Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatima ya uhalali wa Tume ya Jaji Lila kuamuliwa leo

Muktasari:

  • Rais aliunda na kuteua makamishna wa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, lakini uteuzi wa makamishna wa tume hiyo umepingwa mahakamani na wananchi wawili. Shauri hilo limepangwa kuamuliwa leo.



Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Kigoma, leo Julai 17, 2026 itatoa uamuzi wa shauri la kupinga uteuzi wa makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Uamuzi huo unatolewa leo na Jaji Wilbert Chuma aliyelisikiliza shauri hilo. Shauri hilo lilisikilizwa Julai 10, 2026 ambapo mawakili wa pande zote walivutana kwa hoja za kisheria kuhusiana na uhalali na mamlaka ya Rais kuunda tume hiyo na kuteua makamishna wake.

Tume hiyo maarufu kama Tume ya Jaji Lila, iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wake ulitangazwa rasmi Mei 18, 2026.

Rais Samia aliunda tume hiyo kutokana na mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, iliyowasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026.

Hata hivyo, uamuzi wake wa kuunda tume hiyo na kuteua makamishna wake ulipingwa mahakamani kupitia shauri hilo la mapitio ya kimahakama (judicial review) lililofunguliwa na mwanaharakati Bubelwa Ephraim Bubelwa na mwenzake Joseph Daudi Mabugo.

Walalamikiwa katika shauri hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, na makamishna wake watatu.

Makamishna hao wa tume hiyo ambao pia ni walalamikiwa katika shauri hilo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.

Katika shauri hilo walalamikaji hao wanaiomba mahakama hiyo itengue uamuzi wa Rais Samia wa kuteua makamishna wa tume hiyo, na kutoa amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.

Pamoja na mambo mengine, wanapinga uamuzi wa Rais wa kuwateua makamishna hao wa tume hiyo wakidai kuwa Rais amefanya nje ya mipaka ya mamlaka yake ya kisheria na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha sheria.

Pia wanadai kuwa uamuzi huo hauna msingi wa kimantiki, unakwenda kinyume na matarajio halali ya waombaji na ya wananchi kwa ujumla, unahusisha matumizi mabaya ya mamlaka ya hiari, na unapingana na masharti ya Katiba.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, mawakili wa walalamikaji waliieleza mahakama kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32 (R.E. 2023), Rais hana mamlaka ya kuunda tume nyingine baada ya Tume ya Jaji Chande kutoa ripoti yake.

Wakili Mpale Mpoki, akisaidiana na Wakili Hekima Mwasipu, alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu cha 21(1)(a) na (b), Rais baada ya kupokea na kuisoma ripoti ya Jaji Chande alikuwa na njia mbili tu za kufanya.

Alifafanua zaidi kuwa Rais, baada ya kupokea ripoti hiyo, alipaswa kuelekeza wale waliotajwa katika ripoti hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.

Pia alidai kuwa Rais hana mamlaka ya kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio ya Kijinai, bali hilo ni jukumu la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Alisisitiza kuwa DPP ndiye pekee amepewa mamlaka ya kikatiba na kisheria, kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Mashtaka, Sura ya 430 (Marejeo ya mwaka 2023), kuratibu na kusimamia upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai bila kujali sheria nyingine zozote nchini.

Hivyo alidai kuwa kama Rais, baada ya kusoma ripoti ya Jaji Chande, anaona kuna haja ya kuchunguza zaidi, anatakiwa kumuagiza DPP kuliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi zaidi.

Mawakili hao walidai kuwa kitendo cha Rais kuunda tume ya kuchunguza matukio hayo ni ukiukwaji wa dhahiri wa sheria na Katiba kuhusiana na mamlaka ya DPP katika masuala ya kesi za jinai.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo, walipinga madai na hoja hizo.

Pamoja na mambo mengine, Wakili Kalokola alidai kuwa alichokiunda Rais ni Tume ya Uchunguzi na si Tume ya Upelelezi.

Alifafanua kuwa Tume ya Jaji Chande katika mapendekezo yake, hasa pendekezo la nane, ilipendekeza iundwe tume nyingine ya upelelezi, lakini Rais aliamua kuunda Tume ya Uchunguzi na kwamba hizo ni tume mbili tofauti.

Wakili Kalokola alidai kuwa kwa sababu hizo, nafuu zinazoombwa katika shauri hilo haziwezi kutolewa, na akaiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo.