Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hospitali ya Hanang' kukarabatiwa na wadau

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Mkoani Manyara, Janeth Mayanja ameanzisha wiki ya maendeleo wilayani humo kwa lengo la kukusanya michango ya ukarabati wa hospitali ya wilaya hiyo na miradi mingineyo.

Hanang'. Mkuu wa wilaya ya Hanang' Mkoani Manyara, Janeth Mayanja amepokea mifuko 200 ya saruji, ndoo 15 za rangi na mchanga lori 73 kutoka kwa wadau wa maendeleo ili vifaa hivyo visaidie kukarabati miundombinu ya Hospitali ya wilaya hiyo ya Tumaini.

Mayanja amepokea vifaa hivyo katika viwanja vya ofisi yake ikiwa ni uzinduzi wa wiki ya maendeleo ya wilaya hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Novemba Mosi hadi Novemba 5.

Akizungumza leo Oktoba 14 wilayani humo, Mayanja amesema ameamua kuanzisha wiki ya maendeleo ili wadau wa maendeleo wa wilaya hiyo waliopo Hanan'g na nje ya Hanan'g waweze kuchangia vifaa vya ujenzi ambavyo vitasaidia kujenga miundombinu ya hospitali hiyo inayotegemewa na wananchi 350,000 wa wilaya hiyo.

Amesema mifuko 200 ya saruji wameipokea kutoka kwa kampuni ya Bonanza LTD ya Hanang' kama sehemu ya kuanzia, ndoo 15 za rangi kutoka kwa kampuni ya Ngano limited na mchanga lori 73 kutoka kwa HLH Mulbadaw Limited.

Amesema vifaa hivyo walivyotoa wadau ni mwanzo mzuri anategemea kupata mwamko zaidi wiki ya maendeleo ikianza ambapo kila kundi la wadau litakuwa na siku yake.

"Kampuni za kibiashara, wafugaji, wafanyabiashara na wadau wengine wote watashiriki kwenye uchangiaji huu ili tujenge Hanang' yetu," amesema Mayanja.

Amesema ameamua kufanya hivyo ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ambazo anazifanya kwenye kuleta maendeleo katika sekta ya afya.

Amefafanua kuwa kila mwaka serikali inatoa zaidi ya Sh1 bilionni kwa ajili ya hospitali ya Tumaini.

Meneja wa kampuni ya Bonanza Ltd, Akon Clement amesema kampuni yao ni ndogo ila kila wakipata kidogo wanarudisha faida kwenye jamii inayowazunguka.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hanang' Rose Kamili amempongeza Mayanja kwa kuwa na maono mazuri ya kuwakutanisha wadau wa maendeleo.

Kamili ameahidi halmashauri hiyo kutachangia sh30 milioni ili zisaidie ukarabati wa hospitali ya wilaya hiyo ambapo zinaweza kuwalipa mafundi.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Hanang' Mathew Darema amempongeza Mayanja kwa kazi ngumu anayofanya katika kuhakikisha wanapiga hatua na kusonga mbele.

Darema amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea kiongozi mwenye maono ambaye ameanza kwa kasi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo.