Hiki hapa chanzo cha vifo kwa magonjwa yasiyoambukiza
Katibu Mkuu wa TANCDA, Profesa Kaushik Ramaiya akizungumza wakati wa semina ya mkakati wa Wenyeviti na Makamu wenyeviti wa Kamati za Bunge iliyofanyika leo Jumamosi Aprili 25, 2026 mkoani Dodoma.
Muktasari:
- Wakizungumza katika semina ya mkakati wa Wenyeviti na Makamu wenyeviti wa Kamati za Bunge ambayo iliendeshwa na Taasisi ya TANCDA, inayojihusisha na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, wabunge hao wameeleza namna ilivyo ngumu kwa Mtanzania kupima afya kama hajaugua.
Dodoma. Wabunge wametaja moja ya changamoto katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kuwa ni Watanzania kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao.
Wakizungumza katika semina ya mkakati wa Wenyeviti na Makamu wenyeviti wa Kamati za Bunge ambayo iliendeshwa na Taasisi ya TANCDA inayojihusisha na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, wabunge hao wameeleza namna ilivyo ngumu kwa Mtanzania kupima afya kama hajaugua.
Mbunge wa Viti Maalum Christina Mndeme amesema mbali na mazoezi ambayo yamekuwa yakisisitizwa mara nyingi, watu wengi hawataki kupima afya zao na hata wakipima baadhi hawaendi kuchukua majibu.
Mndeme amesema elimu inahitajika hasa katika maeneo ya vijijini ili kila mtu ajenge utamaduni wa kupima afya na kubaini matatizo yakiwa bado kwenye kiwango cha chini.
“Hapa ninachokiona ni ukosefu wa elimu. Kabla ya kuja na wazo la mazoezi na uchaguzi wa vyakula, ni muhimu tupeleke elimu zaidi kwa wananchi, hasa elimu ya saikolojia. Maana ukisema sukari ina shida halafu ukasema asali nayo ina shida, sasa watu wakimbilie wapi?” amesema Mndeme.
Katibu Mkuu wa TANCDA, Profesa Kaushik Ramaiya akitoa mafunzo wakati wa semina ya mkakati wa Wenyeviti na Makamu wenyeviti wa Kamati za Bunge iliyofanyika leo Jumamosi Aprili 25, 2026 mkoani Dodoma.
Mbunge huyo amesema jukumu wanalopaswa kuwa nalo hivi sasa ni kuwa na bajeti itakayowezesha kuwapeleka wataalamu wa lishe kuanzia ngazi ya chini ili wakutane na wananchi na kuwaeleza nini cha kufanya.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kusinim Nuru Mashakari amesema tabia ya kupima afya siyo kwamba inawahusu watu wa vijijini pekee, bali hata viongozi wakiwemo wabunge hawana utamaduni huo.
Kandahiri amesema tatizo kubwa lipo kwa watu wenye majina au wenye vyeo, akieleza kuwa mara kadhaa hujihisi wako salama wakati ni kinyume chake, na ndiyo maana wanajikuta kwenye wakati mgumu matatizo yakiwa kwenye kiwango cha juu.
“Na hasa sisi viongozi, wengi tunakufa na tai shingoni. Mara nyingi hatufanyi uchunguzi (check-up) kujua afya zetu. Hili ni zaidi ya watu wanavyodhani. Fedha nyingi zinateketea kwenye eneo hilo na tusipochukua tahadhari, mbeleni hali itakuwa mbaya zaidi,” amesema Kandahiri.
Katibu Mkuu wa TANCDA, Profesa Kaushik Ramaiya, amesema uwekezaji katika kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza una gharama ndogo, lakini tiba ya magonjwa hayo ina gharama kubwa zaidi kwa nchi.
Profesa Ramaiya amesema taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha asilimia 33 ya vifo vyote duniani husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza, lakini kiwango hicho kinaweza kuongezeka kutokana na mtindo wa maisha wa binadamu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omari Ubuguyu amesema kwa sasa matatizo ya moyo, shinikizo la damu, afya ya akili na magonjwa mengine yanaumiza Watanzania, akitaja sababu kuwa ni maisha ya kukaa bila mazoezi, ulevi kupita kiasi na matumizi ya sigara.
Amesema Watanzania wengi hawapendi kupima afya zao, hata kwa shinikizo la damu ambalo ni kipimo chenye gharama ndogo kuliko vyote, lakini watu husubiri hadi waingie kwenye hatua ya kuugua, na hapo linakuwa tatizo.