Homa ya tamasha la Sauti za Busara yazidi kupanda Zanzibar

Dar es Salaam. Zikiwa zimebakia siku chache, tamasha la Sauti za Busara 2020 kuanza, kwa mara nyingine tena limeandaliwa kwa ajili ya kutoa ladha ya muziki wa Kiafrika katika anga la bara la Afrika huku kukiwa na orodha bora ya watumbuizaji, lengo likiwa ni kusherehekea mkusanyiko wa tamaduni mbalimbali za muziki wa Afrika.

Kama ilivyokuwa kwa matamasha ya Sauti za Busara yaliyowahi kufanyika, jukwaa kuu litakuwa katika eneo la kihistoria la Ngome Kongwe, ambapo watazamaji wataweza kupata burudani ya aina yake ya muziki mubashara kutoka katika majukwaa matatu tofauti.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmud alisema kuna kila sababu ya kusherehekea, ikizingatiwa kuna mkusanyiko wa tamaduni mbalimbali za muziki wa Afrika na fursa zinazoendelea kupatikana kutoka kwenye tamasha hilo.

Tamasha la mwaka huu linaunga mkono juhudi za kukuza muziki unaopigwa mubashara wakati huo huo kukemea unyanyasaji wa kijinsia, suala ambalo linaendelea kutesa tasnia ya muziki na jamii kwa jumla.

Katika Tamasha la Busara mwaka huu linaloanza Februari 13 hadi Februari 16, suala hili la unyanyasaji wa kijinsia litashughulikiwa chini ya kauli mbiu isemayo 'Paza sauti yako, sema hapana kwa unyanyasaji wa kijinsia’.

"Kampeni ya 'PazaSauti' inakusudia kubadilisha mitizamo, kuhamasisha mazungumzo, na kuhimiza heshima kwa wanawake kwa kukuza uelewa juu ya udhalilishaji wa kijinsia. Hivi sasa nchini Tanzania, tunaona ni wanawake wachache tu wanaofanya muziki wa asili na wenye kuvutia. Hii ndiyo sababu kwa tamasha la Sauti za Busara la 2020 tulichagua wasanii kama Siti & the Band (Zanzibar), Thaïs Diarra na MamyKanouté (kutoka Afrika Magharibi), Pigment (Reunion), Evon na Apio Moro (Uganda) na wengine kutoka mkoa wa Afrika Mashariki.

Hawa ni wanawake wenye hisia kali ambao hutumia muziki kufikisha ujumbe na kujielezea. Wakati huo huo, bado wote ni waburudishaji wazuri kwa kupiga (live) mubashara, "alisema.

Alikiri kuwa tamasha moja peke  haiwezi kubadilisha kabisa jamii; hata hivyo, alisema Tamasha la Sauti za Busara linaungana na washirika wenye malengo yanayofanana, kukuza mazungumzo, kubadili mitazamo na kuhimiza hatua dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Alisema muziki wa Afrika haujajikita tu katika burudani; unaweza pia kuwa sehemu ya kuwasilisha ujumbe muhimu.

"Tunatambua jukumu kubwa wasanii wanaloweza kufanya katika jamii, kama wasemaji, wasimulizi, watu wenye maono, wanaharakati na waponyaji. Tamasha hili linaunga mkono uhuru wa kujieleza kwa wanamuziki na hutoa nafasi nzuri ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kufikia hadhira kubwa na nafasi ambazo zinakuza michango yao kwa jamii. ”

Akizungumzia kuhusu Tamasha la Sauti za Busara linalokuja, Meneja wa tamasha hilo, Journey Ramadhan alisema kwa karibu miongo miwili Tamasha la Sauti za Busara limekuwa mstari wa mbele katika kuitangaza Zanzibar na Tanzania duniani, kuvutia watangazaji wa kimataifa na kutoa fursa kwa wanamuziki kuonyesha kazi zao kwa hadhira ya kimataifa.

"Tangu mwaka 2004 wakati tamasha hili lilipofungua milango yake, lengo letu limekuwa kuonyesha muziki ambao ni wa kipekee na wenye utambulisho wa utamaduni. Tumefanikiwa kuonyesha mfululizo kuwa kuna soko na mahitaji ya sauti mpya zinazovutia za asili ambazo ni za kipekee, "alisema.

Orodha ya wanamuziki watakaotumbuiza katika Tamasha la Busara mwaka huu inabeba ladha za muziki wa aina zote na watumbuizaji wengi watakuwa wakitumbuiza kwenye tamasha hilo la Sauti za Busara kwa mara ya kwanza.

Hii ni pamoja na Mehdi Qamoum (Morocco), OumarKonaté (Mali), Blinky Bill (Kenya), GuissGuissBou Bess (Senegal), The Mafik (Tanzania), Ambasa Mandela & The Last Tribe (Kenya), Wakazi (Tanzania), MamyKanouté (Senegal), Onipa (Ghana/Uingereza), Thaïs Diarra (Senegal / Uswisi), Mradi wa Mehdi LaifaouiTrab (Algeria), Sibusiso 'Mash' Mashiloane (Afrika Kusini), NadiIkhwanSafaa (Zanzibar), Siti & the Band (Zanzibar), SeunOlota (Nigeria), Pigment (Reunion), Mannyok (Morisi), FRA! (Ghana), TaraJazra (Zanzibar), Apio Moro (Uganda), IsonMistari aka Zenji Boy (Zanzibar), Kaloubadya (Reunion), Lulu Abdalla (Kenya), Mapanya Band (Zanzibar), SinaUbi & Zawose Ghost Group (Tanzania), Evon (Uganda) ), RahatZamaanTaarab Orchestra (Zanzibar), Mopao Swahili Jazz (Tanzania) na wengine zaidi.