora basi itaangamia. Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2006 inaonyesha vifo milioni 41 kila mwaka hutokea kutokana na magonjwa yasioambukiza sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani.

Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu yanaongoza kwa kuwa na vifo milioni 17.9 kwa Tanzania magonjwa yasiyo ya kuambukiza husababisha asilimia 27 ya vifo vyote vinavyotokea kwa mwaka.

“Hivyo ni muhimu jamii kuwa na uelewa wa masuala ya lishe kutoka kwa ofisa lishe. Pia ni muhimu kuzingatia makundi yote ya chakula kwenye sahani ambayo ni vyakula vya wanga na mizizi, protini, mboga za majani, matunda na kundi la mafuta na sukari.

“Vilevile kula kwa uwiano sahihi, ili kukidhi mahitaji yote ya mwili na kuepusha uwezekano wa kupata kitambi,” anabainisha Husna.

Husna anabainisha kuwa, vipo visababishi vingi vya magonjwa yasiyoambukiza, lakini lishe bado inaonekana ni kisababishi kikubwa kwa mtu kupata magonjwa hayo mapema na haraka zaidi.

Anaeleza kuzingatia lishe na mtindo bora wa maisha, mtu ataepukana na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa na magonjwa ya figo.


WHO

Takwimu za mwaka 2016 za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha zaidi ya watu bilioni 1.9 walikuwa na uzito kupitiliza na watu milioni 650 kati yao walikuwa na unene kupita kiasi.