Huduma nyeti za intaneti zilivyosimama

Muktasari:

  • Miongoni mwa walioathirika ni watu wanaouza bidhaa mtandaoni, wanaofanya kazi za mtandaoni, watoa huduma za kijamii na wengine kushindwa kutuma maombi ya kazi kutokana na kukosekana huduma hiyo.

Dar es Salaam. Licha ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kueleza jitihada zinafanyika ili intaneti irejee kama kawaida, jana na leo hali haikuwa shwari kwa utoaji huduma zinazotumia mtandao huo zikiwamo zile nyeti.

Miongoni mwa huduma hizo ni malipo kwa njia ya simu, kutoa fedha benki, tiba mtandao na elimu mtandao.

Taarifa ya TCRA iliyotolewa leo Jumatatu Mei 13 2024  na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Jabiri Bakari inaeleza kuwa, “jitihada za haraka zimefanyika na zinaendelea kuchukuliwa na watoa huduma wote ikiwamo kutumia njia mbadala... huduma zilianza kurejea kuanzia jana tarehe 12 Mei 2024 kwa baadhi ya watoa huduma.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, upatikanaji wa huduma ya intaneti kwa kutumia njia mbadala utaendelea kuimarika kwa kadiri uimarishaji wa njia hizo kwa kila mtoa huduma unavyoendelea.

Awali, mamlaka hiyo ilieleza kuwa, tatizo hilo lililoanza juzi asubuhi limesababishwa na hitilafu kwenye mkongo wa mawasiliano baharini wa Kampuni za SEACOM na EASSy kati ya nchi za Msumbiji na Afrika ya Kusini.

Tatizo la kukosekana kwa mtandao wa intaneti na upatikanaji wa kiwango cha chini umeathiri nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.

Miongoni mwa walioathirika ni watu wanaouza bidhaa mtandaoni, wanaofanya kazi za mtandaoni, watoa huduma za kijamii na wengine kushindwa kutuma maombi ya kazi kutokana na kukosekana huduma hiyo.

Ubalozi wa Marekani nchini, leo umetoa taarifa kuwa, kwa wenye maombi ya Visa na mahojiano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika jana, leo na kesho yamesitishwa mpaka itakapotolewa tarehe nyingine.

Kwa mujibu wa ubalozi huo, huduma zitabakia kwa wanaokwenda kuchukua raia wa Taifa hilo wenye dharura.


Huduma za afya

Mmoja wa wagonjwa aliyefika hospitalini kupatiwa matibabu leo amesema alishindwa kusubiria mtandao.

“Nimefika nikaambiwa hakuna mtandao nikaondoka sasa ningesubiri kutafuta nini.”

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Patrick Mvungi amesema changamoto zaidi ipo katika tiba mtandao ingawaje bado wanaendelea kutoa huduma.

“Kwa upande wa huduma za tiba mtandao bado tunaendelea nazo, huduma hazijasimama lakini zinakwenda kwa kasi ndogo ikilinganishwa na ilivyokuwa siku za kawaida,” amesema.

Mvungi alisema japokuwa wanatoa huduma bado kuna changamoto, mtandao wakati mwingine unakuwepo na unatoka.

“Tunaendelea kupambana na hilo, wataalamu wetu wa Tehama wanapambana ili wagonjwa wahudumiwe. Madaktari wapo vyumba vya upasuaji na vipimo vinaendelea kama kawaida kwa kutumia mifumo yetu ya ziada,” amesema Mvungi.


Tiketi na usafiri mtandaoni

Leo na jana, baadhi ya watu walialazimika kurudia utaratibu wa zamani wa kukata tiketi za usafiri, baada ya kuwapo kwa changamoto ya intaneti.

Utaratibu huo ni ule unaomlazimisha mtu kufika ofisi ya basi husika ili kukata tiketi kwa ajili ya safari yake.

“Kila nikijaribu kufungua programu inagoma, nikisema nitumie google haifunguki, inabidi tu ufunge safari kuja huku kutafuta tiketi maana mwisho wa siku safari lazima iwepo,” amesema Amina Mgumba mkazi wa Mbezi.

Amesema hali hiyo walikuwa wameshaisahau kwa kuwa ilisaidia kupunguza muda wa kushughulikia jambo linaloweza kufanyika kwa dakika mbili ukiwa katika shughuli zako za kila siku.

Hata hivyo, Priscus Joseph ambaye ni Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), amesema, “mfumo huu ulivyotengenezwa unaweza kukata tiketi hata ukiwa offline (hauna mtandao), hivyo hatujaathirika kwa kiasi kikubwa, walioathiriwa ni wale wanaotaka kukata kutoka sehemu walipo.”


Teksi mtandao

Mbali na tiketi, pia ilikuwa ni ngumu kwa mtu kuita usafiri kwa njia ya mtandao (Bolt, Uber, Faras, Little Ride) kutokana na mtandao wa kusuasua.

Imani Makongoro ambaye ni mmoja watumiaji wa huduma hizo alisema walilazimika kuhesabu muda waliotumia kawaida ili waweze kupewa bei baadaye baada ya mtandao kugoma.

“Tulipata usafiri lakini kila tukiweka namba za kuanza safari iligoma, mwisho tuliwapigia wahusika wa mtandao na wakatuomba tuanze safari, tuhesabu muda tuliotumia tuwapatie wao watatuambia kiasi,” amesema Makongoro.


Malipo ya bili, benki

Kukosekana kwa mtandao kuliweka ugumu hata ulipiaji wa huduma mbalimbali za taasisi za Serikali ikiwamo faini kwa waliokamatwa na kikosi cha usalama barabarani.

Yahaya Yahaya aliiambia  Mwananchi kuwa baada ya kukamatwa saa mbili asubuhi alisubiri kwa saa mbili  nyingine,  kabla ya kupata risiti ya makosa yake lakini hata alipopewa namba ya malipo (control number) iligoma kulipia.

“Nilipopewa control number nilijaribu kulipia ikagoma,  nilijaribu kwenda kwa mawakala watatu wa huduma za kifedha walisema mtandao wa malipo ya Serikali unasumbua ilinibidi niwapatie fedha taslimu,” amesema bodaboda huyo.

Malipo mengine hususani yaliyohitaji kuhamisha fedha kutoka benki nayo ilikuwa changamoto kwa baadhi ya watu.

“Nimejaribu kujitumia fedha kutoka benki kwenda mtandao wa simu nimekatwa lakini haijanifikia, nilikuwa nahitaji kulipia hoteli na kupata matumizi mengine, nimekwama kwa sababu fedha taslimu niliyokuwa nayo inaniishia,” amesema Devotha Kihwelo ambaye yupo safarini.


Wazee wa kubeti

Shughuli za ubashiri wa matokeo ya michezo (betting) kwa kiasi fulani ziliyumba kutokana na wateja hasa wale ambao huwa wanafanya, hivyo kupitia njia ya mtandao kushindwa kufanya hivyo.

Hali hiyo ilijitokeza hata kwa mawakala wa kampuni za ubashiri wa matokeo ambao hutoaji wa mikeka kwa wateja hutegemea intaneti.

“Nilipanga kubashiri timu tano, ukizingatia ilikuwa Jumapili mechi nyingi, lakini ilishindikana,” amesema mdau huku akikataa kuandikwa jina lake.


Wafanyabiashara, mikutano

Akizungumza na Mwananchi, mfanyabiashara ambaye hakutaka jina lake kuandikwa alisema mbali na kukosa wateja kutokana na kukosekana kwa mtandao,  wameshindwa kutoa huduma kwa watu waliokuwa wakitangaza kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

“Wateja hawawezi kuona bidhaa zetu kutokana na kukosekana kwa mtandao, lakini kuna watu wamelipia ili niwatangazie bidhaa zao katika ukurasa wangu; ni hasara kwao kwa kuwa kiwango cha watu waliopaswa kuona matangazo yao nitakapoweka ni kidogo,” amesema.

Baraka Mafole ambaye ni mmoja wa wauzaji wa maudhui mtandaoni alisema alishindwa kuhudhuria kikao kilichokuwa kikifanyika mtandaoni kutokana na programu (google meet) husika wanayotumia kushindwa kufunguka.

“Mwisho wa siku imebidi tu niombe kuwa sitashiriki kikao kutokana na tatizo la mtandao hivyo nimekikosa,” amesema Mafole.

Issa Banka kutoka Hama Tubebe Technologies na Hama Tubebe logistics, alisema wameshindwa kufanya biashara kutokana na kukosekana kwa mtandao.

“Ili tuweze kukupatia huduma lazima uingie katika programu yetu, uchague aina ya huduma unayotaka halafu utafanyika mchanganuo na utaambiwa bei yake sasa haiwezekani leo siku ya pili inatuumiza sana,” amesema Banka.

Amesema badala yake wameanza kutumia huduma ya simu ya mkononi pekee ambayo ni ngumu kufikia watu wote.

Ugumu huo haukuwa kwao pekee bali hata kwa wanunuzi pia.  “Tangu jana kuna bidhaa nataka kuagiza lakini nikiongea na mtoa huduma ni ngumu kunielewa aina halisi ya bidhaa ninayohitaji, ananiambia ingia katika ukurasa wangu piga picha nitumie nijue, tangu jana, sijapata bidhaa hizo na muda wa kwenda dukani ndiyo sina,” amesema Shani Omary mkazi wa Mbezi.


Ushauri

Akizungumzia changamoto ya mtandao, mtaalamu wa mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Moses Ismail amesema hili linaloendelea, Tanzania inapaswa kujifunza, badala yake kuwa na mbadala wa mkongo utakaosaidia changamoto nyingine ikitokea.

Pia, amesema Serikali inaweza kuangalia uwezekano wa kuwa na satelaiti japo ni gharama lakini itakuwa na msaada wakati changamoto inapotokea.

"Changamoto ya ukosefu wa intaneti ni kubwa na inaharibu biashara nyingi na huduma, mfano nilitaka kwenda kufanya mchakato wa Visa nimeshindwa kwa sababu ya ukosefu wa intaneti," amesema.

Amesema kawaida inatakiwa kuwa na mikongo ya baharini mitatu na mmoja unaweza kuwekea mbali na zilizopo nyingine zilizokaribiana, sina hakika na zilizopo ukaribu wake maana hata mawasiliano hayako vizuri maana yake zipo karibu, kimsingi Tanzania ina miundombinu mibovu ya fiber.

Amesema suluhisho la kudumu ni kuwa na mkongo mbadala kama satelaiti.

“Mfano Kenya wanatumia Etisalat kama mkongo mkuu (haijapata shida hii) na EASSy kama redundancy/backup wao hawajaathirika sana maana link iliyopata shida kwao ni redundancy/backup,” amesema Dk Ismail.

Suala la satelaiti linaungwa mkono na wengi hususani watumiaji kuwa linaweza kuwa suluhu ya changamoto ya mtandao iliyojitokeza kama kuwapo huduma ya mtandao wa intaneti iliyotaka kuanzishwa na bilionea Elon Musk kupitia kampuni yake ya Starlink.

Hata hivyo, alipotafutwa kuzungumzia uwekezaji wa Starlink, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema hakuna aliyeizuia kampuni hiyo kuja kuwekeza nchini.

 “Serikali iko na mchakato wa satelaiti ya nchi. La Starlink waulizeni wao wamefikia wapi mimi sio msemaji wao.”

Akifafanua mchakato huo wa satelaiti ya nchi, Nape amesema  ulishaanza tangu Bunge la bajeti lililopita na kwamba utakapokamilika wananchi wataanza kunufaika nao.

Mei 18 mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa mradi wa minara ya kurusha matangazo ya Televisheni Ardhini (DTT) inayomilikiwa na Kampuni ya Azam Media Limited, alisema Serikali yake imeanza mazungumzo kwa ajili ya ujenzi wa satelaiti.

Endapo mpango huo utakuwa dhahiri, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za Afrika zilizofanikiwa kupeleka kifaa hicho angani, ambazo ni Algeria, Ethiopia, Kenya, Zimbabwe, Afrika Kusini, Morocco, Misri, Ghana na Nigeria na Rwanda.

“Najua kama Serikali tunajipanga kuja na satelaiti ambayo niwahakikishie kuwa itakuwepo Tanzania, tunajipanga vizuri tumeanza mazungumzo tutajenga satelaiti Tanzania,” alisema Rais Samia.