Helkopta yatumika kuua nzige
Muktasari:
- Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda na naibu wake, Hussein Bashe wameweka kambi usiku wa kuamkia leo Jumatano Machi 3, 2021 eneo la Engaruka wilayani Monduli Mkoa wa Arusha kusimamia shughuli ya kuteketeza nzige wa jangwani.
Monduli. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda na naibu wake, Hussein Bashe wameweka kambi usiku wa kuamkia leo Jumatano Machi 3, 2021 eneo la Engaruka wilayani Monduli Mkoa wa Arusha kusimamia shughuli ya kuteketeza nzige wa jangwani.
Helkopta ya shirika la kupambana na nzige wekundu ambalo makao makuu yake ni nchini Zambia leo asubuhi imeanza kunyunyiza dawa kuwaangamiza nzige hao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Profesa Mkenda amesema kazi waliyonayo ni kuangamiza kundi la nzige walioingia Wilaya ya Monduli.
"Leo tuko hapa eneo la Engaruka kuongeza kasi ya kuwaangamiza nzige, kama tumemaliza kuwaangamiza nzige hawa Simanjiro tukiweza kupiga sumu leo na kesho tutalimaliza kundi hili na kazi itakayobaki ni kushughulika upande wa Kenya ili nzige hawa wasiingie tena.”
"Nawashukuru sana wakuu wa mikoa pamoja na wakuu wa Wilaya kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa na leo tumelala hapa na helkopta hii itaendelea kubaki hapa mpaka tutakapohakikisha hata yai moja la nzige hakuna," amesema Profesa Mkenda
Maeneo ambayo awali nzige hao walivamia wakitokea nchini Kenya na kuangamizwa ni Wilaya za Siha, Mwanga na Simanjiro.
Februari 19, 2021 katibu mkuu wa wizara hiyo, Gerald Kusaya amesema lipo kundi la nzige zaidi ya milioni 50 walioingia nchini kupitia Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.