Hatari nyingine vyuoni

Muktasari:

  • Wakati sheria za nchi zikikataza utoaji mimba bila sababu za kitabibu, mbinu mpya za kutekeleza uhalifu huo zinaibuka kila kukicha, huku kundi la wanafunzi wa vyuo likionekana kinara kwa vitendo hivyo, Mwananchi limebaini.


Dar es Salaam. Wakati sheria za nchi zikikataza utoaji mimba bila sababu za kitabibu, mbinu mpya za kutekeleza uhalifu huo zinaibuka kila kukicha, huku kundi la wanafunzi wa vyuo likionekana kinara kwa vitendo hivyo, Mwananchi limebaini.

Idadi kubwa ya wanaotoa mimba, hasa wanafunzi, wanadaiwa kutumia dawa aina ya misoprostol, licha ya kuwa hiyo ni kinyume na matumizi yake halali.

Kulingana na Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika Wizara ya Afya, Dk Ahmad Makuwani, misoprostol ziliingizwa nchini mwaka 2004 kuzuia damu inayotoka kwa mwanamke baada ya kujifungua na si kutoa mimba kama inavyotumika na wengi.

Dawa hizo ambazo pia hutumiwa kama kwa matibabu ya vidonda vya tumbo zimeelezwa ni biashara kubwa katika maduka ya dawa yaliyopo karibu na maeneo ya vyuo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya kutoa mimba

Mwananchi lilipotembelea baadhi ya maduka ya dawa yaliyopo karibu na vyuo kadhaa jijini Dar es salaam, alielezwa ni ngumu kuzipata dukani ikiwa utazitaja kwa jina lake.

Mhudumu katika moja ya maduka hayo lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam, alisema dawa hizo ni maarufu kwa jina la ‘dawa za kusafisha tumbo’, neno ambalo hutumika kuficha uhalisia wa matumizi hayo haramu.

“Kaka yangu kama unahitaji miso (misoprostol) usiseme nataka dawa ya kutolea mimba, mimi nakusaidia tu kwa sababu nakuona una shida, lakini hizi zinaitwa dawa za kusafisha tumbo,” alisema muhudumu huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

Alipoulizwa kwa nini wamezipatia jina hilo, alijibu ni hofu ya kubainika na mamlaka zinazodhibiti matumizi haramu ya misoprostol.

Katika duka jingine, muhudumu alikana kuwa nazo dukani kwake na kudokeza kuwa angeweza kuzipata kwa kuwasiliana na aliyenazo baada ya dakika chache, angeweza kuzileta.

“Nipe muda kidogo nawasiliana na mwenzangu anazo lakini ni Sh60,000. Mimi siziuzi ila namjua anayeuza nitakusaidia tu,” alisema.

Alieleza kuwa dawa hizo zinadaiwa kutumika kutoa mimba ya kuanzia mwezi mmoja hadi mitatu lakini zaidi ya hapo yupo mtaalamu anayefanya kazi ya kutoa kwa gharama ya Sh200,000.

“Atameza usiku kabla ya kulala, hakikisha ameshiba ataona siku zake (hedhi) kwa wiki moja, baada ya hapo zitakata, damu zikiendelea kutoka baada ya wiki utakuja kuniona, hiyo dawa anayokuletea inatoa na kusafisha,” alielekeza.

Aidha, katika duka la dawa lililopo barabara ya Mandela, eneo la Uhasibu jijini Dar es Salaam, mhudumu alisema dawa hizo ndiyo nguzo kuu ya biashara dukani hapo.

Mbali na dawa hizo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa maduka mengi ya dawa yaliyopo maeneo ya karibu na vyuo, hujihusisha pia na uuzaji wa dawa za P2 kwa ajili ya kuzuia mimba.


Walichokisema wanafunzi

Kati ya wanafunzi waliohojiwa na Mwananchi, wote walikiri kuifahamu dawa hiyo kwa matumizi ya kutolea mimba badala ya matumizi yake sahihi ya kuzuia damu inayotoka baada ya mwanamke kujifungua.

Mwanaidi Kassim (si jina halisi) anayesoma Shahada ya Masoko na Mahusiano ya Umma katika Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT), alisema anazifahamu misoprostol na rafiki yake aliwahi kuzitumia alipotaka kutoa mimba na akafanikiwa.

“Rafiki yangu aliashapatwa na tatizo, ilibidi nishirikiane naye mwanzo mwisho. Tulimuomba huyo mwanaume wake akamnunulie dawa akagoma eti anaona aibu, ilibidi sisi wenyewe twende dukani tukanunua na akatumia mimba ikatoka,” alisema.

Ili kuficha matumizi haramu ya dawa hizo, naye alisema wahudumu wa maduka ya dawa huziita ‘dawa za kusafisha tumbo’ na kwamba, huwezi kupata kwa jina tofauti na hilo.

Mwananidi alisema dozi moja yenye vidonge vitatu, inauzwa Sh50,000 na hiyo inafanya kazi zote kwa maana ya kutoa na kusafisha tumbo.

Caroline Joseph (si jina halisi pia) wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, jijini Dar es Salaam alisema vitisho vya wazazi na ujana ndiyo vinavyowashawishi wanafunzi wengi kutoa mimba.

“Kwa mfano mimi ikitokea nimepata mimba siwezi kwenda nayo nyumbani, baba ameshaniambia nikipata ujauzito nitafute pa kwenda nikirudi kwake ataniua. Siwezi kubaki na mimba, nitatoa tu ili niendelee kusomeshwa,” alisema.

Alieleza kuwa dawa hiyo ndiyo mbinu rahisi, yenye usiri mkubwa katika kufanikisha shughuli hiyo.

Alisema mbali na maduka ya dawa, pia wapo baadhi ya wanafunzi wanaouza misoprostol vyuoni na yeyote anayetaka kutoa ujauzito huzipata kwa Sh40,000 hadi Sh50,000.

“Sijui wanapata wapi, lakini wapo wanafunzi wanaziuza, kuna watu wanapata ujauzito hapa na wanakwenda kununua,” alisema Caroline.

TAHLISO yafunguka

Licha ya kwamba Rais wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO), Frank Nkinda alikiri kuwepo kwa vitendo hivyo, alisema vimegubikwa na usiri mkubwa.

“Hili jambo linafanywa kwa siri, tunaowabaini ni wale wanaotoa mimba kisha wakapatwa madhara, sasa zile pilika za kupelekwa hospitali ndiyo tunagundua, hata hivyo ni vigumu kuthibitisha kuna siri ya hali ya juu,” alisema.

Nkinda ambaye aliwahi kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo cha Ustawi wa Jamii, aliitaka Serikali kuimarisha udhibiti wa upatikanaji holela wa dawa hizo na kuongeza kuwa, zisitolewe bila cheti cha daktari.

Wahadhiri

Dk Zena Mabeyo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, alisema kuongezeka kwa vitendo vya kupata na kutoa mimba kunathibitisha ombwe la elimu sahihi ya afya ya uzazi kwa vijana.

“Kwa sasa watoto wanaogopa zaidi kuzaa kuliko Ukimwi na wengi wanaingia kwenye mahusiano kwa kujaribu, wakipata ujauzito wanakimbilia kutoa,” alisema.

Mhadhiri huyo ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya ustawi wa jamii, alisisitiza umuhimu wa kufanyika utafiti wa kubaini ukubwa wa tatizo la utoaji mimba kwa wanafunzi ili mamlaka zijue wapi zinaanzia kukabiliana na tatizo hilo.

Si kazi yake

Pamoja na kueleza lengo la dawa hizo, Dk Makuwani alisema zina msaada mkubwa katika kuzuia damu nyingi inayotoka kwa wanawake baada ya kujifungua, tatizo ambalo huchangia asilimia 30 ya vifo vya uzazi nchini.

Kuingizwa kwake nchini, alisema kulitokana na dawa iliyokuwa ikitumika awali kutibu tatizo hilo Oxtofin, kuzidiwa uwezo hivyo misoprostol ililetwa kusaidia lakini si kutoa mimba kama inavyotumiwa na baadhi ya watu.

Dk Makuwani alisema mwaka 2010 baada ya maendeleo ya sayansi, misoprostol ilionekana inasaidia pia kusafisha mfuko wa uzazi kwa mimba zilizoharibika.

“Hii inasaidia kinamama walioharibikiwa ujauzito inasafishwa bila kufanyiwa operesheni kama ilivyokuwa awali, kwa hiyo ni dawa inayoendelea kuwepo kwa kazi hizo mbili zinazotambuliwa kitaalamu,” alisema.

Alisema katika maduka ya dawa, misoprostol zinatakiwa kuuzwa kwa mgonjwa anayekwenda na cheti cha daktari tu, huku kwa wagonjwa wa hospitali zinapatikana katika wodi ya uzazi pekee.

Kuhusu kutoa mimba, Dk Makuwani alisema sheria za nchi haziruhusu kufanya hivyo, isipokuwa katika mazingira ambayo ujauzito huo usipotolewa maisha ya mama yatakuwa hatarini.

Isemavyo sheria

Kifungu cha 150 cha kanuni ya adhabu kinasema, mtu yeyote kwa nia ya kuharibu mimba ya mwanamke, akamnywesha au kumfanya mjamzito anywe kitu chochote kinyume cha sheria, au akatumia nguvu za aina yoyote au njia nyingine kumlazimisha anywe atakuwa na hatia na kuwajibika kwa kifungo cha miaka 14 jela.

Aidha, kifungu cha 151 cha kanuni hiyo, kinasema mwanamke yeyote kwa nia ya kuharibu mimba yake kinyume cha sheria, akatumia sumu au kitu chochote kibaya, au akatumia nguvu na njia nyingine yoyote, au akaruhusu kitu kama hicho au njia yoyote kufanyika kwake, atakuwa na hatia ya uhalifu na atawajibika kwa kifungo cha miaka saba jela.

Matumizi holela

Katika hatua nyingine, Dk Makuwani alitaja madhara ya kutumia dawa hizo kinyume na utaratibu wake, ni mimba kushindwa kutoka na hivyo kumuweka mjamzito katika hatari ya kupoteza maisha.

“Hawa ndiyo wanakuja hospitali mimba ikiwa imetoka kidogo, bahati mbaya wanaishia kwenye matatizo makubwa kama mirija kuziba, hali inayoweza kumsababishia mtumiaji ugumba na wakati mwingine saratani ya kizazi,” alisema.


Udhibiti ni hatari

Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alisema Serikali inafahamu kuwepo watu wanaotumia visivyo dawa hizo na kinachofanywa sasa ni juhudi za uelimishaji wa makundi mbalimbali wafahamu matumizi yake sahihi.

“Tunawaeleza kwamba dawa hizi zina hatari kwa matumizi wanayofanya, kuliko kupata mimba zisizotarajiwa tunashauri watumie dawa sahihi za uzazi wa mpango,” alisema.

Alifafanua kwamba wanatamani kuzuia uuzwaji holela wa dawa hizo, lakini dhamira ya kuuzwa kwake ni kusaidia wanaotokwa damu baada ya kujifungua na sio kutolea mimba hivyo ukizuia unawaweka hatarini wenye matatizo.